Tunayo mengi ya kujivunia!!
Jana tarehe 17/5 nimekumbuka sana nyumbani, nadhani ni kwa sababu jana ilikuwa ni tarehe na mwezi ambao mama yangu alifariki. Kwa kweli nam-miss sana mama yangu.Nakumbuka ilikuwa kila nikienda likizo, nilikuwa natumia muda mwingi kuwa jikoni na mama yangu nikizungumza naye simulizi za kale za enzi ya utoto wangu.
Ni simulizi ambazo kwa kweli kila nizikumbukapo huwa natamani yale maisha yajirudie kwani kuna mengi ya kufurahisha na ya kuhuzunisha ambayo kwangu mimi nimejifunza mengi kwako.
Lakini lipo jambo moja ambalo nimelikumbuka, ambalo kwa kweli huwa linanifikirisha sana. Jambo lenyewe ni kuhusiana na baadhi ya marafiki zangu kule nyumbani.
Kusema kweli ule ukaribu niliokuwa nao na baadhi ya marafiki zangu umepungua kiasi cha kukatisha tamaa.
Sababu kubwa ni kutokana na kile walichodai kuwa nimewatupa kutokana na kutowasaidia kupata wachumba wa Kizungu. Yupo rafiki yangu mmoja mbaye yeye aliwahi kunitamkia wazi kuwa mimi ni mbinafsi kwa kuwa ni mara nyingi ameniomba nimtafutie mchumba wa Kizungu kwa kuwa ninaishi huku ughaibuni lakini nimeshindwa kumtafutia.
Nakumbuka nilimweleza ukweli kuwa siwezi kumsaidia juu ya jambo hilo kwa sababu liko nje ya uwezo wangu, lakini kutokana na labda tuite ufinyu wa kufikiri, nilimpoteza rafiki huyu kwa sababu ya kushindwa kumtafutia mchumba wa kizungu……..yaani kaaaazi kweli kweli.
Hata hivyo nilijiuliza swali moja, kuwa hivi hakuna wanaume huko nyumbani mpaka mtu aamue kutafuta mchumba wa Kizungu? Je ni mapenzi au ni Uzungu unaotafutwa hapo?
Lakini kwa upande mwingine sikumshangaa sana kwa sababu kwa huko nyumbani ipo silka ya baadhi ya watu ambao wanaamini kwamba kuoa au kuolewa na Mzungu ni jambo la kujivunia sana. Huwa nimezoea kauli za baadhi ya watu kule nymbani kila niendapo likizo wakisema, ‘siyo mwenzako yule, kaolewa na Mzungu’ .
Yaani mpaka leo hii bado kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa kuoa au kuolewa na mzungu ni jambo la kifahari na la kujivunia. Kinachotafutwa sio mapenzi tena ni huo uzungu..
Kuna baadhi ya watu wamefikia hatua ya kuamini kuwa sisi waafrika ni duni na wenzetu weupe ni bora na waliokamilika.
Lakini nadhani makosa hayo hayakuanza leo, yameanzia mbali sana. Kwani kizazi na kizazi tumekuwa tukiaminishwa kuwa wazungu ni bora zaidi yetu sisi.
Kwa mfano, mtu kufanya mambo yake kwa umakini na anayefuata muda huyo ataitwa ni mzungu, au mtu asiyependa majungu, uzinzi, uasherati na umbeya naye ataitwa kuwa ni mzungu. Nakumbuka wakati nikisoma kule nyumbani, ilikuwa kama kuna mwalimu ambaye ni mwadilifu kwa wanafunzi na anayewajali, utawasikia wanafunzi wakisema, ‘yule mwalimu ni mzungu’
Yaani kipimo cha kufanya mambo kwa uadilifu na kuwajali wengine kimekuwa kikihusishwa na uzungu, mpaka imefikia mahali kila mtu anatamani kuolewa au kuoa mzungu wakiamini kuwa hao wamekamilika.
Hata huko makazini napo watu wanaochapa kazi kwa uadilifu wanafananishwa na wazungu. Wakati mwingine huwa nacheka kwa sababu naamini hao wanaoamini kwamba mtu kuwa mzungu anakuwa amekamilika ni wazi kwamba hawawafahamu watu hao.
Kwamba kuwa mzungu ni kutokuwa na tabia mbaya, kama uvivu, udokozi, kutojali muda, kusengenya, umbeya, wivu, au kijicho, uzinzi, uasherati, ushoga na tabia zote mbaya tunazozijua hapa duniani, nikujidanganya bure.
Nasema kuamini hivyo ni kujidanganya, kwa sababu kwa wale wanaoishi huku ughaibuni au wale wanaofanya kazi na hawa wenzetu huko nyumbani, watakuwa ni mashahidi wangu.
Kama mlikuwa hamjui ni kwamba hawa wenzetu nakubali kuwa wapo waadilifu na wenye tabia nzuri, lakini pia wapo wenye tabia za ajabu kama uvivu, udokozi, kutojali muda, kusengenya, umbeya, wivu, au kijicho, kutojiamini, uzinzi, uasherati, ushoga na tabia zote mbaya tunazozijua hapa duniani.
Ule udhaifu tulio nao pia wenzetu hawa wanao tena wenzetu hawa wamepitiliza. Ila kutokana na kudanganywa na TV na hizo kauli za wazee wetu tumejikuta tukiamini kitu ambacho hakipo.
Mie wakati mwingine huwa nashangaa pale ninapokutana na baaadhi ya Watanzania wenzangu ambao wanaishi au wamewahi kuishi huku ughaibuni wanapozungumza kwa kubana pua kama hawa wenzetu. Wanashindwa kujua kwamba ile ni lafudhi ambayo inatokana na lugha yao. Ni kama pale unapokutana na Mmakonde, Mngoni au Msukuma au Mpare anapoongea Kiswahili kwa lafudhi ya lugha yao.
Mbona wenzetu kwa mfano Wanaijeria au Wakenya wanaongea kwa lafudhi ya lugha zao. Ni rahisi sana kumtambua Mkenya au Mnaijeria kutokana na lafudhi yake pale anapoongea Kiingereza, tofauti na sisi ambapo Tunajitahidi kubana pua mpaka tunajisahau hata pale tunapoongea Kiswahili.
Na ndio maana kuna baadhi ya wanawake huko nyumbani na hata huku ughaibuni wamefikia hatua sasa wanaukataa uafrika na kuanza kujichubua kwa mikorogo ili kuutafuta weupe.
Kuna wakati nilipokuwa huko nyumbani nilishangaa kuwaona baadhi ya wasichana ambao nawajua kabisa rangi zao kuwa ni weusi kama mimi lakini wamekuwa weupe mpaka wanatisha! Taabu yote hiyo ni ya nini?
Tumefikia hatua sasa kila jambo linalofanywa na hawa wezetu tunaiga, na ndio sababu siku hizi tabia kama za ushoga, usagaji na tabia nyingine chafu tunazozishuhudia huku zimetamalaki huko nyumbani.
Sisi kama Watanzania tunazo tabia nzuri ambazo hawa wenzetu wanazitamani sana tofauti na tunavyodhani. Kwa mfano, sisi ni kawaida mtu kuamka na kupita nyumba mbili tatu na kuwajulia majirani zake hali, au kuingia nyumba yoyote na kama akikuta chakula akala bila wasiwasi.
Kwa upande wa Misiba au harusi watu wamekuwa wakichangiana na kusaidiana kwa hali na mali, yaani tumekuwa na ushirikiano wa hali ya juu tofauti na wenzetu hawa.
Kuwa mzungu haimaanishai kuwa mwadilifu wala kuwa na tabia nzuri, bali tabia nzuri inatokana na tabia ya mtu na malezi kwa ujumla wake, hakuna mahusiano yaliyopo kati ya uadilifu, tabia nzuri na uzungu. Nasisitiza kuwa hakuna kitu kama hicho, ni kujidanganya bure.
Inashangaza kuona kwamba, badala ya kujivunia tabia hizi nzuri tulizo nazo ambazo hata hivyo wenzetu wanazitamani, tunatamani za kwao ambazo nyingi ni mbaya na zenye kuumiza.
Tubadilike………………
19 comments:
sitaki kumshangaa huyo rafiki yako kwa kukuchunia kisa hukumtafutia mume wa kizungu. Wala siwezi kumwona na upeo finyu. La hasha.
Siwezi kumlaumu hata kidogo. Sitofanya hivyo kwa sababu ndiyo kasumba ya dada zetu. Unakuta mtu kasoma, amegraduate na kugraduate, maana tunaambiwa huyo ndiyo msomi, lakini bado atakwambia anataka kuolewa na bwan'mzungu.
Makubwa mbona!
Da Yasinta nakupa pole na hali uliyokuwa nayo ukikumbuka mama. Sina maneno mengi zaidi ya kusema Mungu akupe faraja kwa kuwa mama amepumzika palipo pema.
Jioni njema.
Pole Yasinta ndio hali ya dunia
kwali dada yasinta umesema kweli watanzani hawataki kujivunia utanzania wao wamekazana kuiga za wazungu wanafikiri vitu vyote wafanyavyo wazungu vyote ni vizuri kumbe wanajidaganya labda vitu vizuri vyakuiga kwa wenzetu ni kufanya kazi kwa bidii kama wao na kujali mda nawanajiamini sana ndio maana wanamaendeleo ambayo hawajapata kiurahisi
Tuambie wewe ulipendea nini? uzungu au kitu kingine? usiwabanie wenzako
ninanukuu "Anonymous said...
Tuambie wewe ulipendea nini? uzungu au kitu kingine? usiwabanie wenzako
May 18, 2010 9:34 PM" mwsho wa kunukuu:- Usiye na jina unajua kun a kupenda kwa dhati na kuna kupenda kwa kutaka vitu. Na mie si wa aina ya kupenda kutaka mali. Na kwanza sioni ubaya wa kuolewa/kuoa na yeyote yule. Maana kama kweli unampenda mtu hujali ana rangi gani au ana mali kisi gani. Kwa sababu unachopenda wewe ni yule mtu hata kama ni wa njano au mweusi, kijana, mchina au mzungu hizo ni rangi tu.
Mi mpaka najisikia hasira mtu anapokuwa na hizo colonial mentality za kufikiri mzungu ni bora kuliko yeye,au kuolewa na mzungu ni ni kuondokana na matatizo,wakati si kweli kabisa.
Una haki ya kuwa na hasira kwani sio wewe tu tupo wengi. Ni jambo la kusikitisha sana kuona na kusikia hili. Lakini inaonekana na tamaduni yetu kufikiri kuwa wenzetu weupe ni bora na wanaweza zaidi. Tubadilike jamani....hiki ndio kilio changu--
Yasinta sema! Sema usiogope sema! Sisi vijana hatuogopi vibaraka sema!.
Yasinta pole kwa kutanguliwa na mama.
Ila kuhusu mada ya leo ni kutokana na umasikini wa fikra.
@ Yasinta, bila shaka huyo mdhungu wako hakujifungulia barabara, ilishakuwepo na magari yaliisha teleza mapaka ikakomaa, nilitaka kujua kama kuna tofauti yoyote kati ya ile ya mdhungu na asiye mdhungu
kuhusu kifo, soma matayo 8:22
inferiority complex: watu wengine alowaroga kama ashakufa vile :-(
Ni ujinga tu unaotusumbua :-(
Pole da Yasinta kwa masahibu!
Dah! lakini limemwagika!... :-(
Pole sana Da Yasinta hasa pale unapomkumbuka mama yako.
Ukweli ni kwamba kasumba yetu ya kudhani kila kitu cha mweupe ni kizuri imetoka mbali. Kumbuka enzi hizo za ukoloni, hii ndiyo njia mojawapo waliyotumia kututawala. Yaani kila kitu chetu ni cha kishenzi *REMEMBER?? kwa hiyo mambo kama haya yanapoendelea ndio kusema kwamba bado tunatawaliwa!!! Hey, wengi wetu tumejikomboa muda mrefu uliopita na tunakwaruzana nao mabega huku maishani. Tuache kasumba hizo kwani si za kiungwana. Tujitawale nafsi zetu na si kuruhusu mambo yaliyopita kuendelea kututawala.
Mmmh!
Pole Da Yasinta.
kazi kweli kweli. Kama unataka akuambie ladha ya hii maneno? wewe kama unataka kujua tofauti yake tafuta mzungu wako ujipakulie na kuonja halafu utafautishe.
Lakini jamani hebu tujaribu kuangalia kweli mtu unaweza kuishi na mtu kwa sababu ya mali na sio penzi? Hapa naomba kueleweshwa zaidi kwa sababu katika kichwa changu mie sijui kama ninge/nitaweza kuishi na mtu kwa sababu ana uwezo na sio kwa sababu nampenda. Duh! hapa napata kizunguzungu kabisa!!
Kwanza Pole Yasinta
Pili dada zetu hawapendi wazungu kwa maana ya mapenzi ni pochi.
Umasikini uzaa ufukara na karibu nchi nyingi fukara wanawake hujaribu kukimbia ufukara kwa kumtafuta yule anayeweza kutatua mahitaji yake.Mara nyingi nchi tajiri ni kimbilio Ulaya Magharibi,Marekani,Canada,Japan Australia,Singapore,Pamoja na nchi tajiri za kiaarabu.Kwa namna mmoja au nyingine ufukara kwa nchi masikini kwa kuwa na vipato duni,njia ya mkato ndio hiyo Mzungu maana pesa
Yasinta wee!! mbona umefungua box la Pandora? Maana nyuki watakaotoka humo ndani sipati kusema. Hii mada mara nyingi huzua mtafaruku mkubwa kwa sababu watu wengi wanaamini kuwa wanakoishi watu wenye ngozi nyeupe ni peponi na wenyewe ni malaika, ndio maana mtu mmoja akakujibu kuwa unataka kuwazibia wenzio safari hiyo ya peponi kwa kuwa wewe umeishafika huko, unataka kufaidi pepo hiyo peke yako. Na mara nyingi ni vigumu kufuta au kubadili kile watu ambacho wanakiamini, na kwa siku hizi ni vigumu zaidi kutokana na kuwa enticed na vyombo vya kimagharibi pamoja na sinema zao zinazoonyesha kuwa Ulaya na Amerika ni peponi na Afrika ni motoni.
Nimesema Afrika ni motoni kutokana na potrayal ya image ya Afrika inayofanywa na wamagharibi, kuonyesha tabu, mashaka, shida, maradhi na matatizo ya Afrika wakati upande mwingine unaona mambo mazuri tu hasa kwenye channel zao zinazoonekana ulimwenguni. Mambo yao yote yenye utata na matatizo, ulezi, mauaji, utakaji ubakaji na uuwaji wa watoto na mabaya mengineyo yanaonekana kwenye local channel zao tu na si kwingineko, sasa ni wapi na lini wandengereko na wamatumbi wa kwetu wataona ukweli kuhusu Ulaya na Amerika? Kwa hiyo sie wengine tukisema kuwa kila king'aacho si dhahabu, maisha nako huku magumu tunaonekana wachoyo, waongo na wabinafsi kwa sababu tayari tuko peponi. Mbaya zaidi kwa mtu kama wewe uliolewa na mzungu, kwa sisi tulioolewa na waafrika wenzetu tunaonekana kuwa tunasema hivyo kwa sababu tumekosa tu kama sungura "sizitaki mbichi hizi".
Kwa hiyo kila tutakalosema litaingia sikio moja na kutokea sikio la pili. Na hata hao wadogo zetu na dada zetu wakipata matatizo hawako tayari kusema au kutafuta msaada, wako tayari kufa na tai zao shingoni. Kisa wameolewa na wazungu na wanaona aibu kusema yanayowasibu. Huko South Afrika katika moja ya lugha zao Mzungu anaitwa MULUNGU na sie tumewaguza milungu kweli kweli kila wakifanyacho na wakisemacho kwetu sisi ni kizuri hata kama hakina manufaa kwetu.
Pamoja na sababu za umasikini lakini kuna wengine si masikini na nyumbani wana maisha mazuri tu lakini kwao kuolewa na Mulungu ni sifa na sababu mojawapo ya kuwakoga mashoga na marafiki. Hivi na wengine nafikiri wanamshangaa na kumlaani Yasinta kila sikU kuweka mapicha ya Ruhuwiko, kila siku kukumbuka kwao, kuongea kiswahili, hafai VICHUPI kama wazungu, kwa wao kwao ni kujidhalilisha lakini wanasahau kuwa "mdharau kwao ni mtumwa". Kuna watu tena wengi tu watoto wao hawajui kiswahili hata kidogo wala hata yale maamkuzi yanawashinda. Hawajui mila na desturi zetu wacha za makabila hata zile za majumui tu kama kusalimia wakubwa, kuheshimu wakubwa na mengineyo na hao wala hawajao wala kuolewa na wazungu lakini wanaishi kwa wazungu. Kuna mtu aliwahi kunitamkia tena wakati huo nikiwa bado naishi Dar, eti "mimi ningelikuwa msomi kama wewe na tena ninaishi huku kwenu watoto wangu ningewapiga marufuku kuongea kiswahili". Unafikiri mtu kama huyo akifika ulaya tena azae na mzungu watoto wake hata watajua asili ya kwa mama yao?
HAPO NDIPO UKOLONI MAMBOLEO ULIPOTUFIKISHA
Bi Mkora
MCHARUKO, mada tamu hii na bila shaka Da Yasinta utakumbuka ile stori ile duh.
@kamala anataka kujua ladha, lakini kumbuka sayansi inatuambia eti binadamu tupo sawa, mbona yule mdhungu hana hiyo a.k.a MOTO? yaani utadhani upo kilele cha mlima kilimanjaro a.k.a barafu
kusaka utajiri wa mzungu? Kuna mzungu aliyezaliwa akachagua kuzaliwa mzungu? TUNAUMWA UGONJWA WA KUFIKIRI na wale washamba wenzangu wanaona eti kuolewa na mdhungu ni dili waacheni waolewe labda ndiyo wanakamilisha ndoa kwa akili za za gerezani.
Post a Comment