Monday, July 23, 2012

Tuendelee na ile yetu …….HADITHI HADITHI…..HAPA NI HADITHI YA MVUVI NA SAMAKI WA DHAHABU!!!



Ilipoishia ”Usiwe na hofu, baba kizee enenda kwa amani sasa.” Baba Kizee alirejea kwa mkewe mzuri. Lo! Akaona nini? Jumba zuri na barazani mkewe amesimama , amevaa vazi la maridadi la nyoya jema. Na kichwani kavaa kilemba kilichotariziwa vilivyo na vito vyema vikimning´nia shingoni. Na pete za dhahabu zilipamba vidole vyake na viatu vyororo vyekundu vikimkubali miguuni….NA SASA INAENDELEA…………
Na mbele yake watumishi wakimhangaikia, huku akiwavuta nywele zao na kuwacharaza bakora. Baba kizee akamsaili mkewe mzuri “Je, waonaje sasa mke wangu sasa roho imeridhia kibibi? Mkewe akamjibu kwa jeuri , na kumpeleka mazizini kufanya kazi za suluba huko.
Wiki moja ilipita iklifuatwa na nyingine. Na mkewe mzuri akiwa haridhiki kupita siku zote. Akamwamuru baba kizee aende tena baharini. “Enenda tena baharini ukamkabili samaki mkuu mwambie sitaki kuwa mwanamke wa basaba bora bali malkia mwenye enzi!”
Baba kizee akaona vi mno akadahili kwa nguvu. ”Nini tena, ew mwanamke! La hasha umechanganyikiwa! Kumbuka ya kuwa wanena na kutenda. Kama mke wa mvuvi utaifanya milki nzima ilemewe na kicheko!”
Mke wa mvuvi akazidi kisirani akamvuta masikio mumewe na kusema ”unathubutuje kubishana . Ewe kisonoko na mimi mwanamke wa nasaba  bora? Elekea hivi sasa baharini nakuamuru! Kama hutaki, nitakuburura hadi huko!” Baba kizee alijizoazoa na kwenda tena baharini. Bahari ile ya maji ya mbingu ikawa nyeusi tii, tena inatisha.
Akapaza sauti yake, akaita na samaki wa dhahabu akaja akiogolea. ”Ni nini tena kinachokukera. Ewe baba kizee, hebu niambie!” Kwa mwinamo wa hadhi baba kizee alijibu sawia ”ujaliwe neema Ewe Bwana wa Samaki! Mke wangu mzuri amecharuka tena safari hii ajipa wazo hatakuwa tena mwana wa nasaba bora. Yu ataka kuwa Malkia mwenye enzi.” Naye samaki wa dhahabu akajibu ”Usijali, ewe baba kizee rejea nyumbani kwa amani nawe utamkuta mkeo mzuri yu malkia!”
Baba kizee alirejea kwa mkewe mzuri na nini alikiona? Jumba lla kifalme, likimilikiwa na mwanamke wa hila akiwa ametamakani mezani. Wakuu na mabwana wakimngojelea, wakimnywesha mvinyo kwenye chombo cha dhahabu huku akividonadona vipande vinono vya nyama. Huku walinzi wenye macho makali wakimlinda pande zote wakiwa wamejihami kwa vishoka mikononi. Baba kizee akatupa jicho huku na huko. Jicho likamfeli, akagwaya! Alijiinamia hadhi ardhini mbele yake na kuweza kutoa maneno haya ”Heshima kwako na kicho Ewe malkia habe niambie sasa ikiwa moyo wako umeridhika?” Mkewe hakumthamini hata kwa mtupo wa jicho bali aliamuru watu wake kumuondolea mbali. Ndipo waungwana na wa nasaba bora wakamwelemea mbiombio wakamkwida shingoni. Na kumbeba hangahanga na mabawabu wa mlangoni wakamsindikiza nje kwa vishoka vyao.
Na halaiki yote kwa jumla yao wakajisheheni kwa kicheko. ”Hiyo ndiyo tosha yako ewe kizee mtovu wa busara! Na hilo liwe funzo lako kujijua wewe u nani siku za hapo baadaye! Na hivyo wiki ikayoyoma na nyingine ikafuata. Mama kizee akazidi utakavu, akatuma wajumbe wake kumkamata baba kizee. Walimpata, wakamleta mbele ya Malkia. Naye mke mzuri akanena kwa mumewe ”Enenda tena ukasujudu kwa samaki mkuu. Sitaki tena kuwa Malkia mwenye enzi, bali nataka kutamalaki maziwa yote na bahari na katika vina vya bahari. Nitaweka ngome yangu na huyo samaki wa dhabu atanitumikia mimi. Huku nikimtuma kotekote!” Baba kizee hakuthubutu kupinga kauli ya mkewe hivyo akaenda tena baharini na tazama! Tufani kuu ilitokea mawimbi makuu yaliinuka kumlaki, tetemeko tupu, muondoko wa ghasia, muungurumo mkuu hata hivyo baba alipaza sauti na kuita. Na samaki wa dhahabu akaja akiogelea ”kulikonit ena baba kizee njoo unieleze!” Kwa mwinamo wa hadhi baba kizee akajibu sawia ”Na ujaliwe neema Ewe Mkuu wa Samaki! Nimfanyeje huyu mwanamke? Huyu ajuza mjinga, hataki tena kuwa Malkia pia anataka kutawala maziwa na bahari. Anataka kuweka ngome zake katika vilindi vya bahari, na kukufanya wewe mwenyewe umtumikie. Na kukutuma wewe huk ona huko.” Samaki wa dhahabu alitulia tuli pasi na jibu na badala yake alipiga mkia wake majini akajerea kwenye maji makuu. Baba kizee alisimama ukingoni, akisubiri . Alisubiri kwa muda mrefu, lakini halikuja jibu. Hatimaye akarejea kwa mkewe mzuri, na tazama! Akamkuta amekaa mekoni kwenye kibanda kikongwe cha udongo na miti na mble yake kukiwa na kibeseni kilichoraruka hadi katikati. HADITHI IMEKWISHA..
Je Hadithi hii inatufunza nini? 

2 comments:

ray njau said...

Hadithi imemalizika kwa furaha na nderemo na wenye masikio wamesikia na kuhifadhi mambo yote mema na kamwe tusiwe wenye kukosa shukrani kwa kile kidogo tunachopata na tusinge tamaa kwenye mambo makubwa yaliyo nje ya uwezo wetu.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Ray!!naungana nawe. Tamaa ni mbaya sana...na ni wengi husahau sana kushukuru na kuridhika walichonacho au walichojaliwa.