Tuesday, April 14, 2009

MAISHA YA BINADAMU YANA UTAMU NA UCHUNGU WAKE

Maisha ni yenye ladha ya aina yake. Kwa upande mmoja maisha hayo ni yenye ladha ya utamu na upande mwingine yana ladha ya uchungu na ukakasi. Utamu au uchungu wa maisha hutokana na mambo kadha wa kadha ambayo hutokea maishani.

Maisha huwa na ladha ya utamu pale mtu anapokuwa mwenye siha njema, maelewano mema na wengine, mafanikio katika maisha, hali njema kiuchumi nk. Maisha hayohayo hubadili ladha yake pale mambo yanapokuwa magumu na kukuendea kombo. Ugumu huo wa maisha hutokea pale mtu anapokuwa katika afya mbaya,katika majonzi, msiba, mahusiano mabaya na wengine, kuwa katika mfadhaiko na kushindwa katika mambo mbalimbali ya maisha. Pia mambo mengine yanayosababisha ladha ya maisha kwa amani na upendo katika nchi, vita, hali ya ukimbizi nk.

Mambo kama hayo na mengine ya mtindo huo husababisha maisha kuonekana magumu kubadili ladha yake. Pia yanapomkabili mtu katika nafasi yake mtu huyo hushikwa na mfadhaiko na kusongwa nafsi yake hatimaye hupatwa na jakamoyo na kukata tamaa ya kuishi.

Katika ulimwengu tunaoishi kuna fujo tele. Fujo hizo husababisha ladha ya maisha kuchachuka. Ladha hiyo huyafanya maisha yaonekanane kuwa magumu na yenye kukatisha tamaa. Sasa hivi kuna vilio mbalimbali kutoka kona zote za dunia vitokanavyo na mwenendo wa maisha. Sio mara moja tunasikia redioni na kusoma katika magazeti juu ya kumomonyoka kwa maadili. Kuna maonevu mengi ambayo sasa yanaelekea kwenye kuhalalishwa kama sehemu ya maisha ya kisasa.Ubakaji leo hii umekuwa tu kama hadithi za kuburudisha. Utoaji wa mimba unaoendana bega kwa bega na utupaji wa watoto ni kama vitendewili vya kutengwa na kutegeliwa.

Dunia yetu imetawaliwa na vita na magomvi yasiyo kifani. Vita hivyo husababisha maafa, hali ya ukimbizi na shida nyingine za aina aina. Mfano mzuri ni vita vile vya Demokrasia ya Kongo ilivyosababisha lukuki ya wakimbizi. Tena yapo magonjwa ambayo hayana tiba na ambayo husababisha vifo visivyo na idadi kila siku. Magonjwa hayo huwafanya watu kukosa raha ya kuishi.

Tatizo sugu la madawa ya kulevya linazidi kuota mizizi, pamoja na vyombo vya dola kupiga vita dhidi ya mambo haya ya madawa ya kulevya, wahusika wameziba masikio, hawasikii na wala hawaelewi kitu. Kadiri wanavyozidi kutafuta mbinu za kupunguza au kuthibiti ndiyo kadiri hiyo hiyo biadhara inavyoshika kasi yake. Aidha, matukio ya vifo vya watu wanaojinyonga au kujiua wenyewe kutokana na mifadhaiko ya maisha waipatayo yanazidi siku hadi siku. Ukienda mjini, nako ongezeko la vichaa ni kubwa kiasi cha kutishia amani. Hali ya uchumi nayo huzidi kuwa ngumu siku hadi siku. Wenye uwezo wanazidi kujilimbikizia mali na makabwela wanazidi kudidimia. Rushwa tatizo sugu linazidi kupenyeza zaidi, watoa na wapokea rushwa ni wengi. Katika mtumbwa wa rushwa wako mameneja, madaktari, polisi, wakuu wa vyuo, makarani na hata wangoja malango, hapa ni baadhi tu. Bila rushwa huwezi kupata huduma. Haki iko wapi?

Mambo hayo na mengine mengi ya mtindo huo yanakatisha tamaa ya kuishi. Mtu wa kwanza kukatishwa tamaa ni kijana ambaye ndio kwanza anayaibukia maisha. Kijana anapoibukia maisha anakuwa na ndoto nyingi sana. Matarajio yake hutegemea namna gani ulimwengu utampokea. Lakini sasa anapokumbana na mambo ya aina hiyo ambayo yanakatisha tamaa, kijana anabadilika kabisa na kuwa kama vile hana akili nzuri. Hayo ni masumbuko, mateso, adha na kero kwa walio wengi. Siku za matumaini haziji bali bughudha nyingi zinazidi kila siku.!!!!!!

3 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

mimi naona maisha ni mazuri na ni mema. maisha ni matamu sana mimi nayafurahia. nilipokuwa bado mkristo tuliambiwa kuwa Mungu alipoumba alisema yote ni mema japo hawa (kwa ubunifu wa kike) na adamu wakataka kujua mabaya pia kama wewe ulivyoorozesha mabaya utadhani hakuna zuri lifanyikalo duniani! duh. ubunifu huo.\

hata yesu alitwambia tufurahie kwa kila jambo sasa wewe unatwmbia vijana wanasikitishwa na kukatisha tamaa. amri ya yesu umeiacha wapi?

furahia binti kwani yooooote ni mema. (nanukuu bible)

Yasinta Ngonyani said...

Kamala Ninachotaka kusema hapa ni kwamba:- Kutokana na hali yetu dhaifu ya ubinadamu, maelekeo yetu makubwa ni kukata tamaa. Basi Bwana Yesu kristo anatusihi tusikate tamaa bali tujipe moyo mkuu, naye ndiye kimbilio letu. Yesu mwenyewe alipokuwa kufani katika njia ya mateso alivumilia mateso mpaka mwisho na hatimaye kutuletea sisi ukombozi. Kujipa moyo ni kitu cha msingi na pia kujipa imani.

Albert Kissima said...

Hali ngumu ya umasikini hasa kwa nchi za Afrika inachangia sana kuwepo kwa maovu. Kwa mfano, mauaji ya albino, uporaji ambao mara nyingi hugharimu maisha ya watu, njaa kali, kujinyonga kwa sababu ya ugumu wa maisha n.k, mambo haya yanachangiwa sana na ugumu wa maisha. Juzi juzi tu nilisikia kwenye taarifa ya habari kuwa mama alimwua mwanae kisa alichukua muhogo ambao huyu mama alikuwa ameuweka mahali pengine kwa ajili ya matumizi ya baadae., mwingine alimwua mwenzake kwa kutaka kurushwa shilingi miamoja.
Hakika mambo haya yanasikitisha kwani ni dhahiri kuwa thamani na utu wa binadamu inatoweka siku hadi siku huku vitu vingine kama pesa na mali vikipewa thamani isiyo kifani.