Thursday, March 11, 2010

BROWN ASHIKA TAMA

Tujifunze lugha yetu

Brown ashika tama
“Mmetawala nchi hii kwa muda usiopungua miaka arobaini , na maisha ya watu yamekuwa ya wasiwasi mpaka sasa. Twawaambieni kwamba fungeni virago mrudi kwenu Ulaya, mtuachie nchi yetu tuiongoze wenyewe. Tunawahakikishieni kuwa kwa muda wa miaka kumi ya uhuru wetu, nchi itakuwa imebadilika. Wakati huo, njooni mwone, nchi itakuwa imefika kiwango gani cha maendeleo.” Maneno hayo yalisemwa na Mheshimiwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius K Nyerere wakati TANU ilipokuwa inadai uhuru.

Usemi wa Rais wetu haukuadhirika. Siasa safi na uongozi bora ndiyo ulionufaisha usemi huo. Siasa tunayoifuata ni ile yakutofungamana na upande wowote wa nchi nyingine za ulimwengu. Ni siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo si ngeni katka nchi hii. Sisi tunafuata mfano wa jadi zetu. Ufanisi uliopatikana katika maendeleo yetu umeshtua ulimwengu mzima. Watu wa mataifa mbalimbali huja Tanzania kujionea wenyewe jinsi wananchi tunavyojenga taifa letu.

Siku moja Brown, Mwingereza ambaye aliwahi kuwa Bwana Shauri katika sehemu mbalimbali za Tanzania wakati wa ukoloni, alitalii Tanzania. Yeye alikuwa mwandishi wa gazeti moja huko Uingereza: na aliona kuwa angeweza kukusanya habari nyingi za Tanzania na maendelea yake. alikuja kuona ukweli wa maneno ya Rais Nyerere ambayo zamani aliwaambia wakoloni. Brown alifika Tanzania baada ya mika tisa tu tangu nchi kupata uhuru.

Baada ya kuwasili Dar es Salaam kwa ndege, akaamua kukaa jijini kwa muda wa siku mbili. Halafu alisafiri Tanzania bara kutembelea mbuga za wanyama na sehemu nyingine za kuvutia. Alitembembelea vijii vingi vya ujamaa katika mikao ya Mtwara, Ruvuma, Mbeye, Tabora, Mara, Pwani na mingineyo. Kila alipotembelea, alizungumza na wananchi habari za maisha yao katika vijiji hivyo vya ujamaa. Mazungumzo yaliyomfanya Bwana Brown ashike tama hasa ni yale yaliyosemwa na Mzee Kaswiga wa kijiji cha Mbalizi Mkoa wa Mbeya. Walizungumza chini ya mti mkubwa uliosimama kando ya barabara ya mtaa mmoja wa kijiji hicho.

Bwana Brown alianza mazungumzo kwa kuuliza, “Je, Mzee Kaswiga, unaweza kuniambia shabaha za kuanzisha vijiji vya ujamaa katika nchi hii, au unafahamu sababu ya kuanzisha kijiji hiki tu basi? Mzee Kaswiga akajibu, “ndiyo naweza. Shabaha katika vijiji vyote vya ujamaa ni Umoja. Tumekuwa wanyonge wa maisha kwa muda mrefu sana kwa sababu ya kuishi kwa ubinafsi. Sasa tumeamua kuishi kijamaa ili tufanye kazi pamoja, na mapato ya kazi yawe kwa faida ya wote vijijini. Matokeo yake ni haya unayoyaona katika kijiji hiki.” Bwana Brown akauliza tena, “Unamaanisha nini unaposema kuishi pamoja kijamaa? Kwani hamkuwa mnaishi hivyo kabla ya sasa?” Mzee akajibu, “Babu zetu wa kale walikuwa wanaishi namna hii, wakoloni walipotawala wakaingiza ubinfsi ili mabepari wastawi. Maendeleo ya watu yalikwama, kwani waligeuzwa kuwa na mioyo ya ubinafsi. Lakini sasa hali hiyo hatuna. Wana-Kijiji hujiona kuwa ni kitu kimoja. Kazi zetu tunazozifanya zina lengo la kuinua maisha yetu. Mwana-kijiji huwa amejiweka katika bima ya maisha kwa vile huwa chini ya uangalizi wa kijiji. Huo ndio msingi wa kuishi pamoja, kwa ajili hiyo watu hupendana, huheshimiana kindugu na kusaidiana katika matatizo mbalimbali. Bepari au kabaila hana lake tena.”

Bwana Brown aliandika maneno katika daftari yake. alimtazama mzee Kaswiga kwa tabasamu ya husuda, kisha akamwuliza, “Kwa hiyo una maana kwamba hizo tu ndizo faida mnazopata?” Mzee akajibu, “La, hasha, hizo ni baadhi tu. Shule na hospitali zimejengwa. Maji yamepelekwa vijijini kwa mabomba, pia kuna faidanyingine nyingi. Siku hizi maisha yameanza kutakata ukilinganisha a enzi za wakoloni.” Bwana Brown alionyesha kufadhaika kwa vile maneno ya Mzee Kaswiga yalimsuta. Akajitetea kwa kusema. “Lakini wakoloni walikusudia kutenda hayohayo, kwani walianza kujenga shule na hospital..........” Mzee Kaswiga akamdakiza, “La, la, la, sisemi hamkufanya lolote. Ingawa mlipanga kutenda mengi, kutimiza kulikuwa kwa pole pole; na kwa upande mwingine nataka ufahamu kuwa kukusudia si kutenda, kwani mawazo peke yake hufiki mbingu ya saba! Ni kama ruya ya kupaa hewani usiku.”

Mazungumzo yalizidi kukolea. Bwana Brown akatambua kwamba yule mzee alikomaa na siasa ya ujamaa na mabadiliko ya maendeleo nchini. Hata hivyo alimuliza swali jingine. “Mambo gani yanasababisha kuanzisha vijiji vya ujamaa?” Mzee alichelewa kidogo kujibu swali hilo kwani alikuwa ananusa ugolo. Baada ya kufuta pua na machozi alijibu, “Vijiji vingine vimeanzishwa kwa sababu ya mafuriko ya maji. Watu wanaoishi kando kando ya mito huingiliwa na mafuriko, kwa hiyo huamua kuhama na kuanzisha makao mapya sehemu zilizoinuka. Vijiji vya ujamaa katika wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani vilianzishwa namna hiyo. Sababu nyingine ni ya kudumisha usalama wa maisha ya watu kwa urahisi. Wakikaa pamoja, huwa ni rahisi kujilinda kutokana na maadui. Vijiji vingi vya Mkoa wa Mtwara vilianzishwa kwa sababu hiyo. Vijiji huanzishwa kwa njia mbalimbali. Njia ya kwanza ni kwa hiari ya watu wenyewe badala ya kuelewa na kuridhika na siasa ya ujamaa. Pili nikwamba watu wanaweza kugeuza kijiji chao cha zamani na kukifanya cha ujamaa.” Wakati Mzee Kaswiga alipokuwa anasimulia hayo, Bwana Brown alikuwa ameegemesha shavu lake juu ya kiganja cha mkono wa kulia huku akimsikiliza kwa makini. Alistaajabu kumwona mzee huyo akisimulia habari za vijiji mbalimbali vya Tanzania kwa uhakika kabisa.

Wakati ulikuwa mwingi sana, lakini Bwana Brown hakuonyesha dalili ya kuchoka. Alitaka kufahamu uongozi wa kijiji kwa jumla. Mzee Kaswiga akamweleza Bwana Brown hivi, “Uongozi wetu unatawaliwa na Katiba ya kijiji ambayo imetengenezwa na wana-kijiji wenyewe. Katiba inaonyesha viongozi na kamati za kijiji. Kadhalika inaonyesha masharti yanayotawala maisha ya wana-kijiji, utaratibu wa kufanya kazi na kadhalika. Mipango ya uchumi imepangwa ili itimizwe kwa muda ule wa miaka ya maendeleo iliyopangwa na serikali. Ili mipango hiyo itimizwe ipasavyo, wana-kijiji hugawanywa katika vikosi. Kila kikosi hupewa kazi maalum ya kufanya kila siku iliyo tofauti na kazi ya kikosi kingine. Kwa mfano katika vijiji vya Rufiji kila mabalozi kumi hufanya kikosi kimoja ambacho kinakuwa chini ya kiongozi anayeitwa Mhenga. Kazi ya Mhenga ni kuangalia na kuhakikisha kuwa kazi ya siku inafanywa, na baada ya kazi hupeleka ripoti kwa Mwenyekiti wa Kijiji ambaye huingiza mahudhurio yote katika daftari. Kwa njia hii inakuwa rahisi kuwafahamu watu wasiohudhuria kazi. Wapiga uvivu huchukuliwa hatua kwa mujibu wa katiba. Kazi muhimu hasa zinazoweza kuendeshwa katika vijiji vya ujamaa ni kama kilimo, ujenzi, uvuvi, ufinyanzi ususi, na kadhalika. Ni shabaha ya wana-kijiji kuendesha viwanda vidogo vidogo ili kupata mahitaji yao ya kila siku. Natumaini umeona kazi kama hizo katika vijiji vingine ulivyotembelea.”

