Wednesday, August 8, 2012

MISHAHARA HAITOSHI+TUACHE UZEMBE KAZINI

NI ILE JUMATANO YETU YA KIPENGELE CHA MARUDIO NA LEO NIMEMTEMBELEA JIRANI YANGU..SI MWINGINE TENA NI GONGA HAPA. PIA KWA KUJIKUMBUSHA MAONI  YALIYOPITA GONGA HAPA PIA, KWANI NILISHAWAHI KUIWEKA HAPA MAISHA NA MAFANIKIO..ILA NI NZURI MNO..HAYA KARIBUNI....
------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Makala hii nimeipenda ndiyo maana nikaamua kuiomba  Kwani najua nakamilisha lengo lake la kuifanya isomwe na wengi.
Katika nchi yetu ya Tanzania, watu wanalalamika muda wote kuwa mishahara haitoshi. Gharama ya maisha ni kubwa kuliko mishahara. Hata kwa kuzingatia mahitaji muhimu tu, watu wengi wana haki ya kusema kuwa mishahara haitoshi.
Malalamiko ya mishahara kuwa haitoshi yanasikika duniani kote. Hapa Marekani, shida kubwa inayowakabili watu ni kulipa bili na madeni mbali mbali. Marekani ni nchi ya madeni. Kutodaiwa popote ni sifa nzuri katika utamaduni wa Tanzania. Lakini Marekani, sifa inakuja kutokana na umakini wa kulipa madeni. Mishahara ya Wamarekani wengi inaishia kwenye kulipa madeni. Kwa hivi, nao wanalalamika kuwa mishahara haitoshi.
Wako Watanzania ambao wana mishahara ambayo ingeweza kutosheleza mahitaji muhimu. Tatizo ni kuwa dhana ya mahitaji muhimu ina utata.
Tunaweza kusema mahitaji hayo ni chakula, malazi, mavazi, matibabu, elimu, na usafiri. Lakini, katika utamaduni wetu, orodha ya mahitaji muhimu ni kubwa zaidi ya hiyo. Kumlipia ada mtoto wa shangazi ni wajibu. Kuchangia gharama ya msiba kwa jirani ni wajibu. Kama una gari, kumpeleka mtoto wa jirani hospitalini ni wajibu.
Kwa msingi huo, hakuna Mtanzania ambaye anaweza kusema mshahara wake unatosha. Suala haliishii hapo. Je, ukitembelewa na marafiki, utakaa nao tu nyumbani na kuongea nao, au unatakiwa kuwapeleka mahali wakapate kinywaji? Je, unaweza kuacha kuchangia gharama za arusi ya rafiki yako?Tukizingatia hayo yote, mishahara haitoshi.
Watanzania wengi wana tabia ya kutumia fedha kwa mambo mengi mengine, ambayo umuhimu wake ni wa wasi wasi, kama vile bia. Kwa Watanzania wengi, bajeti ya bia ni kubwa sana. Kwa mtu anayekunywa sana bia, mshahara hauwezi kutosha. Lakini je, bia ni kitu muhimu namna hiyo?
Kwa upande wa pili, Watanzania tunapaswa kutafakari dhana ya mshahara. Mshahara unapaswa kuwa malipo muafaka ya kazi ambayo mtu anafanya. Kazi ndio msingi. Lakini, kuna tatizo kubwa Tanzania.
Watu wengi hawafanyi kazi kwa bidii. Muda mwingi wanatumia kwenye gumzo. Lakini wanategemea kulipwa mshahara, na wanalalamika kuwa mishahara haitoshi. Je, wanastahili hizo hela wanazopewa kama mshahara? Je, wakiongezwa mishahara, wataongeza juhudi kazini au wataendelea kukaa vijiweni na kupiga soga?
Huku Marekani, watu wanachapa kazi sana. Mshahara unatokana na kazi. Mtu asipofika kazini, halipwi. Akichelewa, malipo pia yanapunguzwa. Kwetu Tanzania mambo si hivyo. Mtu akishaajiriwa, anategemea kupata mshahara wake kila mwezi, hata kama anatumia masaa mengi kijiweni. Je, ni bora kuanzisha utaratibu wa kuwalipa wafanyakazi kwa yale masaa wanayokuwa kazini tu, na kupunguza mshahara kwa masaa wanayokuwa kijiweni?
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------
Nami nataka kuongezea ni kwamba hapa Sweden ni karibu sawa na huko Marekani. Yaani hapa hata kama upo likizo hulipwi, inategemea ni likizo gani. Halafu kama unaumwa na halafu huendi kazini zile ziku mbili za kwanza hulipwi kitu kwa hiyo hapo ukiumwa basi ujue mshahara wako unapungua/unakatwa. Kwa hiyo kwa mtindo huo utakuta hata kama mtu unaumwa unajikaza na kwenda kazini. Kwani mshahara wanaokata ni mkubwa sana na ukizingatia maisha nayo yapo juu.
PANAPO MAJALIWA TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO NA RUDIO JINGINE...KILA LA KHERI!!!!

No comments: