Tuesday, May 14, 2013

WANANDOA NA KAULI HIZI: HATA VIKOMBE KABATINI HUGONGANA, ITAKUWA SIE?

Je unadhani au kuamini kwamba kuna ndoa ambazo wanandoa wake hawagombani kabisa? Kama unaamini hivyo, basi unajidanganya na labda unaishi katika dunia ya peke yako.
Ni jambo lenye ukweli wa kutosha kabisa kwamba wanandoa wote duniani hutokea kugombana, lakini kugombana huko hutokana na migongano au mizozo ya muda tu ambayo huweza kutatuliwa na pande mbili kama wakiamua kufanya hivyo.
Wewe unayesoma hapa, napenda kukuambia ukweli kwamba usiogope migogoro ya ndoa, kwani hicho ni kitu ambacho kamwe huwezi kukiepuka. Kuna msemo mmoja unatumika sana huko nyumbani usemao, " hata vikombe kabatini hugongana itakuwa wana ndoa?" Hii ina maana gani, ina maana kwamba haiwezekani watu kuishi pamoja halafu msiwe mnatofautiana, na kama ukiona hivyo, jua kwamba hiyo ndoa si salama kwani siku yoyote bomu litapasuka na madhara yake yatakuwa ni makubwa kuliko kawaida.
Kuna watu ambao hata kama wamekosewa na wenzi wao hunyamaza kimya na kumeza hasira zao, wengine huogopa kuwakabili wenzi wao na kuzungumzia jambo linalowakera kwa kuhofia kuonekana kama wana kasoro au ghubu. Jambo hili ni hatari sana.
Kumkabili mwenzi wako na kumwambia hisia zako kama amekukosea au amekwenda kinyume na matarajio yako ni jambao la maana sana katika kudumisha uhusiano. Lakini naomba nitahadharishe kwamba, ni vyema kufanya hivyo bila kumshusha, kubeza au kusimanga kwani hiyo sio dalili nzuri ya upendo.
Inashauriwa kwamba wanandoa au wapenzi wanapokwaruzana inabidi wajadili tofauti zao bila kusigishana, kila mmoja akitaka kuwa mshindi, hiyo haitasaidia kuimarisha ndoa bali itaongeza tatizo. Ni vyema upande unaohusika na tatizo, uwajibike na kuomba radhi kwa ustawi wa ndoa, huo ndio ukomavu.

Kutojadili mgogoro kwa wanandoa na kuupatia ufumbuzi wa tatizo huwafanya wandoa kuwa mbali kihisia, na athari zake ni kuwakuta wanandoa wakiwa wageni wa kila mmoja kwa mwenzake, yaani hakuna mawasiliano, kila mtu na lwake.
Jambo la msingi kwa wanandoa ni kujadili tofauti zao pindi linapojitokeza jambo linalomkera mmoja wa wanandoa, kwani hakuna jambo linaloweza kujitatua lenyewe bila kutatuliwa na wandoa husika. Kuacha jambo lolote bila kulitafutia suluhu ni sawa na kutega bomu, ambapo siku likilipuka madhara yake ni makubwa sana.
Unaweza kukuta mwanandoa anakereka na mambo madogo madogo ya mwenzi wake lakini hasemi, ingawa yanamkera kupita kiasi akitegemea huyo mwenzi wake atajua na kuacha, thubutu…..inapotokea siku yeye amekosa jambo dogo tu na huyo mwenzi wake akamsema, basi atatumia fursa hiyo kuanza kujibu mapigo kwa kueleza yale yanayomkera kutoka kwa mwenzi wake, na hapo itakuwa kila mtu anavutia kwake kama mwamba ngoma………na aamini nawaambia kuwa kamwe hawezi kupatikana mshindi katika jambo hilo, kwani mjadala huo unaweza kutoka nje ya mada kila mmoja akijitahidi kutafuta makosa ya mwenzi wake hata yale yaliyotokea wakati wa uchumba wenu ili mradi vurugu tupu.
Inatakiwa wanandoa wajadili kila jambo linalojitokeza hadi kulipatia suluhu, vinginevyo ni kuichimbia ndoa yenu kaburi la mapema. Wakati mwingine unaweza kukuta mwanamke analalamika juu ya kutoridhishwa kwake na matumizi ya mumewe, na hapo mume naye ataanza kukumbusha juu ya matumizi yasiyo ya lazima yaliyofanywa na mke huko nyuma. Mke naye hataridhika atakumbushia jambo lingine na lingine hadi hata mada iliyokuwa ikijadiliwa inasahaulika.
Jambo lingine ni kujumuisha mambo, matumizi ya maneno kama, mara nyingi, kila wakati au mara kwa mara si mazuri sana. Unaweza kukuta mtu mwenzi wake amekosea jambo halafu mwenzie anamwambia “Kila mara huwa unafanya hivi” au mara nyingi huwa unafanya hivyo…..Hii ni hatari kwa ustawi wa wanandoa, kwani kwa kujumuisha ni sawa na kumwambia mwenzi wako kuwa kila mara yeye ndiye mkosaji.
Kwa haya niliyoyaeleza hapa sina maana kwamba huu ndio muarobaini pekee wa kuimarisha mahusiano kwa wanandoa, bali ni moja ya mambo muhimu kati ya mengi ambayo yakizingatiwa na wanandoa wote basi ndoa yao itakuwa imara Tujadili pamoja………..

