Ni miaka karibu 15 sasa inakaribia tangu nilipoingia hapa Sweden. Na ni miaka 6 imepita tangu niwe mwanafunzi yaani kukaa darasani na kubukua.
Kuna kitu nataka kuwasimulia ambacho nilikiona miaka sita iliyopita wakati nasoma. Katika darasa letu tulikuwa wanafunzi mchanganyiko, wenyeji na wahamiaji. Kwa hiyo siku hiyo kulikuwa na somo la mila na desturi. Ilikuwa tuangalie filamu inayoonyesha mambo ya hali halisi. Basi tukawa tunaangalia hiyo filamu ambayo ilikuwa inahusu maisha ya mwanadada mmoja (jina linahifadhiwa) ambaye alikuwa akiishi na wazazi wake na alikuwa mtoto pekee katika familia ile.
Mwanadada huyu alikuwa hana maisha ya kawaida. Alikuwa mlevi na mvutaji yaani si sigara tu na madawa ya kulevya alikuwa anatumia. Sasa, kibaya zaidi alikuwa akiwaibia wazazi wake vito vya thamani, na kuuza ili kupata pesa na kwenda kununu hayo mahitaji yake na pengine aliiba pesa pia. Ila alikuwa mwema alikuwa akiwapa rafiki zake pia.
Kwa tabia hiyo ilifikia mahali wazazi walishindwa kumvumilia wakamtimua pale nyumbani na akawa hana sehemu ya kuisha. Akawa analala vibarazani bila hata hata ya kuwa na shuka ya kujifunika, chakula hana na anachovaa hakieleweki…...Siku zikapita.......
Maisha yakazidi kuwa magumu, siku moja akaamua kurudi kwa wazazi wake na kusema ameacha ile tabia. Wazazi wakawa shingo upande ila kwa vile uchungu wa mtoto wanaujua wazazi wakampokea. Siku zikapita lakini ghfla siku moja akabadilika na kuanza tena ila tabia. Kama tusemavyo ukionja asali ni ngumu kuacha. Akawa anaiba vito tena na kuuza ili kupata pesa za pombe na madawa ya kulevya.Wazazi walivumilia, lakini mwisho walishindwa na wakamfukuza tena. Akawa hana kwa kwenda isipokuwa kule mitaani kuungana na marafiki na kuendela kulala vibarazani kama awali.
Mnajua ni jambo ambalo mimi sijaelewa mpaka leo katika kutafakari kwangu. Kwasababu mimi naona hapa sweden kuna misaada mingi ya kuwasaidia watu wa aina hii na nilishangaa kwa nini naye asingetafutiwa msaada? Ukizingatia wazazi wake walikuwa na uwezo na pia alikuwa mtoto pekee wanamwacha na kuwa mlevi tu??
Cha kushangaza zaidi ni kwamba hazikupita siku nyingi wazazi wa mwanadada huyu walijitafutia mbwa. Wakamnunulia mbwa huyo vitu vizuri vya kuchezea, sehemu nzuri ya kulala na chakula kizuri pia alipata. Wakati binti yao yupo hatarini hana chakula, hana mavazi wala sehemu ya kulala.
Hapo ndipo nilipokuja amini sisi binadamu tupo tofauti sana katika kuthaminiana. Mbwa/wanyama wanathaminiwa kuliko binadamu tena mwanao? Kazi kwelikweli!! Ila siku ile nililia sana kwa vile niliguswa sana na nilifoka sana darasani. Mwalimu wangu akanituliza na kuniambia karibu Sweden, Habari ndio hii. Je? Wenzangu mngejisikiaje?
8 comments:
Dada ndio mambo ya Ulaya hayo sasa tizama kama wataweza kumwacha mtoto wao wa kumzaa..Na kutomjali..Jiulize watakujali wewe mwamiaji(ngozi nyeusi) pamoja na hawo wakimbizi
Hii kali kweli jamaa wana roho za ajabu ndio maana wanamhudumia mbwa badala ya kumpeleka mtoto wao kwenye kitengo cha kumsaidia kuachana na ulevi
Sijui ndio maendeleo ya kupindukia au... Watu wamekuwa na roho mbaya na akili mbovu kuliko za hata hao wanyama
wangenga alisema ukistaajabu ya musa utayaona ya firauni.
Kulia kwako na kufoka ni kumpigia mbuzi gitaa tu..hakuna kitachowabadilisha....Naona kwa mika uliyokaa hapo bado ujakutana na mabo ya sweden.......
Mimi wala sishangai ndio tabia zao hao,huwa hawana ule upendo wa dhati.
kazi kweli kweli, ama kweli majuu hamnazo. Nimekumbuka nchi fulani niliyowahi kuishi huko Ulaya, katika nchi hiyo omba omba wananufaika na mkanganyiko wa kisheria na pia huruma ya binadamu kwa wanyama kuliko binadamu wenzao. Katika hiyo nchi, ni kosa kwa askari kumpeleka mbwa kituo cha polisi kama hajasababisha madhara kwa binadamu, pia ni kosa kumpakia mbwa pamoja na binadamu katika gari moja na kuwapelka polisi. Sasa basi utakuta kila omba omba anakuwa na mbwa na kukaa kuomba, sasa polisi wakifika wanashindwa kumkamata kwa vile watampeleka wapi mbwa wake wakati hajasababisha madhara kwa binadamu? hivyo jamaa wanapeta tu, na pia hao mbwa hutumika kama chambo ya kupewa misaada maana wazungu wanamuhurumia zaidi yule mbwa kuliko binadamu, hivyo jamaa wanakula kwa mgongo wa mbwa!!
Napenda kuchukua nafasi hii na kuwashukuru wote kwa mchango wenu nimejifunza kitu. Na nashukuru kuwa binadamu tupo tofauti hapa duniani. Na pia tuna mila na desturi tofauti.
Post a Comment