Saturday, September 26, 2009

MBALI NAWE

Nimelipenda hili shairi na nimeona si vibaya kama tukirudia tena kusoma kwani kila mtu kuna mtu ampendaye ambaye yupo mbali na pia katika blog zetu wote tuna nia moja ya kuelimishana.

Jua linapochomoza, kila siku asubuhi,
Hunifanya kukuwaza, unipae kufurahi,
Maneno nayokweleza, ni ukweli si kebehi,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Wewe u sehemu yangu, nuru yangu maishani,
Nilopewa na Mungu, niwe nayo duniani,
Nitayaonja machungu, kama 'tanipiga chini,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Daima uwapo mbali, hata ni kwa siku moja,
Nitakesha mi' silali, nikeshe nikikungoja,
Tukae sote wawili, tufurahi kwa pamoja,
Kuwa mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Huhisi nina adhabu, napokuwa mbali nawe,
Maisha kuniadhibu, hadi nichanganyikiwe,
Wewe nd'o wangu muhibu, sina tena mwinginewe,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Nakuwa mi' na upweke, nazo karaha moyoni,
Nayo maji yasishuke, niyanywapo mdomoni,
Yanifanya nita'bike, nijawe nayo huzuni,
Kuwa mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Nakosa mie furaha, nakumbwa nao unyonge,
Maisha yawa karaha, kunifanya nisiringe,
Wala sifanyi mzaha, nisemayo 'siyapinge,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Sogea kwangu karibu, e pambo la wangu moyo,
Pendo 'silolihesabu, amini niyasemayo,
Ya moyo wangu dhahabu, unipaye pasi choyo,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Shairi kutoka http://fadhilimshairi.blogspot.com/

12 comments:

Fadhy Mtanga said...

Da Yasinta, nakushukuru sana kwa kuliweka kibarazani kwako shairi hili. Ni wema usiomithilika.

Pia nitumie fursa hii kumwambia tena aliye mbali nami.

Simon Kitururu said...

Ningependa kweli kama ningependwa hivi na aliyembali nami:-(

Chacha Wambura said...

Kama alivonena Mtakavitu Simon, nami ningependa saaana kuambiwa hivo lakini yawezekana ni ka usanii fulani vile kama kale ka 'silali nakuota' ama 'nikinywa maji nakuona kwenye glasi' nk.

Lakini lasima nikiri kuwa kati ya 100 waweza usipate hata mmoja ambaye anamanisha akisemacho.

kwa bahati mbaya sina aliye mbali nami labda ningejaribu kumsapraizi...lol!

nyahbingi worrior. said...

nuff nuff respect sister.

Irie.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

nakupenda

Anonymous said...

Dada Yasinta,
Ni kweli ujumbe umefika na inabidi tupate majibu ya hili shairi kutoka kwa huyo aliye mbali.

Upendo daima!

Koero Mkundi said...

Hata mie nimemtumia aliye mbali nami shairi hili...LOL

shukrani kwako kaka Mtanga na dada Yasinta

Mzee wa Changamoto said...

Fadhy. Message delivered Kaka. Usijali. Mkodo, penda pendwa Kaka. Jiulize kama unampenda kama unavyopenda akupende yeye. Kwani na yeye si yuko mbali nawe?? Lol.
Mtani Wambura basi shukuru Mungu kuwa huna aliye mbali. Kwani unakosa mengi matamu yaumizayo. Ndio!! Matamu yaumizayo. Lol.. Nyabhingi Warrior, I man looove ya comments mankind. Short and clear everywhere.. Owa Tata Mushumba Kamala unampenda nani kati ya hao juuu??? Inatisha kiasi!! Uso na jina ubarikiwe huko uliko. Na Da'Mdogo Koero, ati niniiiii??? Yaani Fadhy amwimbie wake wewe utume tuuu. Sasa hisia zako na Ka'Fadhy ni sawa? Ama unakaririshwa penzi????

Mwisho wa siku mie nabaki kuwa mie. Natumia ufundi wa Ka Fadhy kuandika ukweli wa yule nimpendaye kisha namuimbia (japo sauti yangu ni ya tatu kasorobo)
Hahahahaaaaaaaaaaaa. Wikiendi njema nyote.

Blessings

Chacha Wambura said...

mzee ya changamoto, umethema "Kwani unakosa mengi matamu yaumizayo. Ndio!! Matamu yaumizayo", je una ushahidi kama ni matamu yaumizayo?

aidha uondoe kauli yako ama uthibitishe...lol

ama ktk blog hakuna undava kama wa mjengoni idodomia? lol

kama fratera mstaafu, nadhani hakuna kitu kiutamu kiumizacho, ama? vinginevo itakuwa ni kama negation of a negative, au! lol

Yasinta Ngonyani said...

Mapenzi kweli ni kidonda na kuwa mbali na umpendaye ni kweli inaumiza sana roho. Karibuni tena na tena hapa katika blog ya maisha.Kaziiii kwelikweli ila tujue tupo pamoja.

Chacha Wambura said...

Da Yasinta, mbona unanichanganya? Ati 'kuwa mbali na umpendaye ni kweli inaumiza sana roho' sasa hapo ina maana humpendi siyo?

Kwa sababu nilikuwa nadhani kuwa kama unampenda awe mbali ama awe karibu haina tofauti, ama?

Miye nadhani hamu ya binamu kanyama ka hamu ndo huwa tunaichanganya na mapenzi ama upendo...lol!

Yasinta Ngonyani said...

Chacha kumpenda mtu si lazima awe mpenzi au uliyeolewa naye mimi ni mTanzania kumbuka na ndugu zangu na wazazi wangu wote wapo Tanzania kwa hiyo wapo mbali nami kivyote. Sijui umenielewa?