6 comments:

ray njau said...

Ikiwa wenzi wanataka ndoa yao idumu, wanapaswa kuwa na maoni yanayofaa kuhusu uwajibikaji. Mara nyingi sinema na vitabu vya hadithi huisha watu wawili wanaopendana wakifunga ndoa na kuishi raha mustarehe, maisha ambayo wengi hutamani sana. Lakini, katika maisha halisi, ndoa si mwisho bali ni mwanzo—mwanzo wa kitu ambacho Yehova alitaka kidumu. (Mwanzo 2:24) Kwa kusikitisha, watu wengi ulimwenguni leo hawana maoni hayo. Watu fulani hulinganisha kufunga ndoa na “kufunga pingu za.” Huenda wasitambue jinsi hilo linavyofafanua vizuri maoni ya wengi leo kuhusu ndoa. Namna gani? Ingawa pingu zinaweza kufunga kitu kwa nguvu kwa muda unaohitajika, zinaweza pia kufunguliwa kwa urahisi.
Wengi leo huona ndoa kuwa ya muda tu. Wanaingia katika ndoa haraka-haraka kwa kuwa wanafikiri itatosheleza mahitaji yao, lakini wanatazamia kwamba watatoka kwa urahisi mambo yakichacha. Hata hivyo, kumbuka kwamba Biblia inapozungumzia kifungo, kama vile kifungo cha ndoa, inatumia mfano wa kamba. Kamba za meli hukusudiwa kudumu, zisikatike-katike wala kufumuka hata kunapokuwa na dhoruba kali sana. Vivyo hivyo, ndoa imekusudiwa kudumu. Kumbuka kwamba Yesu alisema: “Kile ambacho Mungu ameunganisha mtu yeyote asikitenganishe.” (Mathayo 19:6)Ukifunga ndoa, unapaswa kuwa na maoni hayohayo kuhusu ndoa. Je, uwajibikaji wa aina hiyo huifanya ndoa iwe mzigo? Hapana.
Kila mmoja anapaswa kuendelea kuwa na maoni yanayofaa kuhusu mwenzi wake wa ndoa. Kila mmoja wao akifanya yote awezayo kukazia fikira sifa nzuri na bidii ya mwenzake, ndoa hiyo itakuwa yenye furaha na yenye kuburudisha. Je, kuwa na maoni yanayofaa kuhusu mwenzi asiye mkamilifu ni kujifanya kipofu? Yehova hawezi kamwe kuwa kipofu, hata hivyo, sisi hutazamia awe na maoni yanayofaa kutuelekea. Mtunga-zaburi alisema: “Kama ungekuwa unaangalia makosa, Ee Yah, Ee Yehova, ni nani angesimama?” (Zaburi 130:30) Waume na wake pia wanapaswa kuwa na maoni yanayofaa na kuwa tayari kuwasamehe wenzi wao wa ndoa.—Wakolosai 3:13.

NN Mhango said...

Ndoa ni kama kipande cha almasi. Hakuna awezaye kusema kwa uhakika kuwa kipande cha almasi kina rangi zipi. Siamini kuwa wanandoa wote wanagombana. Mara nyingi inategemea ndoa imejengwa kwenye msingi gani. Si lazima kugombana. bila sababu. Sitaki kuwasemea wanandoa. Ila uzoefu wangu ni kwamba si lazima kugombana. Inategemea neno kugombana unalitumia kwa mizania ipi. Kuna kutokubaliana kwenye mambo fulani fulani ambako huwezi kuita kugombana. Sitaki nijisifu ingawa kwangu ugomvi ni sumu katika ndoa. Ndoa kama maisha inategemea mambo mengi. Wapo waliojaliwa kuwa na ndoa tuvu na mulua na wengine vinginevyo. Namshukuru Mungu katika miaka yangu mingi katika taasisi hii naridhika na kushukuru kila uchao kwa nilichojaliwa ambacho hunipa fursa ya kufanya kila nitakacho katika mikakati yangu ya maisha. Omba upate mwenza mwema. Na kama ikitokea ukapata siyo, jitahidi kumrekebisha huku nawe ukijitahidi kurekebishwa pale ulipo na weakness. This is the rule of marriage.

ray njau said...

