Mada hii imenigusa sana,,,,nimekuwa muda mrefu nikulalamika sana kuhusu hili yaaani kwanini wasichana waachishwe shule na sio wavukana pia. na kwanini wasichana wasipate muda wa kusoma baaada ya kupata watoto. ..soma hapa china...mada hii nimeiipata http://maendeleonivita.blogspot.se/ soma mwenyewe!!!!
----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
WANAFUNZI
wengi wanaosoma katika shule za sekondari wilayani Tunduru mkoani Ruvuma
wanakatishwa masomo yao wanapofikia kidato cha pili na cha tatu baada ya kupata mimba na kuolewa wakiwa
shuleni.
Hali
hiyo inatokana na historia ya wakazi wa wilaya hiyo ambao ni kabila la wayao
kutokuwa na mwamko katika elimu hasa kutokana na kutoa kipaumbele kwa desturi na
mila za kabila hilo ambazo zinatoa fursa zaidi katika mila potofu za
unyago,msondo na jando kwa wanafunzi wa
shule za msingi na sekondari hali ambayo inaathiri suala zima la
elimu.
Takwimu
ambazo zimetolewa na mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho zinaonyesha kuwa
mwaka 2012 wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na sekondari mwaka huu walikuwa ni
2788 hata hivyo hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu ni wanafunzi 1710 tu ndiyo
walioripoti hali ambayo inakwamisha maendeleo ya elimu.
Flavian Nchimbi kaimu afisa
elimu msingi wilaya ya Tunduru anasema tatizo la mimba katika shule za
msingi zimepungua ukilinganisha na miaka mitatu nyuma kulikuwa na mimba karibu
250 ambapo takwimu za mwaka jana zinaonyesha kuwa katika shule za msingi
zililipotiwa mimba 16 na kwamba kuanzia mwezi Januari hadi Aprili mwaka huu
imeripotiwa mimba moja tu.
Hata
hivyo afisa elimu sekondari wilaya ya Tunduru Ally Mtamila amekiri tatizo la
mimba na ndoa za utotoni kwa wanafunzi wa shule za sekondari kuwa ni kubwa
ambapo wanafunzi wa kike wanakatishwa masomo kwa mimba au kuolewa.
Sarah
Michael(15) mkazi wa Tunduru alikuwa anasoma katika shule ya sekondari Makita
ambapo alipewa ujauzito akiwa kidato cha tatu na mwanaume ambaye alitoroka mara
baada ya tukio hilo hali ambayo ilimfanya aishi kwa shida hadi alipojifungua
salama mtoto wake wa kiume.
“Baada
ya kupata ujauzito niliacha masomo wazazi walinipokea licha ya kupata misukosuko
mingi hasa kutoka kwa baba yangu mzazi,nimejifungua naendelea kumlea mwanangu
katika mazingira magumu sana kwa kweli nakumbuka shule mwaka huu ningekuwa
namaliza kidato cha nne’’,alisema.
Sarah
alisema anapenda sana kusoma lakini wazazi wake hawana uwezo wa kumsomesha hivi sasa hivyo endapo atampata
mtu wa kumsomesha anaweza kuendelea na masomo ya sekondari na kwamba kitendo cha
kupata mimba na kukatisha masomo yake kimetoa fundisho kubwa kwake hivyo hawezi
kurudia makosa ambayo yameharibu ndoto za maisha yake.
Hata
hivyo anasema baba yake ni mwajiriwa wa serikali anafanya kazi ya uaskari
magereza wilayani Mbinga ambaye kitendo cha yeye kukatishwa masomo kilimchukiza
na alitaka mtuhumiwa kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria,hata hivyo
wazazi wa pande zote mbili waliyamaliza
na kufuta kesi.
“Hivi
sasa baada ya mwanangu kukua nimemwomba baba anisomesha ili niweze kuendelea na
masomo,lakini baba bado ana hasira amekataa na kusema ningoje kwanza nijifunze
maisha kwa kuwa mimi niliacha shule na kukimbilia mambo yaliosababisha kupata
mimba naendelea kumuomba radhi baba kwamba sitarudia tena nikipata nafasi ya
kusoma’’,alisema kwa huruma.
