MATANGAZO

Tuesday, May 19, 2009

LEO TUANGALIE MAMBO YA MAPISHI PIA KWANI BILA KULA HATUWEZI KUISHI

Chakula chenyewe si kingine ni Maandazi

5 VIKOMBE VYA UNGA WA NGANO.

* 1 ¼ VIKOMBE VYA TUI LA NAZI ZITO VUGU VUGU.

*3/4 KIKOMBE CHA SUKARI.

* 3 VIJIKO VYA KULIA VYA SAMLI ILIYOYAYUSHWA AU MAFUTA

*1 KIJIKO CHA SOUP HAMIRA.

*1/2 KIJIKO CHA CHAI CHA HILIKI YA UNGA.

*MAFUTA YA KUKAANGA.

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA:

1.Ndani ya kibakuli kidogo, mimina hamira na na vijiko viwili vya kulia vya tui. Weka kando mpaka hamira ianze kufura, kama dakika 5-10.

2.Pasha samli moto

3.Ndani ya bakuli kubwa au sinia, changanya unga, sukari, iliki na samli ikiwa bado moto moto.

4.Mimina hamira ndani ya mchanganyiko wa unga. Changanya na ukande huku ukitumia lile tui la nazi. Tui likipungua unaweza ukaongeza maziwa. Kanda unga mpaka uwe laini.

5.Kata madonge *12 au 15 uyaweke kwenye baraza iliyonyunyiziwa unga na uyafunike ili yapate kufura na yasikauke.

*Ukipenda maandazi manene fanya madonge 12. Ukipenda mepesi fanya madonge 15


Kabla ya kuumuka (kufura)

Baada ya kuumuka (kufura)

6.Madonge yakifura, sukuma kama chapati kisha ukate mara nne kama kwenye picha. Endelea kufanya hivyo na madonge yote. Yawache maandazi yafure tena baada ya kukata kama dakika 15 hivi.


7. Pasha mafuta moto kwenye karai. Maandazi yako tayari kukaangwa sasa.

8.Kaanga maandazi kwenye mafuta ya moto. Upande mmoja ukifura na kuwa rangi nzuri geuza upande wa pili. Endelea nama hii mpaka maandazi yote yawe tayari.



TIPS ZA KUHIFADHI MAANDAZI

1.Unaweza kuweka unga wa maandazi uliyokwisha kuyakata ndani ya freezer yakisha umukua ikiwa unataka kutumia siku nyengine. Tumia waxed paper na unga wa kutosha kuweka katikati ya maandazi ili yasishikane unapoya freeze kwanza katika freezer. Yakishika barafu, toa na yafunike kwa wax paper kiasi kama matano pamoja na uyatie katika freezer bags. Ukitaka kukaanga maandazi siku nyengine, toa maandazi mapema kidogo yatoke barafu kidogo tu. Pasha mafuta moto kwenye karai na kanga maandazi.

2.Vile vile unaweza kuyapika kabisa na kuweka katika freezer bags, ukitaka kutumia ni kuyatoa tu na kupasha moto katika Microwave.

13 Maoni:

Bennet said...

Mimi nimezoea neno kuumuka na hii kufura inatumika sana Zanzibar

Sasa ngoja nikaandae chai maana maandazi ya bure yapo, hongera sana kwa kutupikia maandazi humu ndani

nukta77 said...

Tafadhali mhudumu nipatie soda baridi sana ya Fanta unisogezee na kigoda...

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

najiuliza kama kiafya ni sawa kula maandazi, eti yanaongeza virutubisho gani mwilini?

Yasinta Ngonyani said...

kaka Bennet hiyo chai bado tu nasubiri nilifikiri utanikaribisha.

Da subi karibu hii soda yako baridi na kigoda ndo hicho furahia mlo.

Kamala unataka kuniambia kila ulacho unakula kwa kuwa unajua kina urubitisho gani mwilini?

chib said...

Maelezo yametulia, sasa huo muda wa kuandaa, usubiri yafure, tena uyapige pasi na kuyapiga panga, yafure tena, du.
Kwa kweli umenitia hamu ya kula maandazi, itabidi niingie mitaani hapa Kigali nikaukokote huo unga wa ngano

EDWIN NDAKI said...

asante sana kwa soma zuri la leo..ngoja nikapige practical kisha nikuletee majibu kama zoezi nimefaulu

PASSION4FASHION.TZ said...

Sasa Yasinta kama sio uchokozi ni nini? umenifanya nipate hamu ya kula hayo maandazi utazani ndio umeniwekea hapa mezani kwangu....maelekezo yametulia hata kwa mtu hajui kupika,akifuata hayo maelekezo adanzi litatoka bomba.Asante sana kwa mandazi tips.

SIMON KITURURU said...

Mi udenda tu unanitoka!:-(

kiluvyapub said...

Duh. umenitamanisha sijala maandazi siku nyingi. Ningekuwepo Nanihii ningeagiza sasa hivi

Yasinta Ngonyani said...

Chib! ukitaka chakula kiwe kitamu basi ni kuchukua muda wote unaotakiwa na subira ni muhimu kwa kila kiti. Haya tafuta huo unga usisahau kunikaribisha.

Kaka Edo nasubiri jibu la hili zoezi najua utaweza tu ukishindwa basi ntakuja kukufundisha:-)

Dadangu hapa nilijua tu utasema hivyo karibu Ruhuwiko.

Simon:-(

Kiluvyapub, agiza tu ala sema uko wapi kuna kutuma chakula hapa. kazi kwelikweli

Born 2 Suffer said...

Sis. yani hapo unapata chai ya rangi imehemshwa vizuri na mchaichai halibaki hata ndazi moja katika sinia, Tunakula tuishi au tunasihi tule? hapo sasa.

Anonymous said...

ahsante kwa somo zuri ntaenda kufanya maanake mm mandazi hunishinda kupika bora chapati

Degelavita said...

Ngoja sasa nikaweke jamvi langu chini, nianze kupanga vitu mbavuni. Kabla hata sijaonja yanonekana mattammuuuu