Ilipoishia ”Usiwe na hofu, baba kizee enenda kwa amani sasa.” Baba Kizee alirejea kwa mkewe mzuri. Lo! Akaona nini?
Jumba zuri na barazani mkewe amesimama , amevaa vazi la maridadi la nyoya jema.
Na kichwani kavaa kilemba kilichotariziwa vilivyo na vito vyema vikimning´nia
shingoni. Na pete za dhahabu zilipamba vidole vyake na viatu vyororo vyekundu
vikimkubali miguuni….NA SASA INAENDELEA…………
Na mbele yake watumishi wakimhangaikia,
huku akiwavuta nywele zao na kuwacharaza bakora. Baba kizee akamsaili mkewe
mzuri “Je, waonaje sasa mke wangu sasa roho imeridhia kibibi? Mkewe akamjibu
kwa jeuri , na kumpeleka mazizini kufanya kazi za suluba huko.
Wiki moja ilipita iklifuatwa na
nyingine. Na mkewe mzuri akiwa haridhiki kupita siku zote. Akamwamuru baba
kizee aende tena baharini. “Enenda tena baharini ukamkabili samaki mkuu mwambie
sitaki kuwa mwanamke wa basaba bora bali malkia mwenye enzi!”
Baba kizee akaona vi mno akadahili kwa
nguvu. ”Nini tena, ew mwanamke! La hasha umechanganyikiwa! Kumbuka ya kuwa wanena na kutenda. Kama
mke wa mvuvi utaifanya milki nzima ilemewe na kicheko!”
Mke wa mvuvi akazidi kisirani akamvuta masikio mumewe na kusema ”unathubutuje
kubishana . Ewe kisonoko na mimi mwanamke wa nasaba bora? Elekea hivi sasa baharini nakuamuru!
Kama hutaki, nitakuburura hadi huko!” Baba kizee alijizoazoa na kwenda tena
baharini. Bahari ile ya maji ya mbingu ikawa nyeusi tii, tena inatisha.
Akapaza sauti yake, akaita na samaki wa dhahabu akaja akiogolea.
”Ni nini tena kinachokukera. Ewe baba kizee, hebu niambie!” Kwa mwinamo wa
hadhi baba kizee alijibu sawia ”ujaliwe neema Ewe Bwana wa Samaki! Mke wangu
mzuri amecharuka tena safari hii ajipa wazo hatakuwa tena mwana wa nasaba bora.
Yu ataka kuwa Malkia mwenye enzi.” Naye samaki wa dhahabu akajibu ”Usijali, ewe
baba kizee rejea nyumbani kwa amani nawe utamkuta mkeo mzuri yu malkia!”
Baba kizee alirejea kwa mkewe mzuri na nini alikiona? Jumba lla
kifalme, likimilikiwa na mwanamke wa hila akiwa ametamakani mezani. Wakuu na
mabwana wakimngojelea, wakimnywesha mvinyo kwenye chombo cha dhahabu huku
akividonadona vipande vinono vya nyama. Huku walinzi wenye macho makali
wakimlinda pande zote wakiwa wamejihami kwa vishoka mikononi. Baba kizee
akatupa jicho huku na huko. Jicho likamfeli, akagwaya! Alijiinamia hadhi
ardhini mbele yake na kuweza kutoa maneno haya ”Heshima kwako na kicho Ewe
malkia habe niambie sasa ikiwa moyo wako umeridhika?” Mkewe hakumthamini hata
kwa mtupo wa jicho bali aliamuru watu wake kumuondolea mbali. Ndipo waungwana
na wa nasaba bora wakamwelemea mbiombio wakamkwida shingoni. Na kumbeba
hangahanga na mabawabu wa mlangoni wakamsindikiza nje kwa vishoka vyao.
Na halaiki yote kwa jumla yao wakajisheheni kwa kicheko. ”Hiyo
ndiyo tosha yako ewe kizee mtovu wa busara! Na hilo liwe funzo lako kujijua
wewe u nani siku za hapo baadaye! Na hivyo wiki ikayoyoma na nyingine ikafuata.
Mama kizee akazidi utakavu, akatuma wajumbe wake kumkamata baba kizee.
Walimpata, wakamleta mbele ya Malkia. Naye mke mzuri akanena kwa mumewe ”Enenda
tena ukasujudu kwa samaki mkuu. Sitaki tena kuwa Malkia mwenye enzi, bali
nataka kutamalaki maziwa yote na bahari na katika vina vya bahari. Nitaweka
ngome yangu na huyo samaki wa dhabu atanitumikia mimi. Huku nikimtuma kotekote!”
Baba kizee hakuthubutu kupinga kauli ya mkewe hivyo akaenda tena baharini na
tazama! Tufani kuu ilitokea mawimbi makuu yaliinuka kumlaki, tetemeko tupu,
muondoko wa ghasia, muungurumo mkuu hata hivyo baba alipaza sauti na kuita. Na
samaki wa dhahabu akaja akiogelea ”kulikonit ena baba kizee njoo unieleze!” Kwa
mwinamo wa hadhi baba kizee akajibu sawia ”Na ujaliwe neema Ewe Mkuu wa Samaki!
Nimfanyeje huyu mwanamke? Huyu ajuza mjinga, hataki tena kuwa Malkia pia
anataka kutawala maziwa na bahari. Anataka kuweka ngome zake katika vilindi vya
bahari, na kukufanya wewe mwenyewe umtumikie. Na kukutuma wewe huk ona huko.”
Samaki wa dhahabu alitulia tuli pasi na jibu na badala yake alipiga mkia wake
majini akajerea kwenye maji makuu. Baba kizee alisimama ukingoni, akisubiri .
Alisubiri kwa muda mrefu, lakini halikuja jibu. Hatimaye akarejea kwa mkewe
mzuri, na tazama! Akamkuta amekaa mekoni kwenye kibanda kikongwe cha udongo na
miti na mble yake kukiwa na kibeseni kilichoraruka hadi katikati. HADITHI
IMEKWISHA..
Je Hadithi hii inatufunza nini?
2 comments:
Hadithi imemalizika kwa furaha na nderemo na wenye masikio wamesikia na kuhifadhi mambo yote mema na kamwe tusiwe wenye kukosa shukrani kwa kile kidogo tunachopata na tusinge tamaa kwenye mambo makubwa yaliyo nje ya uwezo wetu.
Kaka Ray!!naungana nawe. Tamaa ni mbaya sana...na ni wengi husahau sana kushukuru na kuridhika walichonacho au walichojaliwa.
Post a Comment