Salima
Hamad(15) mkazi wa Tunduru anasema alikatishwa masomo yake baada ya kupata mimba akiwa kidato cha tatu mwaka 2012 na kwamba wazazi wake walichukizwa
na kitendo hicho ,walifungua kesi ya mwanaume aliyempa mimba,alikamatwa na
kutiwa ndani hata hivyo mwanaume huyo ametorokea nchini Msumbuji hadi
leo.
“Wazazi
walinisakama pamoja na viongozi wa serikali ya kijiji,nilitamani kutoa mimba
lakini nilipiga moyo konde,nilivumilia kulea mimba katika mazingira magumu kwa
kuwa wazazi wangu ni masikini hadi nikajifungua salama kwa kufanyiwa upasuaji
mtoto wa kike,natamani kusoma lakini sina uwezo’’,alisisitiza.
Salima
anasema wazazi wake wamekataa kumsomesha na kudai kuwa hawana uwezo wa kumpeleka
tena shule na hivi sasa anaishi kwa kujitazamia na kuuguza kidonda ambacho
kimetokana na kujifungua kwa upasuaji.
Hemed
Ally mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya msingi Frank Weston wilayani
Tunduru anasema katika mafunzo ya msondo
na unyago wanafunzi wa kike wanaelezwa
faida za kuishi na mume lakini hawafundishwi madhara ambayo wanaweza kupata kwa
kushiriki katika ndoa wakiwa wadogo hali hiyo ndiyo inawahamasisha wanafunzi
kujiingiza kwenye ngono na kushawishika kuolewa na kupata mimba wakiwa
wanafunzi.
Rehema
Sara mwanafunzi wa kidato cha nne sekondari ya Mgomba anasema mila za unyago na msondo
zimesababisha wanafunzi wengi wa kike katika shule hiyo kuacha masomo kwa kupata
mimba au kuolewa ambapo hivi sasa katika darasa lao waliofanikiwa kufika kidato
cha nne ni wanafunzi 106 tu kati ya wanafunzi zaidi ya 230 walioanza nao kidato
cha kwanza mwaka 2010.
Sarah
mkombozi wa kidato cha nne sekondari ya Mgomba ambaye alifanyiwa ngoma ya unyago
na msondo akiwa darasa la tatu amekiri moja ya mambo ambayo wanafundishwa katika
msondo na unyago ni kufanya mapenzi na watu wazima
na kwamba kukataa kufanya hivyo ni kuvunja mila na desturi za
wayao’’,alidai mwanafunzi huyo.
“wenzangu
wengi ambao nilikuwa nao shule ya msingi na wengine ilitakiwa niwe nao sekondari
wameacha masomo kwa kuwa wana watoto baada ya kupata mimba na wengine wameolewa
na kuachika hivyo wanaangaika na maisha’’,alisisitiza.
Mkuu
wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho amekiri mila na desturi za kabila la wayao
zinachangia wilaya hiyo kuwa duni kielimu hata hivyo amesema tayari serikali
imeunda kikosi kazi cha kuonana na viongozi wa mila, makungwi na manyakanga
kuwaelimisha juu ya utoaji wa elimu kwa watoto wa kike kupenda masomo tofauti na
sasa ambapo kundi hilo limekuwa likifundishwa kukabiliana na maisha ya ndoa hali
iliyosababisha kuwepo kwa matukio mengi ya ndoa za utotoni wakiwa
shuleni.
“Mila
na desturi za kabila la wayao kuwafanyia unyago wanafunzi ndiyo chanzo kikuu cha tatizo hili,sisi kama
serikali ili kukabiliana na tatizo hili tumefanya vikao na viongozi wasiokuwa
rasmi lakini wanakubalika katika jamii wakiwemo makungwi, mangariba,
masultani,mamwenye,mashehe na maimamu kwa kuzingatia tumejadili kwa pamoja
tatizo hili”,anasisitiza.
Kwa mujibu wa
Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wasichana 8000 kila mwaka
huacha shule kutokana na ujauzito. Kati yao 3,000 ni wanafunzi wa shule za
msingi.
Kila siku,
wanawake 24 hufariki dunia kutokana na mimba au wakati wa kujifungua. Wanawake
watano mpaka sita wanaofariki kati ya hao ni watoto wadogo, watoto hao hufariki
dunia kwa kuwa miili yao haijakomaa vya kutosha kwa ajili ya
kujifungua.
Naibu
mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Watoto
(UNICEF), Mohamed Safieldin anasema mbali na athari hizo, pia virusi vya ukimwi
(VVU), vinavyosambaa kwa kasi kwa wasichana hao. Tanzania kuna watoto yatima
milioni 1.3 walioathirika kwa ukimwi.
4 comments:
Kuna mtu mmoja wa hekima, alisema watu wawili mombaji na muombwaji,je wapo sawa?
Muombaji akiomba, je ni lazima apewe?
Na je muombwaji akiombwa ni lazima atoe?
Muombwaji akitoa, na akapata madhara kwa kutoa kwake, anastahili adhabu sana na muombaji?
Ukiangalia haya maswali yana maana yake.
Lakini ninachotaka kusema ni kuwa ni wakati muafaka, akina mama, kuwa na lengo moja, hasa kuwafunda watoto wetu wakike, kukataa...kusema NOOOO. Pili kuwa na mikakati ya kuzuia vile vinavyosababisha ushawishi,....
Huenda ni rahisi sana kuliongea hili kwa mdomo kuliko vitendo. lakini kwa wazazi linatuhusu sana, hasa tulio na watoto wa kike ambao ndio wanadhulumiwa. Kwani likitoka hilo la kutokea atakayeumia ni mwanamke, mwanaume, hayupo hapo. sasa kipi bora, kufanya yale yatakayokulinda au kujiweka huru, nusu uchi yakukute, eti kwa vile ni `uhuru', ni haki binafsi.
Ni kweli watoto kuwafunda hadi wajue madhara ya hilo jambo, ni vigumu sana. Na hasa kwa kipindi hiki cha utandawazi, kwani vishawishi ni vingi sana, na ukizingatia maadili ya dini, hasa ya kujihifadhi ili kuondoa tamaa za kimwili, hayazingatiwi, na hili la kujihifadhi linachukuliwa kama ni kuzalilisha, tunasahau madhara yake, ambayo ndio huko kubakwa, kushawishi nk.
Ni mtihani kwa kweli-kweli, lkn kijumla kunahitajika kubwa na hukumu kuwa sawa, kwa aliyempa huyo mtoto uja uzito. Mtoto wa kike yeye keshaadhibiwa kwani atafukuzwa shule, atabeba mimba miezi tisa.
Ni bahati mbaya kuwa rais wao aliyewaahidi maisha bora kwa wote alisema eti wanapata mimba kutokana na kiherehere chao. Ajabu hakuona kiherehere chake cha kupokea kila upuuzi wa sera toka nchi za magharibi uliomsukuma kuiweka rehani nchi yetu. Ni ajabu kuwa hakuona kiherehere chake cha kupenda kuzurura badala ya kutulia ofisini na kusoma na kutatua matatizo ya wananchi. Ni bahati mbaya kuwa hakuona kiherehere chake cha kuwateua marafiki zake katika kulipana fadhila ukiachia mbali kuwavumilia na kuwakingia kifua pale wanapovurunda. Hakuna kiherehere chake cha kuendelea kuwa na mwaziri walioghushi shahada kama vile Makongoro Mahanga, Mary Nagu, Emanuel Nchimbi, Matayo Matayo na William Lukuvi bila kusahau balozi Deodorus Kamala na Meya wa jiji la Dar Didace Massaburi almaarufu Makalio.
Hili ni janga letu sote na kwa pamoja tuwawezeshe wahanga wetu.
Habari kama hii nimeanza kuisikia tangu nilipopata akili, inasikitisha sana kusoma/kusikia bado mpaka leo. Kinachoniuma zaidi ni pale wasichana wanapopata mimba na kutelekezwa na wavulana kuachiwa na kuendelea na masomo. Na baada ya hapo msichana akisha zaa anataka kurudi tena shule anakataliwa eti yeye ni mama/amezaa nani alisema aliyezaa hawezi kusoma tena? ni sheria hiyo kweli?...Na mpaka ikajengeka katika jamii eti hakuna haja kumsomesha mtoto wa kike..
Post a Comment