Wednesday, June 1, 2016

TUANZE MWEZI HUU MPYA/WA SITA KUTEMBELEA.....WANJAWA NDEGE WA SONGEA NI MIONGONI MWA VIWANJA BORA TANZANIA


SONGEA - DAR ES SALAAM
Uwanja wa ndege wa Ruhuwiko uliopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ni rasilimali adimu inayoweza kusaidia kukuza uchumi wa mji wa Songea hasa kutokana na  uwanja huo kuwa ni miongoni mwa viwanja bora Tanzania. Uwanja wa ndege wa Songea ni miongoni mwa viwanja 13 bora vya ndege Tanzania kati ya viwanja karibu 50 vilivyopo nchini.Uwanja huo ambao ulijengwa kati ya mwaka 1974 hadi 1980 umewekewa lami hivyo kuwa na uwezo wa kutua ndege majira yote masika na kiangazi. Utafiti umebaini kuwa uchumi wa manispaa ya Songea umeongezeka ingawa sio kwa kiwango kikubwa baada ya kuanza safari za anga kutoka Songea hadi Dar es salaam ukilinganisha na hali ilivyokuwa kabla ya mwaka 2011 wakati mji wa Songea ukiwa hauna usafiri wa anga. Ofisa habari wa manispaa ya Songea Albano Midelo anasema Kabla ya kuanza safari za ndege
katika uwanja wa ndege wa Songea mwaka 2011,wafanyabiashara,Taasisi za kidini,
wawekezaji na wadau wengine walikuwa wanapata shida ya kusafiri kwa magari ambayo
yanachukua zaidi ya saa 15 kutoka Dar es salaam hadi Songea.
Midelo anasema safari za anga zimesaidia wadau mbalimbali kutumia usafiri wa ndege kutoka na
kwenda Dar es salaam hivyo  kuwezesha kufanya kazi zao kwa muda mfupi badala ya kupoteza saa
kadhaa barabarani hivyo kuzorotesha uchumi wa manispaa ya Songea na wa mtu mmoja mmoja.
“Licha ya kukuza uchumi,lakini usafiri wa anga katika manispaa ya Songea umerahisisha huduma za matibabu, mgonjwa anapozidiwa na kuhitaji rufaa kwa haraka anasafirishwa kwa njia ya anga kutoka Songea hadi Dar es salaam, hivyo usafiri wa anga umesaidia kuokoa maisha ya wakazi wa Songea na watanzania kwa ujumla wake’’alisema. Ongezeko kubwa la  wageni wanaosafiri kwa ndege katika mji wa Songea wanapolala katika nyumba za wageni na kukodi taksi kutoka uwanja wa ndege hadi mjini wanasaidia kuongeza pato katika Halmashauri ya manispaa ya Songea.
Hata hivyo changamoto kubwa ambayo inasababisha wakazi  wa Songea na wageni kutotumia usafiri wa ndege ni nauli kubwa ambayo inatozwa na kampuni binafsi ya ndege ya Auric Air ambayo ni kati ya shilingi 350,000 hadi 400,000 bei ambayo wengi wanashindwa kumudu kulipa.
Utafiti unaonesha kuwa nauli za ndege zikishuka watanzania wengi  wanaweza kusafiri kwa ndege kutoka Dar es salaam hadi Songea hivyo Songea itapata wageni wengi ambao watapata huduma mbalimbali za usafiri,chakula,malazi na kutembelea vivutio vya utalii hivyo kukuza pato la serikali na mwananchi mmoja mmoja. Meneja uwanja wa ndege wa Songea Valentine Fasha
Meneja wa uwanja wa ndege wa Songea Valentine Fasha  amesema licha ya changamoto ya nauli inayotozwa na kampuni binafsi ya ndege ya Auric air bado kuna idadi kubwa ya abiria ambao wameamua kusafiri kwa ndege toka Songea hadi Dar es salaam.“Abiria ambao wanatumia ndege kutoka Songea hadi Dar es salaam wanaendelea kuongezeka kwa mfano kwa mwaka 2015 pekee abiria  karibu 5000 walisafiri kwa ndege idadi ambayo inaridhisha kwa kuwa kabla ya usafiri wa anga idadi ya wageni waliokuwa wanafika Songea pia ilikuwa chini’’ ,alisisitiza.
