Monday, October 19, 2009

Salma: Kwa nini alifungiwa ndani kwa miaka 24?

Mlemavu wa viungo Salma Mkomwa

Mama yake asimulia kisa cha kupata ulemavu

SIMULIZI ya msichana Salma Mkomwa (26) wa Morogoro kufungiwa nyumbani kwao kwa miaka 24 bila kutoka ndani imewashtua wengi hasa baada ya kujitokeza kwenye vyombo vya habari kuomba msaada wa kumwezesha kujikwamua.
Wengi wamekuwa wakijiuliza kisa cha kufungiwa kwa msichana huyo mlemavu kwa kipindi chote hicho. Wapo waliowashutumu wazazi wake na wengine wakidhani kwamba walistahili kupewa elimu juu ya malezi ya mtoto wao badala ya shutuma, alimradi kila mtu alisema lake.
Ili kujua kisa na mkasa, nilifunga safari hadi Kijiji cha Kichangani, Morogoro anakoishi msichana huyo kujua kulikoni? Nilikutana na kuzungumza kwa kina na mama yake, Mwanangavia Sewa.
Alijibu swali la kwa nini alimfungia binti yake kwa miaka 24... "Hatukuwa na uwezo wa kufanya chochote na wala hatukujua hata pa kuanzia baada ya Salma kuanza matatizo haya. Sababu kubwa ni kwamba hali ilikuwa ngumu."
Baada ya majibu hayo, mama huyo alianza kueleza mambo ambayo anadhani ndiyo chanzo cha binti yake huyo ambaye ni mtoto wa pili kati ya sita aliojaaliwa kupata ulemavu huo.
Akiwa na mimba ya miezi tisa, alifunga safari ya kutoka hapo Morogoro kwenda Handeni, Tanga kwa ajili ya kujifungua. Anakumbuka hiyo ilikuwa mwaka 1982.
Wiki moja kabla ya kumpata mtoto huyo, alikwenda shambani kuvuna ndizi, baada ya kupata mkungu wake, alijitwisha tayari kwa safari ya kurudi nyumbani. Akiwa njiani alidondoka.
"Kama unavojua mambo ya kijijini nilijifungua kwa mkunga sikujifungulia hosipitali lakini mwanangu Salma alikuwa mzima kabisa" anasema na kuendelea:
"Lakini wiki moja baada ya kujifungua mtoto akawa analia kupita kiasi kuna kulia kwa mtoto kawaida lakini yeye alizidi hadi kuwashtua watu nyumbani. Tukampeleka Zahanati ya Mzindu, Handeni walipompima wakasema mtoto hana tatizo lolote, wakatupa vidonge lakini hali ilibaki vilevile."
"Baada ya mwezi mmoja miguu ilianza kuvimba usawa wa magoti. Ikabidi nifunge safari kurudi Morogoro na kwenda Hospitali ya Mkoa.
Nilipomfikisha akapigwa x-ray sehemu za magoti ili kujua tatizo. Majibu yakaonyesha kuwa sehemu hizo zimeachana na damu haitembei.
"Madaktari wakasema nimechelewa hawezi kunyooshwa tena mifupa imekomaa. Wakati huo alikuwa na umri wa mwezi mmoja. Nadhani hii yote imetokana na kutojifungulia hospitali labda tatizo lingeweza kujulikana mapema."
Baada ya majibu hayo ilirudi nyumbani. Hali ya Salma iliendelea kuwa mbaya. Aliishia kupewa dawa za kutuliza maumivu na kupunguza uvimbe uliokuwapo miguuni.
Alipofikisha miaka mitano alipata nafuu. Uvimbe ulikoma hata kulialia kulipungua. Wakati wote huo mikono yake haikuwa na tatizo hata kidogo lakini siku zilivyozidi kusonga nayo ikawa inajikunja pamoja na miguu.
"Madaktari walishindwa jinsi ya kufanya na hatukuweza hata kununua gari la kumsaidia ndiyo maana ilibidi akae tu ndani kwa muda wote huo."
Habari kuhusu Salma zilijulikana baada ya Taasisi ya Faraja Trust Fund ambayo inashughulika na watoto wanaoishi katika mazingira magumu kutembelea nyumbani kwao.
Hata hivyo, hawakuwa wamekwenda kwa ajili yake bali mdogo wake wa kiume ambaye amekataa kwenda shule akiwa darasa la tano.
"Ilikuwa kama ndoto na sitakuja kusahau siku ile ambayo alikuja mlezi kutoka Faraja ambaye alikuwa akishugulika na watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu na wasiopenda shule akiwemo mdogo wangu ndipo akanikuta," anasema Salma.
"Siku alipokuja nilikuwa ndani. Aliniona lakini aliondoka bila kuniambia kitu chochote hadi mwaka 2006 alipokuja tena na mama Ligaya alinipiga picha na kuipeleka katika Kituo cha Faraja."
Alipelekwa katika kituo hicho na baada ya kufika huko, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Lucy Nkya kwa kushirikana na shirika hilo walimpokea na kumpatia baiskeli pamoja nyuzi sita kwa ajili ya kuanza kufuma kwa kuwa tayari alikuwa na ujuzi huo.
"Namshukuru Mungu picha hizo zilipokwenda huko zilipokewa na hatimaye nilipata baiskeli ambayo inanisaidia katika maisha yangu kwani siwezi kutembea bila ya baiskeli."
Katika kipindi alichokuwa ndani alikuwa akijifunza kushona kwa kutumia chelewa za ufagio kwani hakuwa na uwezo wa kununua sindano ya kufumia vitambaa.
"Ninaweza kufuma vifuko vya kuhifadhia simu na tai na namshukuru Mungu naviuza Sh2,000 na watu wananunua. Shirika (Faraja), lilinipeleka katika maonyesho ya Sabasaba na hapo watu mbalimbali walielewa nini ninachofanya. Niliuza bidhaa zangu na kupata Sh200,000 na kupata msingi wa kuuza mkaa."
Fedha zinazopatikana katika shughuli zake wakati mwingine humsaidia mama yake ambaye ni mfanyabiashara wa mbogamboga hasa anapokosa bidhaa.
Salma hawezi kutembea wala kutambaa na hiyo ni changamoto kubwa katika maisha yake kwani anapokosa mtu wa kumsogeza alipo hulazimika kubaki hapo alipo liwepo jua au mvua.
Anayo tamaa kubwa ya kupata elimu lakini anasema wazazi wake hawana uwezo wa kumpeleka shule. Anatamani angejitokeza msamaria mwema kumsaidia pengine hiyo ingekuwa sehemu ya kujikomboa kimaisha.
"Nitashukuru pia kama nitapata mahala pa kuishi kwani hapa mazingira ni magumu. Baba ana wake wawili wote wanakaa katika nyumba hii na ana watoto 14 ambao wanamtegemea baba huyo na nyumba hiyo hivyo."
"Naomba tu Mungu mama yangu asitangulie mbele za haki kwani nitapata shida lakini kama nina nyumba yangu kidogo afadhali nitaweza kujisitiri."
Mwanamke aliyemfichua msichana huyo ni Jalia Lupapulo ofisa wa kituo hicho cha faraja chenye makao yake Kihonda, Morogoro. Anaungana naye kuomba wasamaria wema wamsadia akisema hajawahi kusoma. Kituo hicho hivi sasa kipo katika mchakato wa kumtafutia mwalimu maalumu.
Baadhi ya wataalamu wa tiba ya mifupa wanasema kwamba tatizo Salma linaweza kutibika kwa kupunguza kiwango cha ulemavu alichonacho.
"Nikimuona naweza nikajua tatizo ni nini hata kama ana umri mkubwa anaweza akasaidiwa tatizo likapungua ama siyo kwisha kabisa," alisema daktari mmoja.
Na Mahija Mpera gazeti la mwananchi

6 comments:

Anonymous said...

Maskini Dada Salma,pole zake sana.

PASSION4FASHION.TZ said...

Hii story ya huyu dada imenigusa sana,pole sana dada mungu atakusaidia.

Chacha Wambura said...

huu ni mojawapo ya ujinga mkubwa wetu siye binadamu kwa kudhani jambo lisilo la kawaida huwa ni mkosi.

need to think twice.

Pole sana da Salma

chib said...

Kila binadamu ana kasoro fulani kimaumbile na kiakili. Lakini kila mmoja wetu ana nafasi yake katiaka kutoa mchango wake katika jamii kimawazo, kiutendaji na hata kuwepo kwake duniani.
Hakuna haja ya kuficha mlemavu. Chacha unaonekana umekasirika kabisa kama watu wa kule Shirati, ndio hivyo, watu wengine fikra, duni kaka

Chachac Wambura said...

Chib, sijakasirika ila tu statement imeonekana kama imepinda vile kama wapindavyo wanasiasa wetu wa siku hizi...lol

Yasinta Ngonyani said...

Ahsanteni wote nichukue nafasi hii na kusema pole sana Salma kwa kutofaidi maisha yako na wakati kuna uwezekano. Na pia nakupongeza sana kwa kuwa na moyo huo ulionao. Nakutakia kila la kheri na lolote ufanyalo Mungu akuongoze.