Wednesday, April 18, 2012

NAMNA YA KUTOKA KWENYE UTUMWA WA NDOA…….

Habari za leo..Ni ile JUMATANO YA KIPENGELE CHA MARUDIO YA MAMBO MBALIMBALI. Leo nimeperuzi kwa kakangu Kaluse na kukutana na hii mada. KARIBUNI TUJADILI KWA PAMOJA.
Sio lengo langu kuwafundisha wanawake namna ya kuachana na wapenzi au waume zao. Lakini hebu fikiria kwamba kila wakati wanandoa au wapenzi wako kwenye vita. Hakuna amani, hakuna masikilizano. Kutwa nzima mtu anawaza kuhusu uhusiano wake mbaya hadi anashindwa hata kufanya kazi. Je, hali kama hii ina maana kwa mtu kuendelea kuwa kwenye ndoa?

Hapa nazungumzia wale ambao wanashindwa kutoka kwenye uhusiano, ambao wanajua kabisa kwamba, unawatesa na kuwaumiza. Kuna sababu nyingi kwa nini watu hawa wanashindwa, lakini nyingine zinatokana tu na kutojua namna ya kutoka, sio utegemezi wa aina yoyote.
Moja ya sababu, ambazo ninaziona sana hasa kwa wanawake ni kujali jamii itasemaje. Mtu anaona kabisa uhusiano haufai na anatamani kutoka . lakini anajiuliza, hivi watasemaje? Kuna wakati ndugu wanamwambia, yeye ndiye mkorofi. Kama hii ndio sababu anachotakiwa kufanya mwanandoa ni kuhakikisha kwamba anajifunza kuishi kama yeye. Nijuavyo mimi, hata wanandugu au jamii hata ikisema vipi, anayeumia au kuepuka kuumia au kuuawa ni yule aliye kwenye mateso ya ndoa
Jambo la kujiliza hapa ni kama, jamii ndiyo inayopigwa, kutukanwa, kutelekezwa au kudhalilishwa? Lakini jambo kubwa zaidi la kufahamu ni kwamba mtu alishaolewa maana yake ni mtu mzima mwenye haki ya kuamua juu ya maisha yake. Akisubiri ndugu wamwamulie, basi huyo bado ni mtoto..
Jambo lingine ni lile la, je nikimwacha nitapata mwingine? kwani wanaume siku hizi ni shida sana? Ni ujinga unaowafanya wengi kuuliza swali hilo. Unahitaji mwingine wa nini? Unahitaji mwingine ili maisha yako yawe ya maana zaidi au? Kama hakuna mwingine ni vyema kwa sababu maana yake ni kwamba hakuna mwingine wa kukutesa. Lakini wanasaikolojia wanaamini kwamba, ‘kila bidhaa ina mnunuzi.’ Kama unataka mwingine, hata ukiwa na miaka sitini utampata. Huwezi kumpata wakati ukiwa ndani ya tanuru la mateso. Ni lazima utoke kwanza.
Kuna wale wanaoshindwa kutoka kwa sababu wanaamini kwamba mwanamke haruhusiwi kutoa talaka. Hi siyo kweli. Kuna wanaoshindwa kutoka kwa sababu dini zao zinakataza kuachana, hii pia siyo kweli. Mwanamke au mwanaume, yeyote anaweza kuomba talaka na ikatolewa, kama kuna sababu zenye kukidhi haja hiyo. Chombo pekee kinachoweza kutoa talaka au kuidhinisha wanandoa kuachana ni Mahakama, siyo dini au taasisi nyingine. Kinachoitwa ‘talaka tatu’ kwa mfano, ni ushahidi tu, na sio talaka.
Kuna wale ambao hawako tayari kutoka kwenye uhusiano mgumu kwa sababu ya mali. Wanaogopa watagawana mali na wenzao, jambo ambalo hawako tayari kulifanya na mara nyingi hawa ni wanaume. Wapo pia wanawake ambao wao ndio waliokuwa watafutaji wakuu. Swali la kujiuliza ni hili. ‘Ni kipi bora, ni mali au ni amani na utulivu na uhai wako?’ kama ni mali, basi hakuna anayeweza kukuingilia kwenye uamuzi wako.
Lakini, kwa ufahamu tu, ni kwamba, pasipo na amani, mali haina maana na pasipo na amani uhai ni wa kubahatisha pia.
Wengine wanashindwa kutoka kwenye husiano kwa sababu wazazi wa mume na ndugu wanampenda sana. Anaogopa kuwaudhi kwa kuondoka kwenye ndoa ya mateso ya mtoto wao na ndugu yao. Anataka wafurahi, hivyo hawezi kuondoka. Huu nao ni upungufu.
Hivi unakuwa umeolewa na ndugu na wazazi au na mume? Lakini, kwani ukiondoka utashindwa kuwa karibu na watu hawa? Hutashindwa na pengine urafiki wenu utakuwa wa kudumu. Ukiendelea kukaa kwenye ndoa ya mateso kuna siku utakosana hata na hawa, maana unaweza ukalipukwa ukamuuwa mtoto au ndugu yao.
Kuna wale wanaoshindwa kutoka kwenye uhusiano mgumu kwa sababu wana watoto na wanaogopa kwamba, watoto wao watateseka. Hivi ni kuteseka kupi kubaya, kule kwa utotoni au ukubwani? Mtoto anayeishi kwenye ndoa yenye vurugu, anaharibikiwa kuanzia utotoni hadi ukubwani. Lakini, hata hivyo kuachana kwa wazazi, sio lazima kuwe na maana ya watoto kuteseka.
Kuna wakati hata watoto wanamwambia mama atoke kwenye ndoa, halafu mama huyo huyo anadai anakaa kwenye ndoa hiyo kwa sababu ya watoto! Kuna haja ya kujiuliza maswali kwa upana zaidi.
Ukitaka kutoka kwenye ndoa ngumu jiulize maswali haya. Je, ndoa hii ni kwa faida ya nani? Je, niliolewa au kuoa ili kupata shida au amani na upendo? Je, bila ndoa,nisingeweza kuishi mwenyewe? Tafuta mifano ya wasio na ndoa ambao wanafurahia maisha.
Jiulize ni kwa kiasi gani wengine wanasaidia kukusukuma zaidi kwenye ndoa hiyo? Jiulize ukamilifu wako. Je, wewe ni nusu mtu au mtu kamili? Kama ni mtu kamili , basi ishi kama mtu kamili. TUONANE TENA PANAPO MAJALIWA JUMATANO IJAYO. UPENDO DAIMA!!