Hata hivyo, kiburi huwazuia wenzi wa ndoa kusuluhisha matatizo yao. Kiburi huzuia mawasiliano kwa sababu mtu mwenye kiburi hana nia wala ujasiri wa kuomba msamaha. Mtu mwenye kiburi hutoa visingizio badala ya kusema hivi kwa unyenyekevu: “Pole; nisamehe tafadhali.” Badala ya kukubali kwa ujasiri udhaifu wake, yeye husema kuhusu udhaifu wa mwenzi wake. Anapokosewa, badala ya kufuatilia amani, anaudhika, na huenda akalipiza kisasi kwa kumnyamazia kabisa aliyemkosea au kumshambulia kwa maneno makali. (Mhu. 7:9) Kwa kweli, kiburi kinaweza kuiharibu kabisa ndoa. Ni vizuri kukumbuka kwamba “Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwapa wanyenyekevu fadhili zisizostahiliwa.”—Yak. 4:6
Bila shaka, ni upumbavu kufikiri kwamba hatuwezi kamwe kuwa na kiburi. Tunahitaji kutambua sifa hiyo mbaya na kuing’oa haraka. Paulo aliwaambia hivi Wakristo wenzake: “Jua lisitue mkiwa katika hali ya kuchokozeka, wala msimpe Ibilisi nafasi.” (Efe. 4:26, 27)Kutofuata Neno la Mungu kunaweza kusababisha maumivu yasiyo ya lazima. Dada mmoja alisema hivi kwa huzuni: “Pindi fulani, mimi na mume wangu hatukufuata shauri la Waefeso 4:26, 27. Katika pindi hizo, ilikuwa vigumu sana kwangu kulala usiku!” Ni afadhali zaidi kuzungumzia mambo mara moja mkiwa na lengo la kusuluhisha tatizo! Bila shaka, huenda mume au mke akahitaji kumpa mwenzi wake muda kidogo wa kutulia. Pia, ni jambo linalofaa kusali ili Yehova awasaidie kuwa na mtazamo unaofaa. Mtazamo huo unatia ndani kuwa na roho ya unyenyekevu, ambayo itakusaidia kukazia fikira tatizo, badala ya kujifikiria tu na hivyo kufanya hali iwe mbaya zaidi.—Soma Wakolosai 3:12


Sam mbogo said...

Afadhali,kugombana kuliko kusemanasemana,au vimaudhi vidogo vidogo,mfano-wewe hupendi hiki yeye anataka hiki.pia kupishana kauli kutokuwa mnapeana taarifa,endapo kunakitu hakiko sawa ndani ya nyumba(ndoa) tabia ambazo kila binaadamu anazo ziwe za kurthi ama unazo tu zimesababishwa na mazingira yaliyo kuzuguka hasa malezi uliokulia.sasa hivi nilivyo taja kwa ufupi nihatari sana katika ndoa ikiwa huna mawasiliano ya kutosha,napia kama hakuna anaye mkubali mwenzie kwa mapungufu aliyo kuwa nayo. mfano unajuwa kuwa mkeo/mumeo anapenda kujisifia pindipo mpatapo wageni au muwapo mbele za watu. hapo utafanyajje ushasema kila neno kumshauri lakini wapi,utamuacha mtuhuyo etikwasababu ya hali hiyo,inamaana hana mazuri ambayo anakufanyia zaidi ya tabia hiyo?.kwahiyo maji ukiyavulia nguo hunabudi kuyaoga. ndoa nimapambano,afadhali ya ndoa za sasa kuliko za zamani enzi za mama zetu/baba zetu,hasa walio pitia enzi za MWALIMU NYERERE wazazi hao walivumiliana sana hasa mama zetu.ushauri wa nje katika ndoa unakusaidia kuwana mitazamo tofauti,na kuweza kupambanua jinsi watu wengine wanavyo sema au kushauri kuhusu matatinzo ya ndoa,ila uamuzi juu ya tatizo hilo ni wewe yaani nyinyi wa wili mume na mke ndo mnajuwa hasa muziki mnao ucheza.kaka s

Anonymous said...

I just couldn't go away your website prior to suggesting that I actually loved the standard info an individual provide on your visitors? Is going to be back often in order to investigate cross-check new posts

my page ... fast payday loans

Rachel siwa Isaac said...

Duhh...