Thursday, October 21, 2010

NDOA YA MALAIKA HAIJAWAHI KUWEPO DUNIANI


Wakati mwingine misukosuko ya ndoa huwaliza wanawake,
lakini hizo zote ni changamoto !
Kuna kudanganyana kwingi kuhusu ndoa pale mtu anaposhindwa kuwa mwangalifu sana kwa kauli za wengine walio kwenye ndoa. Hii hutokana na ukweli kwamba kuna kujumuisha kwingi sana. Kuna wakati huwa tunasikia au kuambiwa kwamba ndoa ni sawa na jehenamu. Baadhi ya watu walio kwenye ndoa kuna wakati huzungumza kwa njia ambayo hutufanya tuamini kwamba kuoa au kuolewa ni jinai. Ndoa ni ujinga mtupu haina maana, mtu anaweza kusema. Wasemaji hawa wanaweza kuwa ni watu tunaowaamini sana kama wazazi wetu na wengine wa aina hiyo.
Baadhi ya watu badala ya kuponda na kubeza kuizungumzia kama kitu kizuri sana kisicho na doa wala chembe ya usumbufu. Inawezekena kabisa nasi tukawaamini wazungumzaji hao, hivyo kuamini kwamba, ndoa hazina usumbufu.
Inawezekana dhana hii ikaingizwa vichwani mwetu wakati tukiwa wadogo au hata tukiwa watu wazima. Hebu fikiria juu ya mtu ambaye anajisifu kwamba ndoa yake haina hata chembe ya mkwaruzo. Ambaye anaieleza ndoa yake kwa njia yenye kushawishi kuwa, kumbe ndoa zenye matatizo siyo ndoa bali kisirani kitupu. Kama nawe uko kwenye ndoa na ndoa hiyo ina matatizo hata madogo unaweza kudhani kwamba ulikosa kuoana na huyo mwenzako. Dhana hiyoinaweza kuchipuka kutokana na kauli kama hiyo inayoelezea ndoa kama kitu kisicho na mikwaruzo hata kidogo.
Kama usipokuwa mwangalifu unaweza kuacha kuchukua hatua za kujaribu kuondoa tofauti zilizo kwenye ndoa yenu. Utaacha kufanya hivyo kwa sababu mtu fulani atakuwa tayari ameingiza kichwani mwako uongo kwamba ndoa ni “asali” na “maziwa” matupu. Ni uongo kwa sababu hakuna ndoa isiyo na mikwaruzo.
Tunatakiwa kujua kwamba lengo la ndoa siyo kuepuka kukorofishana , hapana . Ukweli ni kwamba kukorofishana kunapotumiwa vema huweza kujenga uhusiano mzuri na imara sana. Kwa sababu kukorofishana hakuwezi kuepukika kwenye ndoa kunatakiwa kutumika kama shule na dawa ya kuimarisha ndoa.
Bila kukwaruzana kwenye ndoa zetu inaweza ikawa vigumu sana kwetu kubandua tabaka la uongo lililotufunika ambalo humfanya kila mmoja kati yetu kushindwa kuona na kumfahamu mwenzake katika tabia yake halisi.
Bila kukwaruzana, kila mmoja wetu atajidanganya kwamba anamfahamu mwenzake kama alivyo wakati siyo kweli. Tunapokwaruzana tunapata nafasi ya kufahamiana vizuri katika hali halisi.
Mwanamke mmoja maarufu aliwahi kuulizwa kama huwa anakwaruzana na mumewe. Alikiri kwamba huwa wanakwaruzana kwa kusema , “ndiyo tunakwaruzana, vinginevyo tungekuwa hatuna tofauti, na hapo bila shaka ndoa na maisha vingekuwa vimepooza sana”. Huo ndiyo ukweli wenyewe, kwamba bila kukwaruzana hatuwezi kufahamiana vema na kujua kwa undani tofauti kati yetu na wenzetu.
Inabidi tujue kwamba hakuna binadamu aliyekamili, yaani asiyekosea, kama ilivyo dunia yenyewe. Kwa hali hiyo hakuna ndoa ambayo haina makosa, kwa sababu ndoa ni binadamu hao ambao siyo kamili. Kwa hiyo, mtu anapotarajia kuwa au kuishi kwenye ndoa isiyo na kukwaruzana, ni sawa na mtu huyo kutarajia kukutana na binadamu ambaye ni kamili, yaani asiyekosea.
Kutarajia kuwa na ndoa ambayo haina kukwaruzana kunaelezwa kuwa ni chanzo kizuri sana kwa ndoa nyingi kulegelege au kuanguka kabisa. Mtu anapoingia kwenye ndoa akitarajia kwamba huko hatapambana na maudhi au kero za aina fulani, ni lazima ajue kwamba, hatadumu kwenye ndoa yake kwa sababu ndoa hiyo anayoitarajia haipo.
Mtu ambaye hakubali au angalau hataki kuelewa kwamba, ndoa ni lazima iwe na mikwaruzo anaweza kukabiliwa na tatizo lingine baya zaidi kwenye ndoa yake. Kwa kutokujua au kuepuka kukwaruzana, hawezi kuwa tayari kukubali kujadili migogoro ya kindoa ili kupata ufumbuzi. Hawezi kulikubali hilo kwa sababu haamini kwamba ndoa yenye kukwaruzana ni ndoa.
Wakati mwingine rafiki, ndugu au jamaa zetu hutusimulia jinsi ndoa zao zisivyo na kukwaruzana kama kwamba ni za malaika watupu. Bila kujua, huwa tunajikuta tumewaamini. Tunapowaamini huwa tunachukulia kukwaruzana kuliko kwenye ndoa zetu kama jambo au kitu ambacho hakikutakiwa kuwepo. Hapo hujikuta tukitamani kuondoka kwenye ndoa hizo kwa matarajio kwamba tunaweza kukutana na “malaika” ambao tutajenga nao ndoa zisizo na doa.
Hata pale ambapo tunasema wanandoa wanapendana sana, bado ndoa yao ni lazima itakuwa na kukwaruzana. Lakini wanachofanya hawa na ambacho huenda wengine hawafanyi ni kujadili tofauti hizo sawia na kuamua kuzisahau na hapo wote kukubali kujifunza kutokana na tofauti hizo.
Wale walio tayari kujadili tofauti zao sawia ndiyo ambao ndoa zao huwa na afya sana hadi wengine kushangaa kama siyo pamoja na kuona wivu. Wale wanaodhani ndoa ni mahali pa kila jambo kwenda kama mtu atakavyo, ndoa zao hupogoka vibaya na kufa kwa kishindo........