10 comments:

Enzihanse said...

Dada katika hili mimi nipo upande wako, bado kuna wanawake wanakaa kwa wame zao wakiwa na masononeko mapaka wanapata magonjwa ambayo hawakustahili, ukishaona umejitahidi kumrekebisha lakini hakuna mwelekeo epu omba ruhusu uondoke kwa ajili ya mapumziko na baadae umwambie ndio utaishi mwenyewe, najua mbele ya Mungu kila kitu kitafanikiwa

Mfano kuna mama moja jirani yangu mume wake alimpiga mpaka akazimia akiwa kitandani alipozinduka anamka ashuke chini akapigwa teke ndipo alipoanza kusema anakufa wanangu , tabu ni kwamba chuma cha watoto kipo mbali hawakusikia ndipo mume wake alitoka akaenda kuka sebuleni , baadae mama aliweza kutoka chumbani na kuwafuata watoto wake na kuanza kuwaeleza yaliyomsibu mtoto wa kwanza ambaye hupo kidato cha nne akamwambia mama ni heri uondoke ukakae kwa bibi sisi tutakaa na baba hapa , tukipata muda tutakuja kukusalimia, lakini bado mama haelewi , mimi nilishindwa kumuelewa jamani maisha haya acha tu

emu-three said...

Swali kubwa `kwanini ifikie hapo....?' Lazima kuna sababu, huenda hiyo sababu ingetafutwa na kutatuliwa upendo huruma na kuthaminiana kungelikuwepo...
Bado nasema huenda bado hatujajua nini maana ya ndoa, ....kwanini shule, wataalamu wasiichangamkie hii tenda, ili kila waoanao wanapitia hapo, maana ndoa ni sehemu ya kukamilisha maumbile yetu,...sehemu ya mawada na rehema..sasa vipi kuwe ni sehemu ya mateso...kuna kuna sintofahamu,lazima kuna sababu..
Najiuliza tena, kwanini umpige mwenzako...kwanini..kwanini...hulka, chuki kisirani...

ray njau said...

Ndoa ni ndoana ukiwa nayo na ikivunjika inakuachia doa.

Rachel siwa Isaac said...

Duhhh dunia hii,Ngoja leo niwewakujifunza zaidi.Ahsante da'Yasinta kwa shule hii.

sam mbogo said...

Kujifunza ni muhimu,sana my bisikuti!1. ndoa si mchezo kila mtu na jinsi avyocheza karata ndani ya ndoa,usipime. kaka s

ray njau said...

Wapendwa wadau wa kibaraza cha mama maisha narejea hapa nikiwasihi mfahamu kuwa muasisi wa asasi ya ndoa ni Yehova Mungu kutokana na upendo wake kwa wanadamu.Ndoa kama taasisi inatajwa kuwa ni takatifu na wadau wake wanapaswa kuishi kulingana na maandiko matakatifu na siyo kwa dhana na hadithi za kufikirika.Matatizo tunayatengeza wenyewe kwa tamaa za mioyo yetu na mwisho wa siku tunaanza hadithi ya mlevi kukimbia kivuli chake mwenyewe.Mchakato wa ndoa upo wazi kwa jamii na kila mdau anaelekezwa kuzingatia vigezo na masharti kabla ya kuingia katika asasi ya ndoa.Ni kinyume na mapenzi ya Yehova kuingia kwenye asasi ya ndoa kwa ajili ya majaribio.Ni vizuri ifahamike kuwa useja una changamoto zake na ndoa nayo ina changamoto zake.Changamoto zinaposhika kasi katika asasi ya ndoa siyo mapenzi ya Yehova Mungu kukimbia bali kutafuta majawabu kupitia madokezo matakatifu na mwisho wa siku tuige mfano wa dhahabu ambayo kupitia moto huthibitisha uimara wake."NDOA NI NDOANA UKIWA NAYO NA IKIVUNJIKA HUKUACHIA DOA".

ray njau said...

KIELELEZO KWA WAKE

10 Familia ni kama shirika, na ili lifanye kazi vizuri, linahitaji kuwa na kichwa. Hata Yesu anajitiisha kwa Yule aliye Kichwa chake. “Kichwa cha Kristo ni Mungu” kama vile “kichwa cha mwanamke ni mwanamume.” (1 Wakorintho 11:3) Kujitiisha kwa Yesu chini ya ukichwa wa Mungu ni mfano mzuri kwa kuwa sote tuna kichwa ambaye tunapaswa kujitiisha kwake.

11 Wanaume wasio wakamilifu hufanya makosa na mara nyingi wao hupungukiwa katika jukumu lao la kuwa vichwa vya familia. Kwa hiyo, mke anapaswa kufanya nini? Hapaswi kudharau mambo ambayo mume wake anafanya au kujaribu kumnyang’anya ukichwa. Mke anapaswa kukumbuka kwamba roho ya utulivu na upole ina thamani kubwa machoni pa Mungu. (1 Petro 3:4) Akiwa na roho hiyo, itakuwa rahisi kwake kuonyesha utii wa kimungu hata katika hali ngumu. Isitoshe, Biblia inasema: “Mke anapaswa kumheshimu sana mume wake.” (Waefeso 5:33) Lakini vipi akikataa kujitiisha chini ya Kristo akiwa Kichwa chake? Biblia inawasihi wake hivi: “Jitiisheni kwa waume zenu wenyewe, ili, ikiwa wowote si watiifu kwa lile neno, wavutwe bila neno kupitia mwenendo wa wake zao, kwa sababu wamekwisha kushuhudia kwa macho mwenendo wenu ulio safi kiadili pamoja na heshima kubwa.”—1 Petro 3:1, 2.

