Monday, May 24, 2010

VISA VYA HUYU KIUMBE MWANAUME!

'Kwenye swala la mapenzi wanaume hawana mzaha'

Katika Gazeti la Mwananchi la hivi karibuni la May 18, 2010, kuna habari iliyoandikwa na mwandishi Anthony Kayanda wa Kigoma ambayo ilinisikitisha sana. Habari yenyewe ni ile iliyohusu mtu mmoja kuuwawa kwa kuchomwa kisu kifuani kwa tuhuma za kutembea na mke wa mtu.

Kwa mujibu wa Gazeti hilo, tukio hilo limetokea katika kijiji cha Kitagata kilichopo katika tarafa ya Makere, Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma. Marehemu ametajwa kuwa ni Ally Bwisigwa ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.

Ilidaiwa kwamba Marehemu alikuwa akitembea na mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Perusi ambaye aliwahi kuolewa na Hassan Rashid mkazi wa Kasulu Mjini na waliishi pamoja kwa muda mrefu kabla ya mume huyo kufungwa gerezani.

Baada ya mumewe kufungwa, Perusi alirudi kijijini kwao huko Kitagata na ndipo alipoanza mahusiano ya kimapenzi na marehemu.

Inadaiwa kuwa baada ya Mume huyo kutoka Gerezani alimuonya mtuhumiwa mara kadhaa kuacha kutembea na mkewe lakini marehemu aliendelea na mchezo wake huo mchafu.

Inadaiwa kuwa Hassan alifanya majaribio mawili ya kutaka kumuua marehemu kwanza kwa kutaka kumgonga na pikipiki na tukio la pili lilikuwa ni lile la kumchoma kisu ambapo hata hivyo kisu hicho hakikumpata.

Nimesema kuwa tukio hilo limenisikitisha sana kwa sababu bado nashindwa kuelewa hivi inakuwaje mpaka mtu unapoteza maisha kwa sababu ya mwanamke, tena kibaya zaidi mke wa mtu!

Ingawa inasemwa kwamba wanawake ni viumbe wa ajabu lakini naamini wanaume ndio viumbe wa ajabu kupindukia. Kwa nini ninasema hivyo? Ninasema hivyo kwa sababu, wanawake kwa ujumla wao wanavyo vibweka vyao katika swala zima la mapenzi, lakini ukija kwa wanaume naamini nao wanavyo vibwekwa vyao tena vya hatari ukilinganisha na vile vya wanawake.

Kwa mfano, hivi ni mara ngapi tumeshawahi kusikia baadhi ya wanaume wakiamua kujinyonga kwa sababu ya kushindwa kuwashawishi wanawake wanaowapenda?

Namini kuwa matukio ya aina hiyo yapo sana na sio kwa huko nyumbani tu bali pia hata katika nchi zilizoendelea. Linapokuja swala la mapenzi kuna baadhi ya wanaume wanakuwa kama Nyati waliojeruhiwa, na ndio sababu unaweza kukuta baadhi ya wanaume wanajiingiza kwenye vitendo viovu kama vile vya wizi au ujambazi kwa lengo la kuwashawishi wanawake wanaowapenda ili wawakubali. Wakati mwingine hujiingiza kwenye matumizi ya Pombe kupita kiasi au hata matumizi ya Bangi na madawa ya kulevya kutokana na kuachwa na wanawake wanaowapenda.


Tabia hii ya wanaume kuhatarisha maisha au hata kupoteza maisha kama tulivyoona katika tukio hilo la Kigoma ni la tangu enzi za kale. Kuna simulizi nyingi tulikuwa tukisimuliwa enzi za utoto wangu huko nyumbani kwamba kuna wakati wanaume walikuwa wakipigana ili kumgombea mwanamke na shujaa anayeshinda katika ugomvi ndiye anayemchukuwa mwanamke anayegombewa.

Inaonekana wazi kwamba uwezekano wa mwanaume kufa mapema au kuhatarisha maisha yake ni mkubwa ukilinganisha na ule wa wanawake. Na hiyo inatokana na wanaume kupenda sifa na kutaka kuwamiliki wanawake wawapendeo. Kuna matukio mengi ya kusikitisha ambayo huwa tunayasoma katika vyombo vyetu vya habari ambapo matukio kama yale ya mwanaume kumuua mwanaume mwenzie ili kumpata mwanamke ampendae ni vya kawaida kabisa.

Kwa mfano katika tukio hilo la Kigoma, licha na kukoswa koswa kuuwawa mara mbili lakini marehemu hakukoma kutembea na mke wa mwenzie, mpaka akasababisha kupoteza maisha.
Hivi kumekuwa na uhaba wa wanawake kiasi cha kupelekea baadhi ya wanaume kuhatarisha maisha yao au kupoteza maisha kutokana na kumgombea huyu kiumbe mwanamke au kuna kitu kingine kinachotafutwa hapo?

Ni aghalabu sana kusikia mwanamke kamuua mume baada ya kumfumania au kumuua mgoni wake tofauti na wanaume. Kama ukipima jambo hilo kitakwimu basi utapata idadi ya wanaume ya kutosha ukilinganisha na ile ya wanawake.
Kimsingi wanaume wamewageuza wanawake kama mali zao wanazozimiliki na hiyo ndio sababu inapotokea kumfumania mkewe au mchumba wake akiwa na mwanaume mwingine mambo mawili yanaweza kutokea, kwanza atamuadhibu mgoni wake au hata kumuua kisha mke naye atasulubiwa au hata kuuawa.

