Thursday, October 30, 2008

KILA MTU ANA NDOTO YAKE KATKA MAISHA

HAPA INAKUJA HADITHI YA JUMA.

Mzee Banzi Kijiwe hujipatia pesa kwa kumlazimisha Juma Kombora kuomba omba mitaani. Wakati mwingine Juma hugoma kuomba mitaani na huwambia Mzee Banzi kuwa anataka kwenda nyumbani kwao Morogoro. Mzee Banzi humpiga sana Juma anapokataa. Juma Kombora ana umri wa miaka kumi tu na pia ni mgeni katika mji wa Zanzibar. Maisha ya Juma ni ya kusikitisha sana na mara nyingi hulala na njaa kwa kuwa Mzee Banzi humwachia pesa kidogo sana.
Juma pamoja na watoto wengine wawili hulala mtaani chini ya usimamizi wa Mzee Banzi. Vijana hawa aliwaleta Mzee Banzi Zanzibar kutoka Morogoro kwa njia ua kuwalaghai wazazi wao.

Juma kabla ya kuja Zanzibar alikuwa anaishi Morogoro na mara nyingi alitumia muda mwingi kuchunga mifugo ya baba yake Mzee Kombora na kucheza mpira wa miguu katika nafasi ya ushambuliaji. Juma alikuwa na ndoto akiwa mkubwa atakuwa mchezaji hodari mwenye uwezo mkubwa wa kupiga chenga za maudhi kama Ronaldo. Lakini siku moja ghafla aliitwa na baba yake na kuambiwa kuwa ataenda Zanzibar na rafiki ya baba yake Mzee Banzi. Mama Juma alifurahi sana siku ya kumuaga Juma maana rafiki wa mume wake, Mzee Banzi, alimpa zawadi mama Juma ya kilo 25 za Maharage na kila 25 za mchele pamoja na vitenge doti mbili. Mzee Banzi na Juma waliondoka Morogoro kwa basi mpaka mjini Dar es Salaam halafu wakapanda boti ya kasi mpaka mjini Zanzibar. Juma alikuwa hajawahi kupanda boti maishani mwake kwa hiyo alifurahi sana kupata nafasi hiyo. Wazazi wa Juma wanaamwamini sana Mzee Banzi na walitegemea atamsaidia Juma kupata kazi nzuri kwenye hoteli za kitalii mjini Zanzibar. Juma hajui wapi atapata msaada amebakiwa na ndoto tu za kuwa huru.

Swali langu:- Kwa nini tunakuwa wapesi kuamini ndugu na marafiki kuwa watatusaidia?.

5 comments:

EDWIN NDAKI (EDO) said...

Yasinta napenda sana simulizi zako.

Nakuomba uanze maandalizi ya kuandika simulizi kwenye kitabi nitakuwa wakwanza kusoma.

Yasinta Ngonyani said...

Edo we mganga wa kienyeji nini mi tayari nimeanza. Asante sana kwa kunitembelea pia kwa maoni

Christian Bwaya said...

Kwa nini tunawaamini ndugu? Kwanza mawili yanawezakana hapa. Kuna wanaowaamini sana ndugu zao kuliko watu wengine (wanaoitwa watu baki.Ukimtajia hata kauhusiano cha mbaali keshafika. Anakuamini kwa asilimia elfu moja. Lakini vilevile wapo watu ambao ukitaja ndugu anabadilika sura. Maumivu. Kumbukumbu mbaya na kadhalika.

Kuwaamini ndugu kunategemeana na namna ndugu hao walivyohusiana nawe tangu hatua za awali.

Hawa wanaowaamini ndugu zaidi wanaweza kuonekana na ahueni kwa maana ya kimahusiano lakini kwa upande mwingine hujikuta wakilemaa kiubunufu kwa madai kwmaba "ah ndugu atafanya" Na matokeo yake ni kupoteza mwelekeo binafsi katika maisha.

Ngoja nisiandike mwenyewe nasubiri maoni ya wengine pia.

MARKUS MPANGALA said...

maswali magumu maswali magumu!!!!! oooh nimekwama. nakubaliana na kaka Bwaya, kwamba ndugu umekua naye, unamfahamu, unamuamini ikiwa naye anafanya hivyo. Ingawa siyo wote wanaoamini ndugu zao, alkini hiyo nadhani iliandikwa iwe hivyo. Hata hivyo ule msmo wa mla nawe hafi nawe ila mzaliwa nawe, nao nautazama katika macho makali kwani inawezekana pia mla nawe akafa nawe. kwahiyo suala la kuamini ndugu atakusaidia ni mfumo jamii ilivyoundwa, hasa sisi waafrika tuna mfumo huo ambao ni imani kama ilivyo imani za kawaida kuhusu jambo. hivi najieleza vizuri? naeleweka kweli? nianze wapi? ngoja nikomee hapa....

Yasinta Ngonyani said...

Bwaya ni kweli kabisa. Binafsi naamini zaidi watu baki.


Na markus ni sahihi umejieleza vizuri ni kweli kabisa usemayo. Asanteni