Bwana Brown alitosheke sana na maelezo hayo. Alijionea mwenyewe jinsi Watanzania walivyokuwa wanapiga vita umaskini, maradhi na ujinga. Maneno ya Rais hayakuwa bure na kwamba Tanzania yastahili pongezi machoni pa ulimwengu. Baadaye Bwana Braun aliwaaga wazee wa Mbalizi kwa furaha na alimsifu sana Mzee Kaswiga alivyozungumza naye kwa busara sana. Aliwatakia kila la heri katika kukiendeleza kijiji chao na nchi yao kwa ujumla.

7 comments:

Koero Mkundi said...

Dada ngoja ninukuu.....
"Bwana Bron alianza mazungumzo kwa kuuliza, “Je, Mzee Kaswiga, unaweza kuniambia shabaha za kuanzisha vijiji vya ujamaa katika nchi hii, au unafahamu sababu ya kuanzisha kijiji hiki tu basi? Mzee Kaswiga akajibu, “ndiyo naweza. Shabaha katika vijiji vyote vya ujamaa ni Umoja. Tumekuwa wanyonge wa maisha kwa muda mrefu sana kwa sababu ya kuishi kwa ubinafsi. Sasa tumeamua kuishi kijamaa ili tufanye kazi pamoja, na mapato ya kazi yawe kwa faida ya wote vijijini. Matokeo yake ni haya unayoyaona katika kijiji hiki.” Bwana Brown akauliza tena, “Unamaanisha nini unaposema kuishi pamoja kijamaa? Kwani hamkuwa mnaishi hivyo kabla ya sasa?” Mzee akajibu, “Babu zetu wa kale walikuwa wanaishi namna hii, wakoloni walipotawala wakaingiza ubinfsi ili mabepari wastawi. Maendeleo ya watu yalikwama, kwani waligeuzwa kuwa na mioyo ya ubinafsi. Lakini sasa hali hiyo hatuna. Wana-Kijiji hujiona kuwa ni kitu kimoja. Kazi zetu tunazozifanya zina lengo la kuinua maisha yetu. Mwana-kijiji huwa amejiweka katika bima ya maisha kwa vile huwa chini ya uangalizi wa kijiji. Huo ndio msingi wa kuishi pamoja, kwa ajili hiyo watu hupendana, huheshimiana kindugu na kusaidiana katika matatizo mbalimbali. Bepari au kabaila hana lake tena.”

Mwisho wa kunukuu....
Maswali yamkujiliza:
=Je malengo hayo yalifikiwa?
=Kama yalifkikuiwa Je ni kwa kiasi gani?
=Na kama hayakufikiwa, Je tatizo lilikuwa ni nini?
=Je kuna nadharia ngapi zilizowahi kuanzishwa na wanasiasa wetu zikapata mafanikio ya kujivunia?

WALLAHI HATA MIMI NINGESHIKA TAMA

Mija Shija Sayi said...

Yasinta wewe ni kiboko! Hata sina la kusema, umevipata wapi hivi vitabu?

watila said...

ahh mbona Mzee kasingwa hajaeleza wananchi wangapi waliliwa na simba?
kwa sababu ya vijiji va ujamaa kuwapeleka watu sehemu ambazo wapo simba siasa zileeee hazikufa tz

watila said...

eeh bwana wee watu waliliwa kweli na simba siku za ujamaa

Yasinta Ngonyani said...

Koero ni maswali mazuri ambayo wote tungependa kupata majibu kwa kweli.

Da Mija kumbuka mimi ni mTanzania halisi nimevinunua bookshop tena KUPERAMIHU:-)

Watila! labda hakuna aliyeliwa na simba....swali nzuri

Majaliwa said...

Asante dada Yasinta.Ila swali linalonikera kichwani mwangu kwa Mzee Kaswiga ni je, "Kama Maneno ya Rais hayakuwa bure na kwamba Tanzania yastahili pongezi machoni pa ulimwengu": mbona vijana wengi kule vijijini miaka hii hapakubaliki,wengi wanazidi kukimbilia mijini?Maana kule Mdunduwalo vijana siku hizi wameadimika kama maini ya kuku:-)

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Duh!