Lakini, pale anapofumaniwa mwanaume mambo huwa ni tofauti sana. Kuna uwezekano mkubwa wa mke huyo kusulubiwa kwa sababu amemfumania mume na wakati mwingine hata huyo mgoni anaweza kushirikiana na mume huyu kumuadhibu huyo mwanamke aliyefumania.
Nadhani kuna haja ya wanaume kujikagua upya na kubadili mwenendo wao mzima juu ya matendo yao ili kuepuka kupoteza maisha kwa jambo ambalo wangeweza kuliepuka.

11 comments:

Unknown said...

Da Yas hii topiki ni kali na pana sana. Kwa mtazamo wangu ni kwamba suala zima la mapenzi liko so kompliketedi. Matatizo ni kwa wote. Si wanaume peke yao. Vibweka vinarindima pande zote mbili. Wanawake wengi tu wamechemka vikali kunapokuja suala zima la kutaka mapenzi. Pia vituko vingi sana hufanywa na akina mama pale wanapohisi kudhulumiwa mapenzi. Ni hadithi zilizopo katika jamii yetu na maisha yetu ya kila siku. Ni sehemu ya maisha yetu.

Baraka Chibiriti said...

Kwa mtazamo wangu sio mwanaume tu! Bali hata mwanamke maana hakuna anae kubali kudhurumika chake ki ulaisi hivi hivi hasa kuhusu swala hili gumu la mapenzi, na inauma sana lazima upate hasira tu. Au sio Dada Yasinta?

Fadhy Mtanga said...

Leo mie najifunza tu humu

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

MHHH

sijui niseme nini, kwani anaondoka nayo?? hapana, si anaiacha? sasa ugomvi wa nini

Maisara Wastara said...

Nawashukuruni sana kwa kunikaribisha, ni bahati mbaya kuwa blog yenyewe imetengenezwa na mpita njia ambaye ni mteja wetu hapa ofisini kwetu.

Nawaombeni radhi kwani kuna mapungufu mengi sana na ameniahidi kuyashughulikia leo hii jioni.

Kwa kifupi, Bado blog ipo katika matengenezo madogo madogo nawaombeni sana msisite kunifahamisha pale mtakapoona kuna tatizo.

Email yangu ni hii hapa:
wastaramaisara1@gmail.com

Naomba ushirikiano wenu wa dhati kabisa.

Wakatabahu
Ni mimi mdogo wenu na dada yenu

Maisara Wastara

Maisara Wastara said...

Mfalme Mrope, naomba nitofautiane na wewe kimtazamo.
Ni kweli kuwa linapokuja swala la mapenzi kati ya wanaume na wanawake kunakuwa na vibweka kila upande, na hiyo itategema kuwa ni upande gani umevutika zaidi kwa mwenzie.

lakini tukiangalia kwa upande unaohatarisha maisha zaidi kati ya jinsia hizi mbili, wenzetu mmetuzidi, kwani nyie kwenu kuua au kupoteza maisha kwa sababu ya mwanamke ni kitu cha kutarajia sana ukilinganisha na sisi wanawake.

kama nimeilewa mada vizuri zaidi, naamini dada Yassy alikuwa anaangalia zaidi upande wenye shari zaidi linapokuja swala la mapenzi.

Sisi wanawake tunayo yakwetu lakini mara nyingi tunaumia ndani kwa ndani na kama kutatokea shari, sana sana itakuwa ni kujitoa roho mwenyewe, lakini nyie.....ni lazima patachimbika

Huo ni mtazamo wangu.

Ni hayo tu kwa leo

Koero Mkundi said...

Longa dada Maisara, habari ndio hiyo Mfalme Mrope na kaka Chibiriti...

Mie leo sitasema kitu kwani Dada maisara kamaliza yote niliyotaka kuyasema..........

MARKUS MPANGALA said...

WAZO NI RUKSA KULIBISHIA AU???? walifunga ndoa? hivi ndoa haitenganishwi na binadamu? ni kweli inaunganishwa na mungu??? hapo ndipo penye akili na hekima tukokotoe mwanzo.

duh jamani NAUNGANA NA JABALI KAMALA,

MARKUS MPANGALA said...

TENA MCHARUKO;
ingekuwa vipi duniani wangeishi mabinti peke yao?????????????????????

Penina Simon said...

Aisee inagusa,Yasinta ukiangalia swala zima hapo ni upendo,
1. Mke wa mtu unapoamua kwenda nje ya ndoa lazima awe umekosa upendo, haijalishi kama unae au amesafiri, nina imani huyu mwanamke upendo ulikwisha kwa mumewe, vinginevyo hata mumewe angekaa gerezani miaka 100... asingesubutu kutoka nje,

2. Wanaume lazima wakubali, kama ulikuwa wapendana na mkeo halafu ugundue anatoka nje, wasichukulie hasira/umilikaji bali watafute ni nini kimepungua hadi mwanamke atoke nje na warekebishe.

3. Ni kweli wanawake wengi hufumania waume zao, lkn utashangaa wengine hawafanyi fujo, matokeo huanza kujirekebisha pale walipopungua na mambo kwenda sawa ( imean waume zao kuacha kucheat)

Mwanasosholojia said...

Ndugu zangu, mahusiano yanahitaji kupaliliwa, hata kama mtu uko umbali gani...uvumilivu sawa, lakini kuna kikomo...kasoro zinaanza kujitokeza yanapokosekana haya...kuchukua kisicho "chako", tamaa peke yake? (sababu zaidi ya moja)