Makala hii nimeitoa katika Gazeti la Jitambue la hayati Munga Tehenan.

3 comments:

emu-three said...

Ndoa ni mjumuiko wa watu zaidi ya mmoja, na haiwezekani kuwa wanajamii hawa wakawa na uoni mmoja, sidhani. Kama ni hivyo, kusigishana na kutokujua undani wa mwenzako kunazaa mtafaruku!
Mtafaruku huu unategemeana na ufahamu wa kila mmoja, wengine wanaweza kufahamiana na wengine ufahamu wao ukawa mdogo, na hapo ndipo migongano inapofika pabaya!
Nini kifanyike ni kukaa na kuambizana, na kama mnjua nini maana ya ndoa basi tatizo hakuna, lakini wengine hawataki kushuka chini, kutokana na ufahamu huo mdogo, kila mmoja anataka kumpanda mwenzake, ....hapo ipo kazi!

ADELA KAVISHE said...

nimeipenda sana hiyo my dia ujumbe mzuri,,kujitambua ni jambo la muhimu sana katika mahusiano na uvumilivu pia kwani watu wengi sana wanalia katika mahusiano kilakukicha wengine kabla ya ndoa mnaumizana je mkiingia kwenye ndoa itakuwaje si ndio balaa.na muhimu kuchunguzana kabla ya kuingia kwenye ndoa.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

ukijitambua mambo yote unaona kama sarakasi!!!