Wednesday, February 8, 2012

DUNIA YETU

Haya ndugu zangu ni JUMATANOnyingine tena na ndio kila KIPENGELE chetu cha marudio mbalimbali. Leo hii nimefika hadi Peramiho nilikuwa nikinunua mikate na nikafungiwa na gazeti la MLEZI.Kufika nyumbani sikulitupa lile gazeti nikawa nalisoma na kukutana na habari hii ambayo ilinivutia na sikupenda ninufaike mimi tu na ndio maana nikaona niiweke hapa leo. KARIBUNI.
Vitendo hivi msibani Mmmhh….!!

Kuna mambo yanayojitokeza na kuonekana wakati wa msiba na wakati wa kuzika. Kwa kweli, yanaleta huzuni Kubwa sana hasa unapowaona waombolezaji kwa njia ya nyimbo, baadhi yao wamelewa pombe, na kuomboleza kwa sauti kali yenye dhihaka isiyolenga hali halisi ya tukio lenyewe la msiba, kana kwamba wapo kwenye sherehe. Wapo watu wanaoitwa kwa jina maarufu “Watani wa jadi” wa msiba ule wakileta mizaha, vicheko na pilika pilika za hapa na pale ikiwa ni pamoja na masimango kwa marehemu. Kama marehemu alikuwa mtu wa Ibada, basi watawaambia wana familia kuwa ndugu yenu yupo kanisani kupeleka sadaka au kwenye Ibada ya jioni au Asubuhi. Kama marehemu alikuwa anakunywa pompe, watasema kuwa ndugu yenu mfuateni kilabuni. Hali kadhalika kama alikuwa mwindaji, watajaribia vile marehemu alivyokuwa akibeba mzigo wa nyama pori, na mambo mengine mengi. Na wakati mwingine huzua tafrani kati ya wanafamilia za marehemu na babu na bibi za marehemu kwa madai kuwa ndio waliomloga ili kulipa nyama waliokuwa wanadaiwa na wachawi wenzao. Kiasi kwamba watani hao wanawaweka wafiwa roho juu juu na hata kushikiana silaha za jadi kama vile rungu, panga, mkuki n.k.
Mnapofika makaburini eneo la kumsitiri marehemu, unawakuta watu wa aina nyingine wanaozungumzia habari za mpira wa Yanga na Simba kama watani wa jadi, kocha Marcio Maximo na timu ya taifa ya Tanzania kwamba yafaa abwage manyanga: mpira wa Manchesta, Chelsia, Arsenal na kadhalika. Watu hao hawasaidii kazi za kumsitiri marehemu na wala kuitikia nyimbo au sala za maombolezo. Wanajisahau kabila. Mikono mfukoni na misimamo ya kimikogo.
Utawakuta mabinti wamevaa nguo zao za kubana, tena fupi. Na juu kitovu kinaonekana wazi kabisa. Wao wenyewe wanajisikia fresh…Wamejipodoa kana kwamba wanaenda kwenye sherehe fulani au disko. Pamoja na kwamba kuna nguo nzuri za heshima, kwa mtu kwenda nazo msibani au kwa watu wa pwani huvaa nguo zao za heshima baibui. Si lazima uvae nguo nyeusi ili kuonekana kuwa umefiwa, lakini ni muhimu kuwa na mavazi yanayotofautiana kabla ya kufiwa na baada ya kufiwa. Hali kadhalika utamkuta mtu anasikiliza simu, tena anazungumza kwa nguvu bila huzuni yoyote, akizungumzia biashara zake zinavyoendeshwa.
Nawasihi wenzangu, tumsindikize mwenzetu katika safari yake ya mwisho kwa nyimbo na sala huku wenyewe tukiwa katika hali ya Ibada . Tena, haipo sababu ya kuanza kubishana wakati wa kuzika tunapomshusha marehemu kaburini. Kama kuna kitu hakipo sawasawa kwa mfano, kaburi halikuchimbwa kadiri ya vipimo vya sanduku, tuelezane kwa taratibu na heshima. Tusipige kelelse kama vile tupo kilabuni, sokoni au mnadani
Na Pius C. Nyoni: Likusanguse-Namtumbo.

5 comments:

sam mbogo said...

utani wa makabila na makabila husika hauwezi epukika. sema tu sikuhizi hasa maeneo ya mijini mambo ya misiba yamebadirika sana,ukianzia na mavazi,huduma zitolewazo msibani, mfano,muziki wa kukodi, video, chakula pia makaburini sikuhizi mpaka matenti yana wekwa,makochi. kwa kweli sasa hivi nigharama sana msiba kwa wenye nazo.kaka s.

Rachel Siwa said...

Misiba ya leo inagharama sana,tena wakati wa kuuguza pesa hizo hazipatikani,kwani zingeweza labda kuokoa maisha ya marehemu,hilo la Watani hahahaaah kaka yangu alikuwa hajui kama kuna mambo ya watani,tulipofiwa na baba kwani ndiyo Msiba wa kwanaza mkubwa ndani kwetu,Watani wakaanza kuiga mzee na kumwambia kaka yangu avue viatu n.k weweee mbona alitaka kurusha ngumi,mama na ndugu wengine wakamwambia aache kwani ni mila.Duuhh lakini inauma sana umefiwa na mpendwa wako wawo wanahitaji pesa na kukutania.

sam mbogo said...

Bisikuti yangu,Rachel umenena,mambo ya watani wajadi,hasa mijini wengi huwa wanakuwa nahasira kama huyo bro wako.najaribu kukumbuka kama mnyamwezi nimtani na mhehe au mbena kwa sababu kuna mama mmoja wa kibena huniitaga,mtani.! haya nisomo zuri sana leo tumepata. kaka s.

ray njau said...

Hapa kuna maadili ya kimungu na utamaduni wetu.Utata ni pale mwingiliano wa majukumu unapokutana na vigezo na masharti vya wakati husika kutozingatiwa na wadau.

Anonymous said...

Nakumbuka wimbo wa Kingoni:
We mdala wangu
Tihamba kumsiba
Wihwala ngemayi
Ya msopi saba
maana yake nini?
Da Yasinta wafasirie basi.