Monday, October 5, 2009

Kupanda kwa bei za nafaka Ruvuma...Haijawahi kutokea kama mwaka huu

Mnunuzi wa viazi mviringo akishangaa kupenda kwa bei ya vyakula katika soko la mazao la Sodeco mkoani Ruvuma

KUENDELEA kupanda kwa bei za vyakula, hususan nafaka mkoani Ruvuma kunaelezwa kwamba kunachangiwa na mfumuko wa bei, ushuru wa mazao ambao unatozwa na halmashauri za wilaya pamoja na mavuno madogo msimu huu baada ya wakulima wengi kuchangamkia mazao yasiyohitaji pembejeo kama mbolea. Wakulima wengi wanalima mazao mchanganyiko ya biashara kama ufuta, karanga, soya pamoja na jatrofa ingawa pia wanalima mahindi kidogo. Sababu kubwa ni kukwepa kununua mbolea ambazo wanasema ni ghali na hawana uwezo kuzinunua licha ya kuwa na nguvu za kuzalisha mahindi mengi.

Wafanyabiashara katika Soko la Mazao la Sodeco, Songea wanasema mahindi yamekuwa machache kutokana na ushuru mkubwa kwa wakulima hivyo kuwauzia wafanyabiashara kwa bei kubwa.
"Tunaiomba serikali itusaidie kupunguza ushuru katika halmashauri kwani kutoza ushuru mkubwa kwa wakulima na wafanyabiashara ndiko kunakochangia bei za mazao kupanda kila mara,"anasema mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo, Bakari Musa. "Kwetu kupanda huko kwa bei za vyakula ni dalili mbaya kwa maisha ya kila siku ya wananchi, hususan wale wenye kipato cha chini, kwa sababu kupanda kwa gharama hizo hakuendani na kuongezeka kwa ajira wala viwango vya mishahara inayotolewa katika sekta ya umma na binafsi nchini,"alisema.

Mfanyabiashara huyo anasema iwapo halmashauri zitaendelea kuwadai ushuru wa mazao wakati wanaposafirisha mazao kutoka kijijini na kutoka mjini kwenda mikoa mingine, nchini nao wataendelea kupandisha bei ya mazao ili wapate faida. Katibu wa Umoja wa Wanunuzi wa Mazao Mkoa wa Ruvuma (UWAMAVIRU), Thadeo Mwakaguo anasema ushuru umekuwa tatizo kubwa na faini zimekuwa kubwa kitu ambacho ni kero kwa wakulima.
Anasema doria ambazo zimewekwa na halmashauri ndizo zilizochangia kwa kiasi kikubwa masoko kukosa mazao na hivyo kusababisha kupanda kwa bei. "Haijawahi kutokea kupanda kwa bei za nafaka kama mwaka huu Ruvuma. Kilo moja ya mahindi iliyokuwa ikiuzwa kati ya Sh150 na 180 inafika hadi Sh 300 kitu ambacho ni hatari kwa wananchi," anasema Mwakaguo.

Anasema mavuno yamekuwa mabaya wengi wamevuna tofauti na matarajio yao kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Mvua zilikatika mapema na Februari kukawa na jua kali hivyo kusababisha baadhi ya mazao kunyauka na mengine kufa kabisa. Anasema kwa kawaida katika kipindi cha Mei na kundelea kunakuwa na ongezeko kubwa la mazao sokoni hapo kwani hupokea wastani wa tani 30 mpaka 40 kwa siku kutoka kwa wakulima vijijini lakini mwaka huu kuna uhaba mkubwa wa chakula kwani mazao yanayopelekwa ni kidogo.

Katibu huyo anasema uongozi wa wafanyabiashara umepanga kukutana na halmashauri ili kuzungumzia suala hilo la ushuru. Anasema mbali ya hali kuwa mbaya, halmashauri hiyo inataka kuongeza ushuru huo kutoka Sh 1,000 kwa gunia la kilo 100 hadi Sh1,500. Anaitaka serikali kuwa makini na kuwadhibiti mawakala wanaouza mbolea zilizokwisha muda wake kwani zimewasababishia wakulima hasara kubwa msimu uliopita. Mkuu wa Masoko ya Manispaa ya Songea, Salum Omera anashauri kuwa biashara ya mahindi ifanyike kwa uangalifu kuwaepusha wananchi dhidi ya balaa la njaa.

