Monday, October 1, 2012

KUMBE KUNA:- KIMWAGA MDADISI!!!

Jumatatu ya leo nimeona turudi nyuma kidogo ...kumbe kuna KIMWAGA MDADISI  pia sio KAPULYA MDADIDI TU....Hadithi hii kutoka kitabu cha JIFUNZENI LUGHA YETU KITABU 5...KARIBUNI
------------------------------------------------------------------------------------------------------------

 KIMWAGA NA BABU YAKE
HAPA NI KITABU CHENYWE KWA MBELE
Hapo zamani palikuwa na mtoto mmoja akiitwa Kimwaga. Mtoto huyo alimpenda sana babu yake Lukindo. Kimwaga na babu yake waliishi katika kijiji cha Kwemasafi, Wilayani Korogwe. Jioni, baada ya jua kuzama, Kimwaga alikuwa akikoka moto kwenye kibanda chao cha mazungumzo. Babu yake alikuwa akipenda sana kuota moto na kuzungumza na mjukuu wake.
Siku moja jioni, Mzee Lukindo na Kimwaga walikuwa wakiota moto. Kimwaga alikuwa mtoto MDADISI sana. Alimsimulia babu yake habari moja iliyomshangaza. Alisema, "Babu, leo tulikuwa tukilima katika shamba letu la shule. Mimi niliinua jembe kwa nguvu ili nichimbue magugu. Jembe likagonga jiwe, nikaona cheche za moto zinamulika. Hivi babu moto ulitoka wapi?
Babu yake akamwuuliza, "Hivi mjukuu wangu hujui hadithi ya moto?" Kimwaga akamjibu, "Sijui. "Babu yake akamwambia, "Basi nikueleze kidogo. Hapo zamani za kale binadamu hawakuwa na moto. Waliishi katika mapango yenye giza. Walikula matunda na nyama mbichi. Maisha yao yalikuwa ya taabu sana.
"Kwa bahati, siku moja mzee mmoja akachukua mawe, akayagongagonga ili yavunjike apate jiwe la kuchimbia viazi mwitu. Alipoyagonga aliona yakitoa cheche za moto. Alifikiri sana. Halafu akaweka manyasi makavu karibu na yale mawe, na akaendelea kuyagongagonga. Mara yale manyasi yakawaka moto. Kumbe alikuwa amegundua moto kama ulivyoona wewe leo wakati ulipolima huko shuleni."
Kimwaga akamwambia babu, "Kumbe hata mimi nimegundua moto." Kisha akaendelea, "Babu, juzi tulipokuwa tunatoka shule tulinyeshewa na mvua, tukalowa. Tulipofika kwenye shamba moja tulijificha chini ya kibanda kimoja kidogo. Mwenzetu Kimweri akapekechapekecha vijiti viwili vikavu. Mara tukapata moto, tukautumia kwa kukaushia nguo zetu. Je, babu moto ule ulitoka wapi?"
Mzee Lukindo akasema, "Aaa, wewe Kimwaga unadadisi sana. Basi sijakueleza hadithi nyingine. Hapo zamani sana, kabla mimi sijazaliwa, palikuwa na mtoto mmoja mtundu sana. Siku moja alitaka kutoboa kigogo kikavu ili atengeneze kidude cha kuchezea. Akachukua kijiti akaanza kupekecha. Kile kigogo kikatoa unga mweusi. Akaendelea kupekecha kwa nguvu sana. Akaona moshi. Mwisho ule unga mweusi ukashika moto. Akachukua nyasi kavu na kuziweka karibu na ule unga. Nyasi zikawaka moto. Kumbe naye alikuwa amegundua moto."
Siku nyingine tena, Kimwaga akamweleza babu yake namna alivyomtazama buibui. Akamwuliza babu yake , "Je babu, ule uzi ambao buibui hujengea nyumba unatoka wapi?" Mzee Lukindo akajibu, "Buibui ni mdudu wa ajabu. Anapotaka kujenga nyumba yake hutoa maji kutoka tumboni mwake. Maji haya yanapotoka nje tu huganda, na anapokwenda huonekana uzi."
Babu yake Kimwaga alipomaliza kusimulia habari za buibui, Kimwaga alikuwa anasinzia kwa sababu siku ile alichelewa sana kwenda kulala. Mzee Lukindo akamwambia, "Sasa mjukuu wangu, nenda ukalale. Nitakueleza hadithi nyingine kesho," Kimwaga akaenda zake kulala.
JUMATATU NJEMA KWA WOTE...

2 comments:

ray njau said...

@Yachinta npe chitabu nchome nwaphundiche wajinga;ai chindimba.....................x2.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Ray! Duh umenikumbusha wimbo huu ngoja nimalize kwechukwechu ngoma ya kimakonde....