Monday, April 28, 2014

KUFUJWA KWENYE NDOA NI NINI?

Ni wiki nyingine na Jumatatu nyingine tena ya mwisho kwa mwizi huu wa nne! Nimeamka nikiwa na mawazo mawazo basi nikachukua kitabu hiki na kusoma. Kitabu chenyewe kinaitwa MAPENZI KUCHIPUA NA KUNYAUKA. Kilichoandikwa na Munga Tahenan... nikafananisha na wimbo ule wa Remmy Ongala usemao nilidhani nimepata kumbe nimepatikana.... bahati mbaya sijaupata wimbo wenyewe....Habari yenyewe inasomeka hivi:- Karibuni tujadili pamoja.

Ifuatayo ni habari ya mwanamke ambaye aliwahi kuja kwangu kwa ushauri kuhusu ndoa yake: Mama Kotilda Mkataha aliolewa mwaka 1980 na mume msomi aliyekuwa na wadhifa mkubwa kwenye taasisi moja ya fedha ya serikali.

Ndoa hii ilifungwa kwa sababu, Kotlida hakuwa na njia, lakini anasema, tangu wakiwa kwenye uchumba, alikuwa tayari na wasiwasi kama ndoa yao ingekuwa ni ya amani. Anasema, wakati bado wachumba, huyo bwana aliwahi kumpiga kibao kwenye kituo cha UDA kwa kosa la kuchelewa kufika kituoni kama walivyokuwa wamekubaliana.
Ndoa ilikuwa ni ya mateso makubwa hata kabla haijafungwa. Mwezi mmoja baada ya ndoa, Mume alimachisha mkewe kazi kwa kwenda kufanya fujo ofisini kwa bosi wake kwa madai kuwa bosi huyo alikuwa na uhusiano na mkewe. Kotlida alianza kuishi kwa mashrti. Hakuna kutoka, hata kwenda kwa jirani bila kuomba ruhusu na kutoa maelezo marefu kwa nini aende huko.
Kusimangwa, kukosolewa, kuitwa mjinga na mbumbumbu, ikaanza kuwa sehemu ya maisha ya mama huyu, Hali iliendelea hivi na Kotlida akawa anajiambia, kuna siku hali itabadilika. Lakini. kwa bahati mbaya, hali haikubadilika. Wakati anakuja kwangu, alikuwa ameshaanza kuamini kwamba, huenda ni kweli alikuwa anastahili kutendewa vile na mumewe.
Huku ndiko tunakoita kufujwa. Mpenzi mmoja anapomuumiza mwingine kwa kauli zake au limwili, mara kwa mara, tunasema hapo kuna kufujana.
Mpenzi mmoja anapokuwa na mamlaka aliyojipa dhidi ya uhuru na haki ya mwenzake, tunasema hapo imekuwa kufujana. Mara nyingi, wanaofuja ni wanaume. Miongoni mwa matatizo ya ndoa ambayo mtu hashauriwi kuendelea kuyavumulia ni kufujwa. Ndani ya kufujwa kuna maumivu makubwa ya hisia na mwili.
Ni vizuri hata hivyo, nikasema kwamba, neno kufuja ni jinsi ya kuelezea hali hii, ambapo mtu mwingine angeweza kuita matesa katika ndoa, kuonewa katika ndoa au kutumia istilahi yoyote.

Swali langu:- Kwanini alipoona mambo yanazidi hakuondoka?

2 comments:

Anonymous said...

Hii inaitwa mfumo dume. Unajua yote hii ni kukosa uelewa wa haki zake mwanamke, lakini dunia inabadilika na watu wengi siku hizi wana ufahamu kuhusu haki zao hasa wanawake ukilinganisha na kabla ya uhuru. By Salumu.

Bashikulu Mligo said...

Kuhusu habari ya kufunjwa kwenye ndoa ni kweli wengi wanawake wanafujwa sana. Nimejitahidi kwa muda wa zaidi ya miaka ishirini ya ndoa na mke wangu ili nami nisiwe mfujaji kwa mke wangu. Tunapendana na kuaminiana sana.
Najua wana ndoa wengi wameingia kwenye matatizo sana. Haya yanaanza toka wakati wa uchumba, inawezekana wakati huo kila mmoja anakuwa na pupa kwa mwenzake bila kufanya uchunguzi wa maana juu ya mtarajiwa wake. Leo muda haunitoshi kuongea mengi. Nikitulia nitakuja kuongea kwa kirefu na kutoa ushauri kwa wanadoa zilizo mashakani.

Sasa nijibu nilichouliza.