Wednesday, June 29, 2016

UKOSAPO NENO JEMA, KHERI UJINYAMAZIE.

Nakuasa usikie, usemaji ni karama,
Maneno usirukie, sema mambo kwa kupima,
Utamkapo ujue, neno halirudi nyuma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Kheri ujinyamazie, ovu huleta khasama,
Majuto yasikujia, “Laiti nisingesema”,
Mtu baa azuae, Motowe utamchoma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Ni wengi wajiponzao, kwa zao mbovu kalima,
Heshima waitakao, waseme usemi mwema,
Wale waumbukanao, ni kwa ndimi kuparama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Watazame wakuao, dunia kuwatazama,
Ni wale wapimiao, kabla ya kuyasema,
Na kimya wanyamazao, wakosapo neno jema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Neno huenda likuwe,lizidi hata vilima,
Mambo mawi liyazue, akili zende mrama,
Au mema yatukie, liwapo neno la wema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Funzo walitufunzao, wazungupule wa zama
Zama za kale na leo, walokimcha Karima,
Yawe mema tusemao, tusije zusha zahama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Mola akubarikie, na ambaye akusoma,
Na furaha ututie, uwe ni diwani njema,
Mema utuhadithie, wana kwa watu wazima,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Shairi hili limetungwa na Mshairi maarufu Afrika Mashariki Bwana Amri Abedi, nami nimeona sio vibaya kulirejea ili tujifunze pamoja................. panapo  majaliwa tutaonana tena...

10 comments:

NN Mhango said...

Ni kweli uliyonena, kusema kuna mashaka,
Heri ubaki kununa, kulikoni kupayuka
Uamuapo kunena, sema lisilo na shaka
Ukosapo la kunena, Heri kukujinyamazia

Wahenga walishasema, heri kimya ni dhahabu,
waweza kosa heshima, ukaambua adhabu
Mabovu ukiyasema, wawezaitwa kidhabu,
Ukosapo la kusema, heri kujinyamazia.

Wengi wameangamia, ulimi umewaponza
Wengi bado waumia, kupayuka kunaponza
muhimu kufikiria, siyo kupayuka kwanza,
Ukosapo la kusema, heri kujinyamazia

Sina tena na kusema, bora kujinyamazia
Hapa ndipo kaditama, nyumbani natangulia
Nawaombea neema, heri ninawatakia
wote wataoamua, kunyamaa si kusema.

Yasinta Ngonyani said...

Kumbe nawe kaka Mhango upo juu kwa mashairi...Hongera alo! Pia ahsante nimependa utunzi wako.

NN Mhango said...

Shukrani sana. Hukujua kuwa mimi ni mshairi siyo? Au nikutumie kitabu changu cha ushairi LULU YETU TANZANIA ambacho bahati mbaya sijapata mchapishaji. Hata hivyo ninavyo vitabu vitatu vya mashairi ya Kiingereza ambavyo vimeishachapishwa yaani Souls On Sale, Born with Voice na Psalm of the Oppressed si haba.

Yasinta Ngonyani said...

Mwal. Mhango...Hakika sikujua kabisa nimefurahi sana kujua hili....nitafurahi kusoma mashairi yako...

NN Mhango said...

Dada Kapulya pulika, shairi ninaandika,
Soma na kusawajika,hili ni lako hakika,
Kutunga kwangu si shaka, pale muda nikinyaka
Dada Kapulya lisome, najua wasawajika.

Ushairi ni mtamu, nafsi huburudisha,
Ni kunga ilo muhimu, isiyotaka mzaha,
Huu ni utaalamu, wenyemanenoye yana raha
Dada Kapulya lissome, moyo utasawajika.

Leo mengi sintosema, muda wanipa kisogo,
Nakuombea neema, natoka kwenye uringo,
Bora tuombe Karima, atutenge na vinyongo,
Mwenzio kitenda jema, usiache kushukuru.


Beti nne ni kikomo, mbele sitaendelea,
Hapa natia mgomo, kalamu naiegua,
Huu mwisho wa kisomo, ukomo nimefikia,
Shairi hili ni lako, nakupa ujisomee.

nisalimie watoto, pamoja na baba yao
Kwako hii changamoto, ni moto ni uwashao,
Hapa ninatoa mwito, nalingoja shairilo,
Inshallah tukijaliwa, naliongoja shairilo.

Yasinta Ngonyani said...

Shairi nimelisoma, ambalo umeniandikia,
Ahsante nasema, cha kukukujibu leo sina,
Ila nakuomba, subira kuivuta,
Nasema tena ahsante kwa hizi beti.

NN Mhango said...

Du kumbe nawe wamo. Ongeza bidii utaishia kuwa mshairi maarufu kama wengine.

Yasinta Ngonyani said...

Haaa..kaka Mhango bwana, eti nimo. Nimefurahi kwa kunipa moyo...ila mmhhh kuwa mshairi maarufu.....

Agnes Kambarage said...

Uko vizuri kaka kwa utunzi wa mashairi

NN Mhango said...

Agnes shukrani sana japo nimesoma comment yako baada ya muda mrefu;