Saturday, April 18, 2009

MAVAZI YA WANAWAKE

Nimelipenda shairi hili kwani linasema ukweli limeandikwa na Katekista Rafael Mlelwa katika gazeti la Mwenge:-

Natembea natazama, ni hali ya kushangaza,
Mitaani akina mama, mambo wanayoigiza,
Wengine watuwazima, inakuwaje nawaza,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Vazi la Mtanzania, tangu kale heshima,
Watu walijivunia, wa lika zote nasema,
Haya nawasimulia, walivaa akina mama,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Suruali mwavalia, mfanane na wazungu,
Asili mwaikimbia, mnanitia uchungu,
Watu wote angalia, mnamdharau Mungu,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Vimini mwajibalia, mwana kama vikatuni,
Nyingine mnapasua, makusudi mapajani,
Mapaja twaangalia, pia na nguo za ndani,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Siketi taiti pia, mitaani mwavalia,
Hiyoni ya kulalia, maungo yaoneshea,
Mitaani mwatembea, watu kwa kuangalia,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Kweli mwatia karaha, moyoni nasononeka,
Singerendi mwavalia, maziwa yanaonekana,
Mitaani mnahaha, kutwa nzima mwazunguka,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Kwa umbo mmeumbika, kwa uzuri asilia,
Uarabu mwautaka, tena kwa kujichubua,
Kama Mungu angetaka, mngekuwa Saudia,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Wengine watu wazima, tena ni wake za watu,
Watoto wenu lazima, watawaigeni tu,
Malazi yao lazima yatakuwa yenye kutu,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Hapa mimi nasimama, naomba mnisikie,
Wanamama wenye hekima, hali hii tukemee,
Hakika mimi nasema, tena isiendelee,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama-

7 comments:

mumyhery said...

mhu mwenzangu!!!

Yasinta Ngonyani said...

Oh karibu sana dada Mumyhery Kibarazani kwangu

Anonymous said...

mhh, sio mchezo, hivi hilo gazeti la Mwenge unalipata vipi huko ughaibuni, nimeyamisi sana haya magazeti mawili: mwenge na mlezi! idumu Peramiho

Simon Kitururu said...

Mmh!

Yasinta Ngonyani said...

Ndugu usiye na jina ni hivi Gazeti la Mwenge ni mpendwa babangu ananiletea.Na pia nilikuwa huko juzi tu:-)

Simon Mmh vp?

Anonymous said...

du sio mchezo, heri yako babako anakukumbuka namna hiyo, hilo gazeti ni zuri sana kwa habari za dini na maisha kwa ujumla, natamani nami ningekuwa nalipata huku kudasi,

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli ni nzuri sana na lina mafundisho mengi sana ya dina na maisha kwa ujumla.pole kwa kuwa kudasi