Saturday, December 20, 2008

INAENDELEA TOKA JINSI YA KUPEANA HABARI KATIKA MAISHA YA NDOA:- NI LINI TUPEANE HABARI?

Kuna mambo yawezayo kuongelewa kila wakati, kuna taarifa na habari tunazoweza kutaja wakati wowote. Kuna mambo mengine – yaliyo magumu zaidi kuongelea – nayo yanahitaji wakati wa pakee. Mume amwambiaye mkewe kuwa si mpishi hodari, hapo akijua kwamba mke wake amechoka sana siku hiyo, hatumii busara katika kupeana habari. Hali kadhalika, mwanamke atafutaye nauli ya kwenda nyumbani kwao akijua kwamba mumewe amekula hasara katika biashara yake juzijuzi tu, bibi huyu hatumii busara pia.

Kuna nyakati nzuri za kusema kitu na kuna nyakati mbaya za kufanya hivyo, yaani wakati unaofaa na usiofaa kusema jambo fulani. Mara nyingi mazoea ya maisha ndiyo yanayotufundisha. Maisha ni mwalimu wa waalimu. Mambo ambayo ni magumu kuyasema, kwa sababu yaweza kumshangaza ama kumwumiza mtu, yasemwe wakati ambapo yule mtu yuko katika hali ya kuweza kuyapokea. Jaribu kupata mzuri zaidi wenye hali ya utulivu mwingi ndipo mzungumze naye pamoja juu ya matatizo yaliyopo. Kwa mfano, wakati ambapo yupo tayari kukusikiliza, akiwa hana wasiwasi juu ya mambo mengine, wakati ambapo anajisikia vizuri

Kuna njia moja ya kufanikiwa katika kupeana habari, njia ya kufaulu kujenga uhusianao wa mapendo, nayo ni kusikiliza kwa upendo na kusema kwa upendo. Maana yake, kuwa na usikivu na pia kumjali mwenzangu. Ninamsikiliza si kwa masikio tu bali hata kwa moyo, tujitahidi kukisia maana iliyofichika ndani ya maneno anayosema.

Kuna wimbo unaojulikana sana usemao, “Watu wanaosikiliza bila kusikia, watu wanaoongea bila kusema kitu....” Mara nyingi tunakuwa hivi, watu wenye kusikiliza bila kusikia na kuongea bila kusema kitu. Maana yake ni kwamba tunasikiliza maneno lakini hatusikilizi kwa makini ya kutosha ili maneno hayo ytoe maana halisi kwetu.
Na mara nyingi tunaongea tu bila ya kufikiri tunalosema na bila kumfikiria huyu ambaye tunasema naye. Tumezoea kuongea lakini hatukuzoea kupeana habari itakiwavyo. Kuna tofauti kubwa hapa.

Mara nyingi pia hatujui jinsi ya kusikiliza. Ni ya maana sana kwangu ikiwa naongea na mtu mwingine, kujua kwamba ananisikiliza kwa uangalifu kweli au nusunusu tu. Nusu ya mafanikio katika kupeana habari kwa namna bora yatokana na kusikiliza vizuri. Ninaweza kushirikiana kimawzao kweli kama ninaweza kujiingiza mwenyewe akilini na moyoni mwa mtu, kama ningelikuwa moyoni mwake kabisa na kuona mambo jinsi ayaonavyo yeye.

Kupeana habari ni kitu kisichokoma, lazima kiendelee. Huwezi kamwe kusema, “Najua mambo yote juu yake.” Au, “Namjua kabisa kwani si tulifunga ndoa miaka 10 iliyopita.” Hapana. Siku kwa siku mabadiliko hutokea kwako na kadhalika kwa mwenzako hubadilika pia. Hili ni mojawapo la mambo ya ajabu sana katika ndoa yako, kwamba kila mara yapo mambo mapya ya kuvumbuliwa, mambo ya kuongea pamoja.

Kupeana habari kusipofanyika siku kwa siku utashangaa siku moja na kushtuka kuona kuwa mwezi wako ni mgeni kabisa na mgeni huyu si mwingine bali ni mume wako au mke wako. Kwa sababu tu, wakati fulani mliacha kupeana habari, mliacha kuongea pamoja juu ya namna mnavyofikiri, jinsi mnavyojisikia, mambo mnayotumaini.

Ni jambo la kusikitisha kweli kuona kwamba wapo watu wengi wa ndoa wanaishi pamoja, hula,hufanya kazi na kulala pamoja lakini kwa kweli hawaongei pamoja. Wanaongea, ndiyo, lakini siyo juu ya mambo yanayowapenya mioyoni mwao. Hawathubutu kungea waziwazi juu ya mambo yanayowafanya wasisikie wenye upweke, kutoeleweka na wenye huzuni. Na maisha yao ya ndoa hayana maana tena. Hatuwezi kupeana habari baada ya mwezi au juma. Kupeana habari ni chakula cha kila siku cha ndoa yako.