Anawataka wakulima wasipende kuuza mazao yote ya chakula bali wabakishe kwa ajili ya kusadia familia zao hasa wakati wa njaa. Anasema kumekuwa na mfumuko mkubwa wa bei katika nafaka. Gunia la kilo 100 la mahindi linauzwa Sh 35,000 na linaweza kupanda muda wowote kuanzia sasa, mchele kilo moja ni Sh 1,400 hadi 1,500, maharagwe gunia moja ni Sh 100,000 maeneo mengi ya hayana mazao ya kutosha.
Anasema kwa sasa halmashauri ina mpango wa kupanua masoko ya mazao ili kuwasaidia wananchi kupata huduma katika maeneo yote na pia kuimarisha miundombinu ya masoko hayo.
Hata hivyo anawalaumu wafanyabiashara wengi kwa kukwepa kulipa kodi.
Hata hivyo, anasema kwamba ofisi yake haitumii nguvu katika ukusanyaji wa mapato zaidi ya kutoa elimu.
Lakini Meneja wa Takwimu Mkoa wa Ruvuma, John Lyakurwa anasema kupanda kwa bei za vyakula mara kwa mara kumechangiwa na kupanda kwa bei za usafirishaji wa mafuta. Anasema bidhaa zikiwa chache wafanyabiashara wanapandisha bei tofauti na wakati wa mavuno. Lakini anasema cha kushangaza mwaka huu hata wakati wa msimu wa mavuno, bado hali ni mbaya, bei zimeendelea kupanda kila mwezi. "Pamoja na kuwa sasa hivi ni msimu wa mavuno bado vyakula na baadhi ya vitu vimeendelea kupanda, kwa mfano, mchele ulitakiwa kuuzwa kilo moja Sh 800 lakini unauzwa Sh 1,400 mpaka 1,500,"anasema Lyakurwa. Anasema uwezekano wa bidhaa hizo kuendelea kupanda kutokana na gharama za usafirishaji, ushuru ni mkubwa na kumsababishia mzigo mkubwa mlaji wa kawaida ambaye ni mwananchi.
"Tunataraji kufanya tathmini ya upungufu wa chakula ili kujua kilichosababisha kupanda kwa bei ya vyakula na hatua zitakazochukuliwa ili kuzuia kupanda holela kwa bei za vyakula na bidhaa mbalimbali za viwandani. Mkazi wa Songea, Julian Haule anasema kuwa bei za vyakula zimeendelea kuwa juu hali inayoashiria kupungua kwa bidhaa hiyo vijijini. Anaamini kwamba sababu kubwa ni upungufu wa mvua za vuli.
Anasema serikali inapaswa kuwa makini dhidi ya wafanyabiashara wajanja ambao wanatumia mwanya huo kupandisha vyakula kiholela kwa madai kuwa inachangiwa na usafirishaji kupanda pamoja na kukosekana kwa mazao ya kutosha msimu huu huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
"Wafanyabiashara wanatuumiza sana tumekuwa tukilazimika kununua bidhaa na chakula kwa bei wanayopanga wao kwani hata kama mwananchi mmoja akigoma, wengine ambao wana uwezo watanunua hivyo kutufanya sisi tunaotegemea mishahara ambayo ni ya kipato cha chini kuishi maisha ya tabu. Tunaiomba serikali itusaidie kudhibiti mfumuko wa bei ya vyakula hali ni mbaya hasa huku mikoani," anasema Haule.



Habari hii imeandikwa na Joyce Joliga wa Songea katika gazeti la mwananchi

7 comments:

Chacha Wambura said...

YN, je ni kwa sababu ya ramadan?

kama siyo basi hatuna mifumo madhubuti ndo sababu mfumuko wa bei umepanda kutoka 6% wakati awamu ya 3 inaachia madaraka mpaka 12 nukta kazaa wakati huu.

unatarajia hapo maisha bora yatakuja?

mafuta hapa musoma kwa mfano, ni sh 1700 kwa lita moja wakati mwanza ni sh 1500 naushei hivi. Cha kushangaza ni kuwa kuna depot hapa musoma ambapo baadhi ya vituo vya mafuta vya mwanza huchukua mafuta hapa, sasa swala linakuwa tatizo ni nini hasa?

ama ndo tumeshaanza kugharimia uchaguzi mkuu?

tafakari!

chib said...

Mfumuko wa bei upo kila mahali, ndio maisha bomoka kwa kila mtanzania

Anonymous said...

Na bado! wakulima wanalima kwa tabu, mbolea bei juu, hakuna anayewajali, mwaka jana mfuko mmoja wa mbolea ulikuwa unauzwa kati ya 50000/= na 70000/= hakuna aliyepiga kelele, sasa walifanikiwa kuvuna wanapouza bei juu kufidia gharama za uzalishaji watu mnaanza kupiga kelele, pigeni kelele zenu serikali iwasikie, lakini sisi wakulima ndio hivyo, tunapandisha bei na sisi! na kwa kuongeza tunalima zaidi mazao ambayo hayahitaji mbolea, tumechoka kutumika na kupewa sifa za kijinga eti "the big four" upuuzi mtupu!!

Markus Mpangala. said...

Blogu yako MAISHA, na kupanda bei huko ni maisha tu dadangu, naamini kila kitu kinawezekana kushuka. ndiyo Ruvuma yetu

Chacha Wambura said...

Mpangala, nakupinga kuwa kila kitu kinaweza kushuka...labda si Tz.

kupanda bei ni rahisi saaana lakini kushuka,mh!!!

PASSION4FASHION.TZ said...

Wambura kasema kweli,kwa Tz kupanda bei kitu ni rahisi sana,lakini kushuka ni ndoto.

Yasinta Ngonyani said...

Chacha Wambura inawezakana kutokana na ramadhani au kama labda ni kweli mvua nilikuwa haba na pia inawezekana kama mfano huo wa mafuta pengine ukienda mkoa mwingine bei itakuwa taofauti.

Chib, Ni kweli.

Usiye na jina twende polepole. Na yote usemayo ni kweli.

Markus, Maisha:-)

PASSION4FASHION.TZ, Shukurani. Maisha ni safari ndefu tutafika tu.