Friday, March 1, 2013

Inuka Twende Ni Kwa Walioagana​- MAGGID MJENGWA

Ndugu zangu,
Hakuna wawili watembeao pamoja pasi na maelewano.
Ukiwaona wanadamu wawili wanatembea pamoja, basi, wana makubaliano. Ni watu waliopatana.
Kwenye kundi la watu wa mataifa tofauti ukimsikia Mtanzania anamtamkia Mtanzania mwenzake, tena kwa Kiswahili; " E bwana inuka twende zetu!", na Mtanzania huyo mwingine akabaki amekaa bila kushtuka, basi, utilie mashaka UTanzania wake.
Ndio, " Inuka twende ni kwa waliogana". Ni watu wenye kufahamiana. Ni ndugu.
Nimeanza kuingiwa na hofu kuwa Watanzania tumeanza kupoteana kama ndugu. " Inuka twende' yetu imeanza kuangaliwa kwa sura ya udini, ukabila na itikadi.
Hatujafika pabaya sana, lakini, tunakoelekea ni kubaya. Tumeshaziona ishara. Miongoni mwetu Watanzania tumeanza kuzisikia kaauli za ; " Umewasikia jamaa zetu Wakrito? Umewasikia jamaa zetu Waislamu? Umewasikia jamaa zetu WaZanzibar? Umewasikia jamaa zetu wa Bara?......"
Hizi ni ishara za undugu unaosambaratika. Zamani sisi sote tulikuwa ni ndugu. Tulitembea pamoja, ishara ya watu tuliopatana.
Leo kuna Watanzania wanaoambiwa; " E bwana wee, siku hizi nakuona unatembea na kuongea na wale jamaa zetu wa upande mwingine!"
Ndio, Watanzania tumeacha kuwa ndugu. Tunagawanyika kwenye mapande. Ni kwa kuzitazama tofauti za dini, kabila na itikadi.
Hatujafikia pabaya, lakini, tunakoelekea ni kubaya. Tukumbuke; " Inuka twende ni kwa waliogana". Watanzania tulishaagana. Tulishakubaliana. Tulijua tunakokwenda kama Taifa. Kama ndugu. Tumeanza sasa kusambaratika.
Tuinuke sasa twende kupambana na yote yenye kutugawa kama ndugu wa taifa moja. Tuna kila sababu, nia na uwezo wa kushinda mapambano haya dhidi ya ubaguzi wa aina zote.
Na hilo ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
mjengwablog.co.tz

2 comments:

ray njau said...

Je, Ni Afadhali Kutokuwa na Dini?
=================================
Hata watu fulani wamefikia mkataa kama wa mwanafalsafa Mwingereza Bertrand Russell kwamba ingekuwa afadhali kama mwishowe “dini zote zingetoweka.” Kulingana na maoni yao, suluhisho la matatizo yote ya wanadamu ni kuondolewa kwa dini. Hata hivyo, huenda wakaamua kupuuza ukweli kwamba wale wanaokataa dini wanaweza kusababisha chuki nyingi na ubaguzi kama vile tu wale wanaoiunga mkono. Mwandishi wa masuala ya kidini Karen Armstrong anatukumbusha hivi: “Angalau Maangamizi Makuu yalionyesha kwamba imani zisizo za kidini [zinaweza] kuwa hatari kama tu vita vya dini.”—The Battle for God—Fundamentalism in Judaism, Christianity and Islam.
Kwa hiyo, je, kwa kweli dini ina uvutano mzuri au ndiyo chanzo cha matatizo ya wanadamu? Je, suluhisho la matatizo hayo ni kuondoa dini zote?

ray njau said...

UBAGUZI WA KIDINI
===================
Kitabu The Nature of Prejudice kinasema: “Chuki hutokea watu wanapotumia dini yao kutetea [ubinafsi] na mapendezi ya kikabila. Hapo ndipo dini na ubaguzi hupatana.” Kitabu hichohicho kinasema kwamba jambo linaloshangaza zaidi ni jinsi watu wengi wanaodai kufuata dini “wanavyopoteza sifa zao za kiroho kwa urahisi na kuwa na ubaguzi.” Jambo hilo linaonekana wazi katika dini za watu wa rangi moja, chuki na jeuri kati ya vikundi vya kidini, na ugaidi unaochochewa na dini.

▪ Biblia inasema nini? “Hekima inayotoka juu [kwa Mungu] . . . ni . . . yenye kufanya amani, yenye usawaziko, . . . haifanyi tofauti zenye ubaguzi.” (Yakobo 3:17) “Waabudu wa kweli watamwabudu Baba kwa roho na kweli.” (Yohana 4:23) ‘Wapendeni adui zenu na kusali kwa ajili ya wale wanaowatesa ninyi.’ (Mathayo 5:44) Jiulize hivi: ‘Je, dini yangu inanichochea kuwapenda watu wote kikweli, kutia ndani hata wale ambao huenda wakataka kuniumiza? Je, dini yangu inamkaribisha kila mtu bila kujali taifa, rangi, jinsia, hali yake ya kiuchumi, au ya kijamii?’