Sunday, April 8, 2012

Neno La Leo: Yesu Akasema; " Simon, Acha Kuvua Samaki, E Nenda Ukawe Mvuvi Wa Watu"

Ndugu Zangu,

Bwana Yesu alipotembelea mto Galilaya, aliwakuta wavuvi wakivua samaki, Simoni alikuwa ni miongoni mwa wavuvi hao. Yesu akasema; " Simoni, acha kuvua samaki,nifuate ukawe mvuvi wa watu. Naam. Watu wengi wanaangamia kwa kukosa uelewa. Kwa kutojitambua. Wanahitaji ukombozi wa kifikra.

Na siku zote, haki uinua taifa, vivyo hivyo, dhulma huangamiza taifa. Na mahala pasipo na haki, basi, hapo hapatukuwa na amani.Oneni, maovu yametamalaki katika dunia tunaoishi. Siku zote, kujipendelea ndilo shina la maovu.

Si tuna mifano hai. Oneni, wale wenzetu waliokaa na wakaamua kuuza nyumba za Serikali. John Magufuli ni mmoja wa watu hao. John alisimamia utekelezaji wa dhulma ile kwa Watanzania. Lililopelekea uamuzi wa hila na ghilba wa kuuza nyumba za serikali ni ubinafsi na hulka ya baadhi ya viongozi kutaka kujipendelea.

Karibu wote waliouziwa au kujiuzia nyumba hizo za Serikali, nyumba za wananchi, tayari walikuwa na nyumba kabla. Siku zoe, hamu inakuwa ni jambo jema, endapo binadamu ataweza kuitawala hamu/tamaa yake.

Wanadamu tusipoitawala hamu yetu, tukaanza kujipendelea, kuwasahau wengine, basi, hilo huwa ndio chimbuko la maovu. Hupelekea kutoelewana baina ya wanandugu, na hata kwa marafiki walioshibana.

Hupelekea vurugu na machafuko katika jamii. Tunazungumzia uwepo wa upendo, haki na usawa. Dini nyingi zinazungumzia umuhimu wa upendo, haki na usawa katika jamii. Iwe ni Uislamu na Ukristo vivyo hivyo. ”

Naapa kwa zama . Hakika binadamu wote wamo katika hasara isipokuwa wale walioamini na wakafanya matendo mema. Wakahusiana na haki na wakahusiana na subira” (Koran tukufu, Surat ASWR)

Biblia nayo inasema; kuwa Kaini alikuwa mtu wa kujipendelea mno, akamwua nduguye. Mfalme Saulo alijipendelea mno, akamdhulumu Daudi. Yuda alijipendelea mno, akalikubali kumsaliti Yesu kwa Vipande thelathini vya fedha. Hatimaye, akamsaliti Yesu.

Na ufufuko wa Bwana Yesu utukumbushe jukumu letu la kupambana na maovu katika jamii. Utukumbushe jukumu la kusaidia kazi ya kuwakomboa kifikra wanadamu wenzetu. Kama Bwana Yesu alivyomkumbusha Simoni kwa kumwambia; ” Simoni, acha kuvua samaki. E nenda ukawe mvuvi wa watu. Na hilo ndilo Neno la Leo. Pasaka Njema.

Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam0788 111 765http.//mjengwablog.com

No comments: