Friday, December 5, 2008

MAPENDO NI KITU GANI?

Tunaona hili neno "Mapendo" likiwa limeandikwa mahali pengi sana. Tunaliona katika magazeti kila siku. Tunaliona kwenye sinema, mara nyingi hata sisi tunalitumia, pengine hata bila kujua maana yake.
Kitu hiki kiitwacho "mapendo" ni nini hasa ? Ni neno dogo sana. Katika lugha yetu labda hakuna neno linalotumiwa na keleweka vibaya kama hili.

Tuangalia mfano huu:- Mvulana mdogo anamwambia mwalimu wake kwamba anapenda pipi. Msichana mdogo anasema kwamba anapenda mtoto wake wa bandia. Mtu mwingine anasema napenda viatu vyenye visigino virefu ambapo mwanamke "yule" naye anasema kuwa anapenda kutazama vitu vizuri kwenye madirisha ya maduka. Mwingine anapenda joto la kiangazi, mwingine mvua za masika. Je? wote hawa wana maana gani wasemapo kwamba wanapenda?

Kwa ujumla, twaweza kusema kuwa tunatumia neno "mapendo" juu juu tu na mara nyingi bila kuelewa maana kubwa ambayo neno hili dogo linalo. Mapendo ni mojawapo ya nguvu kubwa zilizomo ndani ya moyo wa mwanamume na mwanamke. Kupenda kwa nguvu zote za moyo wa mtu. Lakini kupenda kwa moyo wote ni kitu ambacho lazima tujifunze kidogo kidogo.

Hatua za kuelekeza kwenye upendo wa kweli
upendo, kidogo wafanana na ngazi:- una hatua mbalimbali.

Hatua ya kwanza ya upendo tunawea kusema ni kama ule wa mtoto mdogo. Upendo wa kutaka kupokea. Anakuwa na furaha kwa sababu amepewa kitu.

Hatua ya pili, upendo unaanza kuangalia kandokando; ni wakati ambapo mtoto huanza kutoa kwa wengine. Ndipo mtoto hugundua urafiki. Sasa mtoto anakuwa na furaha kwa sababu ametoa kwa mwingine kitu kilichokuwa chake mwenyewe na kumfurahisha mwingine. Mtoto amejifunza sasa sehemu muhimu sana ya upendo wa kweli.

Hatua ya tatu ni ile ambapo mtu anakuwa tayari kwa vyote viwili, yaani kutoa na kupokea. anakuwa tayari kutoa ili apate kumfurahisha mwingine; lakini pia anakuwa tayari kupokea kitu na ndiyo namna nyingine ya kumfurahisha mtu wakati mwingine. Sasa amekwisha gundua siri mojawapo kubwa ya maisha, siri iliyo katka kiini cha upendo wa kweli.

Kwa maneno rahisi tungesema kuwa, Kupenda ni kutoa. Lakini pia ni vigumu. Kupenda ni kutoa. katika kupenda ni lazima kutoa, kutoa kile kitu ambacho labda unakihitaji ama usingependa kukitoa. Upendo ulio mkubwa zaidi na wa ndani zaidi ndio ule wa kujitoa nafsi yako kwa ajili ya heri ya mtu mwingine.

Kutoa ndio kiini cha upendo. Ile hali ya kutaka kupokea tu kwa mwengine ni ubinafsi na upendo wa kibinafsi. Upendo hutazama kwa mwingine, kwa yule mpendwa, na kuuliza; Nitatoaje zaidi ili mwenzangu awe na furaha zaidi? Ambapo ubinafsi na kujipenda binafsi hujiuliza na kupanga namna ya kupata vitu. Nitafanyaje ili niweze kupata zaidi kutoka kwa mwenzangu? Mambo haya mawili , kama uyaonavyo ni tofauti sana.

Itaendelea...........

3 comments:

Fadhy Mtanga said...

Da Yasinta ahsante sana kwa mada yako ya leo. Kupenda.
Kupenda, kwa mtazamo wangu ni hisia fulani zenye nguvu ndani ya moyo wa mtu zinazompelekea kuwa na hali ya tofauti kwa mtu mwingine. Labda niseme ni hali ya nafsi inayomwongoza mtu kumfurahia mtu mwingine na kuwaza mema juu yake. Lakini pia, kwa mtazamo wangu jamani, kupenda ni kuwa mtumwa wa hiyari wa jambo fulani.
Huu ni mtazamo wangu mtani.
Ni hayo tu.

Christian Bwaya said...

Asante sana Yasinta kwa mada murua. Upendo.

Umefafanua vyema sana. Hongera. KUmbe kupenda katika hatua ya juu, ni kuwa tayari kutoa. Watu wengi huwa na mawazo ya kupokea zaidi. KUmbe kufanya hivyo si kupenda.

Nadhani tukitaka kupokea zaidi, kw amujibu wa uchambuzi wako Yasinta, ni lazima tutoe zaidi, hivyo tutapokea zaidi. Tukipokea zaidi, tunajiskia kutoa zaidi na kuendelea. Asante sana kwa kutuelimisha.

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli Fadhy kupenda ni mamlaka, enzi amri na nguvu hapa duniani. asante

Bwaya ni kweli ni lazima kutoa kwanza ndipo utapata zaidi. asante nawe kwa kupitia hapa.