Monday, March 4, 2013

Mtoto Wako Ni Mwalimu Wako!!!!

Ninimesoma habari  hii kwa makini sana na napenda kusema nakubaliana na kaka Mjengwa...na ndio sababu katika malezi yangu sijakuwa mbali na wanangu . Hata hawajawa na mlezi mwingine zaidi yetu na labda walimu. Wazazi tujitahidi sana kuwa karibu na watoto wetu ni mambo mengi sana tutapata kutoka kwa watoto, ni watoto lakini wana mambo mazuri sana ....haya endelea kusoma hapo chini ili nawe ujifunze kitu kama nilivyojifunza mimi...karibu....
Ndugu zangu,

Moja ya maamuzi mazuri niliyopata kuyafanya ni hili la kutojihusisha na siasa za majukwaani ili kuwa na muda zaidi na watoto wangu.
Hakika, miaka kumi ya mwanzo ya makuzi ya mtoto ni muda muhimu sana katika makuzi ya mtoto. Hapo ndipo unajengwa msingi wa mtoto maishani.
Mzazi unatakiwa kuwa karibu na mtoto katika miaka yake kumi ya mwanzo, lakini, hata baada ya hapo, kabla mtoto hajatimiza miaka kumi na minane, bado mzazi unatakiwa kuwa karibu na mtoto wako. Kujenga misingi ya mahusiano ya mtoto na mzazi, awe mzazi wa kike au kiume.
Mara nyingi tumefanya makosa kudhani kuwa mahusiano yanayopaswa kujengwa ni kati ya watu wazima. Kati ya mke na mume, na kati ya mzazi na wazazi wengine. Tunayasahau mahusiano kati ya mtoto na mzazi.
Tunafanya makosa kuwaachia mayaya wa nyumbani jukumu la kulea watoto wetu. Tunafanya makosa pia, kuwaachia walimu tu, jukumu la kufuatilia mienendo ya elimu ya watoto wetu.
Na wazazi wa kiume tumekuwa mfano mbaya sana wa kuliacha jukumu la kulea kwa mzazi wa kike.
Hakika, mtoto, awe wa kike au kiume, anahitaji sana kuwa karibu na mzazi wa kiume pia. Kuwa na mahusiano ya kirafiki pia. Kazi ya mzazi haipaswi kuwa ni ya kukaripia watoto tu, bali kuwa rafiki nao, kuwa na muda wa kucheka nao. Na kubwa zaidi, uwa tayari kujifunza kutoka kwa watoto.
Na mtoto anaweza kuwa Mwalimu mzuri kwa mzazi, kama mzazi atamwandalia mtoto mazingira ya kuifanya kazi ya ualimu kwa mzazi wake.

Niwe mkweli, kuwa nimejifunza mengi kutoka kwa watoto wangu kama wao wanavyojifunza kutoka kwangu.
Mathalan, leo asubuhi nilimkuta mwana wangu akisoma kitabu (hicho pichani). Nikamwomba anisimulie kidogo juu ya anachosoma. Alipoanza kunisimulia, basi, nilijikuta nataka kumsikiliza zaidi. Kinahusu mtoto ambaye wazazi wake walitengana. Mzazi mmoja anaishi Marekani na mwingine Canada.
Mtoto huyu aliondoka kwa mama yake Marekani ili aende kumwona baba yake Canada. Alipanda ndege ndogo. Alikuwa yeye na rubani tu.
Huko angani rubani akapatwa na mshtuko wa moyo. Mtoto huyu akalazamika kuongoza ndogo hiyo. Aliongoza huku ndege ikipotea angani. Mwisho ndege ikaishiwa mafuta, maana hakujua haswa namna ya kuongoza ndege.
Ndege ikaanguka ziwani. Bahati njema mtoto aliweza kuogelea na kunusurika. Akalikuta pango, hapo akaanza kutafuta mbinu za kuishi akisubiri msaada wa kuokolewa... Kisa kinaendelea...!
Tunajifunza nini?
Umuhimu wa wazazi kuwajengea watoto wetu utamaduni wa kujisomea. Mimi niliwasomea vitabu watoto wangu tangu wangali wadogo sana. Hivyo, nikawajengea hamu ya kusoma.
Si ajabu, kuwa leo wanasoma vitabu kiasi cha hata kuweza kunisimulia ya kwenye vitabu ambavyo nisingeweza kuviona maishani mwangu. Na kuna ninayojifunza. Hivyo, watoto wangu wanakuwa walimu wangu pia.
Naam, mtoto wako ni mwalimu wako.
Na hilo ni Neno la Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765
JIONI NJEMA KWA WOTE!!!!


3 comments:

Nicky Mwangoka said...

Ni kweli lakini tunapuuzia

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Nicky...karibu sana tena hapa kwetu...na ndio hapo tunapokosea kupuuzia kwa sababu hii ndiyo kazi muhimu kuliko zote hapa duniani...

ray njau said...

Huu ndiyo wajibu wetu wa msingi lakini kama binadamu tunajisahau na kushindwa kujali wajibu wetu!!!