Tuesday, September 22, 2009

WANAUME NA KAULI HIZI: 'HUYO SIO WA KUOA, NI WA KUCHEZEA TU'

Bila shaka wewe msomaji unayesoma hapa utakubaliana na mimi kuwa umeshawahi kuzisikia kauli hizi kutoka kwa wanaume pale anapozungumziwa mwanamke mzuri kwa sura na umbo.

Kwa kawaida vipimo vya uzuri wa mwanamke kwa wanaume vimegawanyika. Wanaume wengi hupima uzuri wa mwanamke kwa sura au umbo, lakini linapokuja swala la kuoa, suala la tabia na mwenendo hupewa nafasi kubwa.

Na ndio maana wakati mwingine unaweza kushangaa kukuta mwanaume ambaye ni hodari wa kuchagua wanawake wazuri, lakini ukija kumuona mke aliyemuoa, utakuta ni mbaya kwa sura na umbo, lakini kwa upande mwingine utakuta mke huyo ni mzuri katika maeneo mengine kama vile, tabia nzuri,upendo, wema, na anayemudu malezi ya watoto katika familia.

Sifa nyingine ni zile za kumkubali mwingine kirahisi, kuwa tayari kusaidia yanapojitokeza matatizo katika familia, mpenda amani na kumfanya mume wake aone kuwa hakukosea kumchagua yeye kuwa mke wake. Kwa kifupi wanawake wa aina hii hata kama wangekuwa ni wabaya kwa sura na umbo bado wako kwenye nafasi ya kuonekana kuwa ni wazuri, na huolewa kirahisi zaidi.

Wanawake wazuri kwa sura na umbo ambao tabia na mienendo yao hairidhishi wako kwenye nafasi kubwa ya kuishi bila kuolewa, na kwa bahati mbaya zaidi wanawake wengi wanaohesabika kuwa ni wazuri, tabia na mienendo yao ni ya kutilia mashaka. Wanaume wengi huvutiwa na wanawake hao kujenga uhusiano nao hasa wa kimwili tu na si vinginevyo, na ndio maana wanawake wazuri kwa sura na umbo wanalo soko kubwa sana kwa wanaume, lakini huishia kuchezewa zaidi kuliko kuolewa.

Wanaume nao kwa upande wao wamejenga dhana kwamba wanawake wazuri sana sio wa kuoa na hivyo kuwaogopa. Wanaamini kwamba wanawake wazuri sana ni wasumbufu, kitu ambacho kina ukweli kwa kiasi fulani. Wanaume wanaamini kwamba wanawake wazuri sana kwa sura na umbo huwasababishia waume zao maradhi ya moyo,shinikizo la damu na wakati mwingine hata kuwafanya kupata matatizo fulani ya kiakili, na hiyo inatokana na waume hao kuwa katika mashaka ya wake zao kuchukuliwa na wanaume wengine wakati wowote kutokana na uzuri wao. Hata hivyo wanawake wazuri nao huwaendesha waume zao wakijua kuwa ni wazuri na soko lao liko juu na waume zao nao huwanyenyekea wakihofia kuachwa.

Na ndio maana usishangae kuona kuwa wale wanawake ambao watu wamekuwa wakiamini kuwa ndio wabaya kwa sura au umbo lakini tabia na mienendo yao ni mizuri ndio wanaoolewa na hata ndoa zao zinadumu, tofauti na za wale wanaoonekana kuwa ni wazuri sana kwa sura na umbo na ambao tabia na mienendo yao si mizuri, ndoa zao hazina umri mrefu.

16 comments:

Fadhy Mtanga said...

Mimi niseme nini? Yote umemaliza weye. Maneno mengi ntaharibu utamu. Habari ndo hiyo.
Usichoke.!

Godwin Habib Meghji said...

kwa hili sina uhakika, itabidi nifanye utafiti kwanza ndio nikubaliane na wewe au kukupinga

Faith S Hilary said...

Nobody is perfect sio...au kila mtu ana kasoro, labda wapo wachache ambao wazuri kwa umbo na kitabia vile vile though ni kama kutaka kwenda kuchimba almasi DAR (lol)...true said sister, mwenzio ana hiki wewe huna na ulichonacho wewe mwenzio hana...

Ramson said...

dada yasinta naomba kwanza nikupongeze kwa mada hii nzuri, maana umepiga bakora kwa wanaume na wanawake.

Labda nikuulize swali dada yangu, hebu ninong'oneze, ili watu wengine wasisikie, hivi na wewe unaangukia katika sifa ipi? maana kila nikiangalia picha yako hapo kibarazani, Mashaallah... umejaaliwa kwa sura na umbo..sasa mzee mzima, baba watoto wako hapati Presha kuwa ataporwa siku moja?.....LOL.

Ni hivi mimi nitatoa maoni tofauti kidogo, kusema ukweli kama unazungumzia wanawake wazuri kwa sura na umbo si kwamba tu wanayo matatizo katika ndoa zao bali pia hata huko mashuleni na vyuoni wana kazi kweli kweli...

Takwimu zisizo rasmi zinaonesha kuwa wanawake wenye sura maumbo mazuri kusoma kwao kunakuwa ni kwa kusuasua sana ukilinaganisha na wale wanawake wanaosemwa kuwa wana sura ngumu, yaani sio wazuri kwa sura na umbo, hawa huelekeza nguvu zao zaidi katika masomo na kwa kuwa hawabughuziwi na wanaume wakware wanakuwa huru na hujisomea kwa bidii na mwishowe hufaulu. lakini wanawake warembo kwa sura na umbo muda mwingi wanahangaikia uzuri wao na kuwa bize na wanaume kwa kuwa soko lao liko juu, kila mtu anawataka, na badala ya kutumia muda mwingi kusoma hutumia muda mwingi kuzunguka na wanaume na matokeo yake wote tunayajua...lakini hata hivyo wsiku hizi wamekuwa ni wajanja sana wengi hutumia miili yao kuwahadaa waalimu au maprofesa kwa kuwapa ngono ili wawezeshwe kufaulu katika mitihani na ndio maana likaibuka neno la Digrii za chupi,msichana anaonekana kabisa hana uwezo darasani lakini mwisho wa siku unamuona amefaulu na kusonga mbele. Digrii za chupi siku hizi ziko kila mahali na hata katika ajira zetu mambo ni hayo hayo....wanatumia miili yao kila mahali kuanzia shuleni, katika ajira mpaka kupanda vyeo..na hili madhara yake wote tunayajua.

Naomba nieleweke hapa sisemi kuwa wanawake wote wazuri kwa sura na umbo wana matatizo hayo, nimesema baadhi yao.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

Ramson na uzuri wa Yasinta, heri mimi sijasema, amina

ila sijui kama kuna wanaume wanaomchezea mwanamke. kama ni kuchezea basi wanachezeana. mkwani wakati mwanaume anamchezea mwanamke anakuwa anafanya nini? si anafurahia mchezo tena anadansi kabisa? si mwanamke (hasa wa mujini) anacheza zaidi? iweje asingiziwe mwanaume> acha hizo

viva afrika said...

m speach less, viva blogers, viva MAISHA.

Mwanasosholojia said...

Leo naona dada Yasinta tumeamka na mawazo yanayofanana, umekwenda mbali zaidi, mi nimeishia jirani kidogo kibarazani kwangu, ila maswali yanabaki yale yale na ugumu wake katika kuyatafutia ufumbuzi...masuala ya mahusiano yana utata wake kutokana na utata walionao wanaoingia katika mahusiano! Hongera dadangu kwa mada nzuri

Master Taji said...

"You cannot find a man who is right, you need to make the man right!"
Huwa nawaambia wadada ambao nawakuta wanahaha na waume zao.
Usemi huu unawafanya wasite kidogo, watafakari kwa makini.
Nakosea nini?
Namkosea ama ananikosea?
Nimeshindwa ama tunashindwana?
Atabadilika kweli? Nitambadilisha kweli? Au nibadilike?

Ndoa ni changamoto, inahitaji kila kukicha utunge mkakati mpya kutokana na "actions, which create equal and opposite reactions". Samahani, hiyo ina tafsiri ya Kiswahili kweli?

Ok, kwahiyo hakuna "right man" je, kuna "perfect woman?"
Usemi utakuwaje hapo sasa?

