Thursday, March 15, 2012

Uganda yaanza 'kutibu watoto wanaosinzia'

Watoto Uganda, wanakumbwa na,

ugonjwa usiojulikana chanzo wa 'kusinzia'

Uganda imefungua vituo vya afya vya kwanza maalum kwa kusaidia maelfu ya wattoto ambao wana dalili za ugonjwa ambao haujajulikana chanzo chake wa 'kusinzia.’
Vituo hivyo vilivyo kaskazini mwa nchi, ambako ugonjwa huo umeenea, vinakusudiwa kudhibiti dalili mbaya za ugonjwa huo.
Chanzo cha ugonjwa huo hakijajulikana lakini unawapata watoto pekee, wanaoshambuliwa na dalili za kudumaa kiakili na kimwili na kusinzia.
Kuna taarifa za ugonjwa huo kuwa upo nchi za Sudan Kusini na Tanzania.
Kudhibiti dalili
Zaidi ya watoto 200 wenye ugonjwa huo walijitokeza Jumatatu kwa ajili ya matibabu katika vituo hivyo katika wilaya za Kitgum, Pader na Ramor, Kamishna wa Huduma za afya nchini Uganda Dr Anthony Mbonye aliiambia BBC.
Wafanyakazi wa afya hawawezi kutoa tiba yoyote maalum mpaka madaktari wagundue chanzo halisi cha ugonjwa huo –lakini Dr Mbonye anasema wamewapa mafunzo kusaidia maisha ya watoto kwa kudhibiti dalili za fadhaa kwenye mfumo wa neva.
Dawa za kupambana na kifafa zimekuwa na nguvu kutibu wagonjwa wa kusinzia, kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani.
Ugonjwa wa kusinzia unasababisha watoto kufaidhika na kutetemeka na hatimaye kufa.
Mwandishi wa BBC mjini Kampala Ignatius Bahizi anasema mbunge wa jimbo hilo Beatrice Anyor, amekuwa akiongoza kampeni kwa serikali kushughulikia zaidi tatizo hilo ambalo anasema limesababisha wasiwasi mkubwa maeneo ya vijijini.
Wizara ya Afya nchini Uganda imerekodi matukio 3,000 ya ugonjwa huo na karibu vifo 200 vimetokea tangu mwaka 2010.

No comments: