Tuesday, May 4, 2010

WATOTO NA MATATIZO YA MTINDIO WA UBONGO

Wapo watoto wengi wanaozaliwa wakiwa na matatizo mbali mbali, lakini mojawapo nitatizo la mtindio ya ubongo ambalo leo nimeona nilizungumzie kwa undani zaidi.

Matatizo ya mtindio wa ubongo yanatokana au kusababishwa na vinasaba (Genetic), dawa alizotumia mama wakati wa ujauzito, matumizi ya madawa ya kulevya, pombe, hali ya hewa, au hata ajali. Mojawapo ya sababu hizo nilizozitaja zinaweza kusababisha kuzaliwa kwa mtoto mwenye mtindio wa ubongo au mtu kupata mtindio wa ubongo.

Nikianza na tatizo la pombe, ni kwamba pombe ina athari kubwa na mbaya kwa akina mama wajawazito. Lipo tatizo linalofahamika kitaalamu kama Fetal Alcoholic Syndrome (FAS) ambalo huwapata watoto ambao wazazi wao walikuwa wanatumia kiwango kikubwa cha pombe wakati wa ujauzito.

Watoto wanaozaliwa na tatizo hili wanakuwa na nyuso ambazo sio za kawaida (Facial Deformities), kwa mfano watoto hawa wanaweza kuwa na pua bapa na macho yaliyoingia ndani au kuwa na mtindio wa ubongo (Mental Retardations), matatizo ya kusikia na kutokuwa na uwezo wa kusoma.

Kwa hiyo unywaji wa pombe hata kwa kiwango kidogo katika kipindi cha mwezi mmoja hadi mitatu ya mwanzo kwa mama mjamzito huchangia kwa kiasi kikubwa kuzaliwa kwa watoto wenye matatizo haya.

Watoto wote wenye matatizo haya ya mtindio wa ubongo wanaweza pia kujifunza kusoma iwapo watapewa msaada maalum na kuandaliwa mazingira mazuri yatakayowashawishi kujifunza kusoma. Malezi kwa watoto wenye matatizo haya, yanatakiwa yawe tofauti na yale ya watoto wa kawaida.

Watoto hawa wanahitaji kuoneshwa upendo, kusikilizwa na mengineyo ya aina hiyo. Hata hivyo swali la msingi tunalopaswa kujiuliza ni kwamba, tutawatambuaje watoto wenye tatizo hili la mtindio wa ubongo wakingali wadogo?

Ukweli ni kwamba ni vigumu sana kwa wazazi kuwatambua watoto wao wenye tatizo hili, kabla watoto hao hawajatimiza umri wa miaka mitatu au minne. Kwa kawaida inashauriwa kwamba mtoto yeyote ambaye anafanya mambo yake pole pole ukilinganisha na watoto wengine wa umri wake, inapaswa kupelekwa haraka hospitalini kwa daktari bingwa wa watoto ili afanyiwe uchunguzi wa kina.

Hata hivyo dalili zifuatazo zinaashiria kuwa mtoto ana tatizo hili Kwanza haoneshi dalili yoyote ya kulia au anaweza kulia kidogo sana. Pili huchelewa sana kutembea na hata kuongea. Tatu haoneshi kuvutiwa nna mazingira yanayomzunguka, kwa maana kwamba hata kama kuna vitu vya kuchezea hawezi kujishughulisha navyo. Nne ni vigumu sana kufundishika na hata kujifunza kusoma huwa ni kazi ngumu ukilinganisha na watoto wa rika lake.

Tano hawezi kula mwenyewe, kuvaa mwenyewe au kujifunza kutumia choo. Hata hivyo zipo dalili nyingi zinazoweza kujitokeza na mara nyingi zinatambuliwa na madaktari maalum wa watoto.

Jinsi wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto wenye tatizo hili:

Watoto wenye mtindio wa ubongo wanafundishika, iwapo tu watafundishwa kwa makini, utulivu na uvumilivu mkubwa, yaani mtu anayemfundisha mtoto wa aina hii hatakiwi kamwe kuwa na hasira, na pia inashauriwa sana kuwapongeza wanapofanya vizuri japo kidogo.

Mwalimu anatakiwa awe mpole na ufundishaji wake usiwe wa haraka haraka, aoneshe mapenzi kwa mtoto, hapaswi kumkemea hata kama anakaosea .

Watoto wa aina hii inashauriwa wapewe nafasi ya kujenga urafiki na watoto wenzao warika lao. Huko nyuma watoto wenye matatizo ya akili walikuwa wantengwa na watoto wenzao katika madarasa, kwa kuwekwa kwenye madarasa maalum.

Lakini siku hizi inashauriwa wachanganywe na wanfunzi wenzao wasio na matatizo ya akili, japo hata kwa nusu siku. Utaratibu huu hujulikana kitaalamu, kama mainstreaming. Itaendelea.....

3 comments:

Jacob Malihoja said...

Kutokana na ukweli huo kuna hatari kubwa sana katika miaka ijayo Tanzania itakuwa na watu wengi sana wenye mtindio wa ubongo. Madawa ya Kulevya yalivyoshamiri nchini, kilimo cha Bangi, utitiri wa baa na ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya msuala hayo ya utindio wa ubongo ni tatizo sugu.

Lakini ukiacha tatizo la watoto kuzaliwa na mtindio wa ubongo madawa ya kulevya na pombe hupelekea genetics kuja kusababisha hata mtu kuja kulipuka ukichaa ukubwani.. jambo ambalo wengi wamekuwa wakihusisha na ushirikina bila kuangalia historia ya wazazi wa huyo mtu aliyerukwa na ukichaa.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

duh!

Unknown said...

Samahani natoka nje ya MADA, ila nakukaribisha pia katika libeneke la KATUNI
www.artsfede.blogspot.com