Sara aliwawekea wake mfano gani mzuri?
Sara akizungumza na Abrahamu

12 Mume awe ni mwamini au la, mke hatakuwa akimvunjia heshima ikiwa ataeleza maoni yake kwa njia ya busara hata kama yanatofautiana na ya mume. Huenda maoni yake yakawa sawa, na yanaweza kufaidi familia nzima ikiwa mume atamsikiliza. Ingawa Abrahamu hakukubaliana na mke wake Sara alipopendekeza jinsi ya kutatua tatizo fulani la familia, Mungu alimwambia: “Sikiliza sauti yake.” (Mwanzo 21:9-12) Bila shaka, mume anapofanya uamuzi ambao haupingani na sheria ya Mungu, mke wake anapaswa kuonyesha anajitiisha kwake kwa kuunga mkono uamuzi huo.—Matendo 5:29; Waefeso 5:24.

13 Mke anaweza kutimiza jukumu lake kwa kutunza familia. Kwa mfano, Biblia inaonyesha kwamba wanawake ambao wameolewa wanapaswa ‘kuwapenda waume zao, kuwapenda watoto wao, kuwa na utimamu wa akili, safi kiadili, wafanyakazi nyumbani, wema, wakijitiisha kwa waume zao wenyewe.’ (Tito 2:4, 5) Mke ambaye pia ni mama anayefanya hivyo, atapendwa na kuheshimiwa daima na familia yake. (Methali 31:10, 28) Lakini kwa kuwa ndoa ni muungano wa watu wasio wakamilifu, huenda hali fulani wasizoweza kuvumilia zikawafanya watengane au kutalikiana. Biblia inaruhusu kutengana hali fulani zinapotokea. Hata hivyo, kutengana hakupaswi kuchukuliwa kivivi hivi tu, kwa kuwa Biblia inashauri: “Mke hapaswi kuondoka kwa mume wake; . . . na mume hapaswi kumwacha mke wake.” (1 Wakorintho 7:10, 11) Msingi pekee wa Kimaandiko wa talaka ni uasherati.—Mathayo 19:9.

Rachel siwa Isaac said...

Nakuunga mkono kaka S my bisikuti!hahahhhah USIPIME.

Yasinta Ngonyani said...

Ahsante wote kwa michango yenu! Mie ngoja nami nitoe dukuduku yangu ambayo naona ni kipingamizi kikubwa sana katika maisha ya ndoa kwa mwanamke ni kwamba:- Wanawake wengi wanakubali kupata mateso kwa kuogopa kuiaibisha familia yake. Yaaani ile kujua binri fulani kaachika si mnajua mila na desturi ni kwamba ni aibu sana na kwamba je nikiachika hakuna atakayemtaka tena na halafu inasemekena labda katika ukoo ule itakuwa kama nuksi na wengine hawataolewa tena...Ila hii yote ni kwa vile imani hii imejengeka.....TUFUNGUKE WANAWAKE KWANI TUNAWEZA KILA KITU...

Anonymous said...

Mimi nimechukuia sana mjadala huu coz muandishi amezungumzia upande mmoja tu, hii inamaanisha kuwa wanawake tu ndio wanaopata mateso katika ndoa, kitu ambacho si kweli, na mateso ya ndoa sio mutukanwa, kupigwa au kunyimwa haki za msingi, unaweza usifanyiwe aina hizi za mateso na bado ukawa na mateso katika ndoa.

Hivyo dada au kaka angu ulietoa ujumbe huu ili tuchangie, ni vyema ukaelezea kijumla jumla ili kupata wachangiaji wengi, na pia kuondoa hisia za kiubaguzi dhidi ya wachangiaji

Ali Mohammed Ali
Zanzibar