Je, ni kwanini 'uzuri" unasababisha watu wawe tofauti, wajisikie,wabweteke, wawe wenye dharau na madaha, wajithaminishe zaidi?
Nadhani ni kwasababu almasi hutokana na mkaa, lakini hutoka ng'avu zaidi, yenye thamani zaidi.
Hivyo mtu mzuri hujitenga na kujiona wa thamani na pekee zaidi.

Si ajabu tangu utotoni, mtoto anayeelekea kuwa mzuri atasikia "eh, mtoto mzuri huyu jamani!" kisha atapewa zawadi na kubebwa, atakuwa katikati ya macho na mwangaza wa kila mtu.

Tabia zinazoweza kujijenga ni zile za dharau na tamaa. Wazungu wanaita vanity. Tamaa ya kuwa zaidi ya zaidi. Kujisikia binafsi, kutothamini wengine, kukubali yule tu ambaye atatoa au kugawa vitu na vito vya thamani ya urembo alionao!

Si ajabu, mwanamke na hata mwanaume mzuri huharibika haraka. Ni wachache wanaoweza kujizuia kujisikia.

Kuwa na hakika kwamba utampata mwanamke mzuri na mwema pia, ni sawa kweli na kuchimba almasi Dar es salaam!

Lakini jamani, si tunafahamu kwamba hata almasi inabidi isuguliwe kupata mng'ao safi na unaoipa thamani zaidi?!

Hivyo, ukiopoa kizuri, endelea kusugua mwenzangu, futa vumbi kila dakika, sugua na mate ikibidi na hakikisha unajiona kwenye mng'ao!
Usipojiona, wengine watakuja na vichubulio maalumu....

Albert Kissima said...

Du! Mengi yamesemwa,lakini naimani hayajaisha, hata kama nikiyarudia.


Wanawake wazuri kwa umbo na sura wengi wao wanaishia kuwa na watoto ambao kila mmoja anakuwa na baba yake,huishia kutelekezwa na wanawake wa aina hii ni vigumu sana kuolewa.Kwa hili, ninamifano hai kabisa ya kina dada wa aina hii na maswahibu yanayowakumba, yani ukiwakuta barabarani huwezi tambua kuwa wameshazaa na kuzaa,watoto wanaachwa kwa bibi zao na babu zao, wao wanapeta mtaani.

Unknown said...

Hii mada ya leo dada Yasinta Kaaazi kweli kweli.....
naona walionitangulia wamemaliza kila kitu sina cha kuongeza ila RAMSON, MASTER NA KISIMA.... KAAAAZI KWELI KWELI KWELI.....
Haya mjadala uendelee, naona hapa sijamuona mzee wa changamoto..LOL

chib said...

Nimefurahia maoni ya wadau

Mzee wa Changamoto said...

Beres aliimba akasema "step aside now, another man wants to take over, cause you don't know what you got and now it's time to loose it"
Sina hakika na MAANA ya UZURI, lakini najua kuwa yategemea na upande uliosimama kuangalia uangaliacho. Kwani KUOA na KUCHEZEA vyatofautishwa na nini? MTAZAMO. Unaweza kuchezea unachooa ama kuoa ulichochezea. Kwa hiyo pengine kuoa na kuchezea ni HATUA za KIMTAZAMO anazokuwa nazo mtu na SIO SIFA ANAYOZALIWA NAYO AMA ANAYOAMBATANA NAYO MTU. Anayeonekana kuchezewa hapa, anaweza kuolewa pale na akawa bora kuliko anavyodhaniwa. Kwenye ndoa (poleni ambao hamjazionja) kuna mengi ya kujifunza (kama utakuwa tayari kjifunza) na kama ilivyo kwa kitu chochote kile kihusichacho mtu zaidi ya wewe mwenyewe, kuna kupoteza kitu il uongeze kitu" Na hii yaweza kuwa muda, fikra, upendo, michezo na mengine mengi.
Kwa hiyo asiye tayari kukubaliana na UZURI wa alie mbele yake anaweza kudhani huyo ni wa kuchezea na ni kwa kuwa hajaamua KUPOTEZA FIKRA HIZO ili aweze KUONGEZA FIKRA ZA UZURI WA NDANI ALIONAO ALIYE MBELE YAKE basi atakaa kutotambua thamani ya kilichopo mbele yake.
Hakuna mtu anayeweza kuonesha UZURI WAKE HALISI kwa yule ambaye hana hakika kama ni wake na hakuna anayeweza kutoa kla alichonacho kama hadhani anaweza kuwa salama asipobaki na kitu.
Kwangu kusema kwa "ni wa kuchezea" ni kujidhihirishia kuwa huna uwezo wa kusoma kilicho ndani ya aliye mbele yako.
Na ndoa njema ni ile ambayo Mume na Mke wanajuana mapungufu yao na wanaweza kuwianisha kwa kusaidia wakijua ni wapi pa kumsaidia nani ili awe anavyotaka kuwa. HAKUNA ALIYEKAMILIKA na sote hatuna mapungufu ya aina moja. Kwa maana nyingine ni kuwa ukiwa na mtu , na ukabahatika kukuta wewe ni jasiri katika mapungufu yake na yeye ndiye jasiri katika mapungufu yako hapo utakwa umepata MATCH ambayo itadumu. Lakini kabla hamjajuana hivyo, ni lazima kudhihirishiana na katika "stage" hii ndipo mmoja anapodhani yu-zaidi ya mwingine na kusema huyo hamfai na hawezi kumuoa ama kuolewa naye hivyo ANAMCHEZEA TUUU.
Kama una uhusiano ama unataka kuoa ni lazima ukmbuke kuwa wanasema ndoa inakupa maximuma 80% ya ulichotaraji (kama utawekeza) na nyingine 20% utaziona nje. Suala ni kujitahidi kuchukua hizo 20% kuziweka ndani ya 80%, lakini mara nyingi tunaona watu wanaacha 80% na kukimbilia 20%. Wakitambua hilo, ni KILIO CHA MBWA (MDOMO JUU). Ndio maana mapenzi ya "kimada" huvutia ukiwa na mke na ukimuacha na yeye "anatema".
Ni upungufu wa fikra.
Naacha

PASSION4FASHION.TZ said...

Yasinta hakika leo umeamua kusema,hakika mada ya leo kiboko,haipendelei upande wowote mmm! kama mdau mmoja kasema speechless,sina la kuongeza nitaharibu.

mumyhery said...

kumbe!!!

Yasinta Ngonyani said...

Kwanza nnapenda kusema nimeyapenda sana maoni yenu.Na ninawapendeni wote.
Ni kweli hii mada imekuwa si ya kubagua, nimeandika kwa kuangalia pande zote. Kwani mara nyingi wengi wengi wamekuwa wakisema napendelea upande mmoja.

Nawashukuru wote kwa mchango wenu nami nimezidi kujifunza mengi toka kwenu ambayo sikujua. Ni kweli hakuna hapa duniani aliye sawa kabisa, kila mtu ana kasoro yake.
Ni kweli pia ukiwa na sura nzuru na umbo zuri kazi kwelikweli. lakini mimi sioni kama kuna watu WABAYA na WAZURI. Kama nakumbuka vizuri muimbaji mkongwa dr. Remmy Ongala aliimba kama wewe ni mbaya basi oa mke mbaya na kama wewe ni mzuri basi ou mke mbaya. hapo utakuwa umepunguzi mgogoro wa kusema mimi MZURI na mimi MZURI.

Na mwisho napenda kumjibu kaka Ramson! kwanza asante kwa swali, pili asante kwa sifa uliyonipa, tatu hizo picha zote ni mume wangu ndiye mpigapicha wangu, nne katika ndoa yetu kuna neno liitwalo KUAMIANA. Kuporwa siku moja.....Lol.

karibuni tena na tena !!!!!!

Chacha Wambura said...

Da Yasinta (of course na wadau wengine), hivi yule mwanamziki aloimba ule wimbo ulopigiwa kelele saaaana kuwa 'wanawake wazuriwazuri wameolewa wamebaki manungaembe' alikuwa na maana gani?.

Kwa mujibu wa maada yako wazuri hawaolewi na kwa mujibu wa muziki huo wazuri ndo wanaolewa. Mbona nachanganyikiwa?

Mnijuze wajameni!!!