Alisema ndege zilizokuwa zinatua kwenye uwanja huo kabla ya mwaka 2011 zilikuwa zinakodiwa kwa gharama kubwa ambapo kuanzia Oktoba 17,2011 kwa mara ya kwanza ndege ya abiria ya Auric ilianza kutoa huduma kwenye uwanja huo kuja Songea na kurudi Dar es salaam.Hata hivyo amesema serikali itakaponunua ndege ya serikali nauli ya ndege inaweza kupungua na kwamba lengo la mamlaka ya ndege Tanzania ni kuhakikisha kuwa kila mtanzania aweze kusafiri kwa ndege kwa kuwa usafiri  wa ndege ndiyo  wa haraka,salama na uhakika zaidi.
Fasha amebainisha kuwa ndege ya Auric inatoa huduma za usafiri siku tano kwa wiki ambazo ni Jumamatu, Jumanne, Jumatano, Alhamis na Jumamosi, ndege hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 13, inatumia saa 2.15 kutoka Songea hadi Dar es salaam.Hata hivyo amesema ndege kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 50 inatumia takriban saa moja tu
kutoka Songea hadi Dar es salaam na kwamba nauli kwa ndege kubwa pia inapungua ukilinganisha na ndege ndogo.
Kulingana na meneja wa uwanja huo,Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania ina mpango wa kupanua uwanja wa ndege wa Songea ambapo serikali imefanya upembuzi yakinifu katika viwanja 11 Tanzania ukiwemo uwanja wa ndege wa Songea ambavyo vinatakiwa kuboreshwa ili viweze kutoa huduma bora na za kisasa na kusababisha ndege kushawishika kutoa huduma Songea.
Fasha amesisitiza kuwa uwanja wa ndege wa Songea unatarajiwa kupanuliwa na kupewa vifaa vya kisasa ili uwe  uwanja wa kisasa zaidi pia ni matarajio ya serikali kuleta ndege ya serikali ambayo inaweza kuboresha huduma za usafiri wa ndege katika safari ya Dar es salaam-Iringa hadi Songe
“Route zote za ndege katika Tanzania zina huduma za ndege isipokuwa hakuna route ya Dar es salaam, Iringa na Songea,Rais wetu Magufuli amepania kulisimamia shirika la Ndege hivyo naamini atahakikisha route yetu inafanikiwa,lengo ni kila mtanzania aweze kupanda ndege,aone dunia inavyoonekana akiwa angani,aweze kusafiri kwa haraka kwa gharama nafuu’’,alisisitiza.Amesema shirika la ndege la Tanzania likifufuliwa na kusimama utakuwa ni ukombozi kwa watanzania wote kwa kuwa sasa ndege zitaruka na kutua katika kanda zote ikiwemo ya Dar es salaam,Iringa hadi Songea  hivyo kufuta tabaka kwamba kila mmoja ataweza kupanda ndege kutokana na gharama kuwa chini.Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Waziri wa ujenzi,uchukuzi na mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema shirika la ndege Tanzania (ATCL)limetengewa shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kununua ndege tatu mpya.Hata hivyo Profesa Mbarawa alisema idadi ya ndege zitakazonunuliwa na bei ya kila moja itajulikana baada uya uchambuzi kukamilika. Alisema mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania katika bajeti ya mwaka 2016/2017 imetengewa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kutekeleza miradi yake ikiwemo ukarabati wa viwanja vya ndege ,usimikaji wa taa,mitambo ya kuongozea ndege na kuendeleza upanuzi
wa viwanja vya ndege.
Mwisho
CHANZO:-Stephano Mango

No comments: