Sunday, May 3, 2009

UBAGUZI WA RANGI TANZANIA/AFRIKA

Baada ya kusoma mada ya Prof. http://matondo.blogspot.com/aliandika kuhusu Ubaguzi wa rangi Tanzania (inasikitisha sana) nimepata wazo la kuandika kitu hiki
Napatwa na uchungu nionapo/sikiapo sisi waafsika tunavyowaheshimu wenzetu wazungu. Tunavyowanyenyekea na kuwaona ni watu wa maana kuliko sisi wenyewe. Nimewahi kusikia watu wakisema una bahati kuwa pamoja/kuolewa au kuoa mzungu. Yaani wanaona Fahari sana kuwa karibu na mtu mweupe.

Bado sijajua kwanini isiwe bahati kuolewa/kuoa mwafrika kwanini tusijionee fahari rangi yetu. Na kuna wanaofikiri mtu "mweupe" mzungu ni tajiri sana na wana kila kitu. Kwa uzoefu wangu kwa jinsi nilivyoishi hapa nilipo HAPANA. Wao ni watu kama sisi isipokuwa ni rangi tu. Kitu kingine ni kwamba maisha ya hawa wenzetu ni standard nyingine vitu, chakula nk. ni ghali sana. Basi wafikapa Afrika hata kama wana pesa kidogo wanaonekana wana hela nyingi kwasababu vitu na chakula ni bei rahisi kuliko watokako.
Nawaambieni si fahari kuwa /kuolewa au kuoa mzungu. Ukiwa Afrika na hasa mkiwa madukani na sokoni tunauziwa vitu kwa bei kubwa sana kisa nipo na mzungu. Kazi kwelikweli! Hawawezi kufikiri mzungu ni mtu tu wa kawaida.

Siku moja tulikwenda kununua kitanda mimi na mume wangu. Tulipouliza bei wakatuambia ni shilingi laki moja . Siku hiyohiyo baada ya dakika tano hivi tukamtuma kakangu aende kuuliza bei palepale tulipouliza sisi yeye akaambiwa ni shilingi 60,000/=. Kwa kweli ilibidi tucheke, baada ya muda tukaenda na kununua kwa bei hii ya mwisho, alipotuona kuwa ni sisi "wazungu" tena aliona aibu sana .

Nikawa nawaza na kushangaa ni kweli hapa Tanzania yangu au? Kwa kweli inachekesha sana na pia inasikitisha sana kuona Tanzania yetu ipo hivi.

10 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Ndio nchi yetu hiyo. Badala ya kuwaheshimu na kuwapenda, tunawanyenyekea na kuwaona kama TAFSIRI HALISI YA PESA. Kwamba kila mwenye ngozi hiyo ni lazima awe nazo na pia hajui lolote kuhusu bajeti. Pengine ni kwa sababu wenzetu huthamini sana muda na ujuzi ambao mtu hutumia kutengeneza kitu, lakini pia, tunazidisha "kuwagonga" bei.
Siri nyingine Dadangu. Usiende kununua vinyago na mumeo. Tena jitahidi hata kutoambatana na kina Camilla, na pia usionekane kama anayeweza kuwa ameshavuka hata mpaka wa Namanga. Ukienda "ki-mtoko mtoko" Utanunua kinyago kimoja kwa bei ya vitatu.
Si huwa unajiandaaa kwenda kanisani na shereheni na kwingine? Basi ujiandae kwenda kufanya shopping ya vitu hivi ambavyo bei yake hupangwa na mwenye navyo kwa kipimo cha kumtazama mteja. Jivalishe kichovu kisha nunua hivyo vitu (kwa bei halali) then rejea nyumbani ubadili na kuendelea na ratia zako za mavazi kama kawaida. La sivyo, utalia kilio cha mbwa MDOMO JUU.
Pole saaana

Mzee wa Taratibu said...

Hii si Tanzania tu wanaowaheshimu hawa bali nchi zote duniani hata sisi hapa Oman, Kitu kinawasaidia ni rangi tu yao ukitazama katika uchafu wao ni wachafu mno kwa kila ktiu, mungu kawajaalia akili tu na wameweza kuteka dunia toka ezni hizo, lakini si watu wa maana ukitazama.

Fadhy Mtanga said...

Ubaguzi?
Mi sijui nisemeje? Nimejifunza mambo mengi. Lakini baya nililojifunza ni kuwa pengine hakuna wabaguzi kama sisi wenyewe ngozi nyeusi. Sisi weusi tunashabikia sana vita dhidi ya apartheid lakini kiukweli sisi ni wabaguzi mwisho. Siku moja nilikuwa naendesha njia ambayo trafiki walikuwa wakikagua magari. Niliposimama, nyuma yangu akasimama waiti mani. Akaruhusiwa, ila mimi kila kitu kilikaguliwa.
Si hivyo tu, hata maofisini, wenye ngozi nyeupe wanatukuzwa vibaya mno. Makanisani nako ndo usiseme.
Na hawatukuzwi na weupe wenzao, bali sisi blaki kala.
Huwa najiuliza mara lukuki, nani mbaguzi hasa?
Nadhani sisi nasi twajibagua. Tupo radhi kumtukuza, kumnyenyekea, (nikisema hata kumsujudu nadhani sikosei) mtu mweupe. Ingawa kuna weusi kibao wenye akili kupindukia, wenye karama kubwa ya uongozi kuliko hao weupe.
Walitukuzwa Net Group Solution, lakini hasara waliyoitengenezea Tanesco ni kubwa kuliko inapoongozwa na mweusi. Tuliwatukuza.
Lililonichefua ni Mramba akiwa waziri wa Miundombinu aliondoa neno Mwalimu katika jina la uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar. Kisa, eti wazungu wanapata taabu kulitamka.
Hata lugha ya kwao twaitukuza na kuidharau yetu.
Nachelea kusema, twajibagua wenyewe, kama sivyo, basi twautukuza ubaguzi.
Nimesema sana.
Ni hayo tu!

Mwanasosholojia said...

Da Yasinta, kwanza pole kwa hako kamkasa ka kitanda!Yaani ni kama vile uliponzwa na kuongozana na "mwenye nazo" kama wanavyosema wabongo walio wengi wenye mtazamo potofu kwa wazungu. Hata huku nayashuhudia mengi, wenzetu (wazungu) wana maisha ya kujibana sana (careful spending/ spend little), ingawa najua wana- accumulate much. Hii ndo rationality yao economically. Si ajabu kumuona mzungu profesa anaendesha baskeli! Kwetu bongo profesa wa kibongo aendeshe baiskeli!weeeeee....weeeee, sasa ataonekanaje kuwa na yeye ni profesa? Ninachofahamu mimi ni kuwa, wabongo wengi tuna kasumba, tunafikiri (kama ulivyosema) wenzetu wazungu ni watumiaji sana kwa kuwa ni matajiri, in turn tunaiga pasipo kufanya uchunguzi wa kina...magari mazuri- mengine kwa njia za kifisadi (wakati wengine wanatembelea TZ 11 vijijini. Sijui tunakwenda wapi?!!

Koero Mkundi said...

Kuna Rafiki yangu anaomba na kukesha ili aolewe na mzungu, kisa anataka kuishi ughaibuni, anadai maisha ya bongo ni michosho na yanakera, na hata wanaume wa kibongo hawana upendo kama wazungu.

Rafiki yangu huyo ambaye ni graduate anazidi kusisitiza kuwa wazungu huwapika wake zao' huwafulia na hata kwenda sokoni kununua mahitaji ikiwa ni pamoja na kusaidia kulea watoto, lakini wanaume wa kibongo, thubutuuuuu...... hawana msaada wowote kazi yao kuagiza tu, "fanya hiki.....leta hiki......ilimradi amri mtindo mmoja...

Nimehitahidi kumuelimisha weeee, hanielewi kabisa,, imebidi nimuache lakini kwa makala hii ya dada Yasinta pamoja na maoni ya wadau wenzangu nampelekea labda atabadili mtazamo wake

Fadhy Mtanga said...

Da Koero umenikumbusha kitu. Nami namfahamu mtu anayekesha kuomba kuolewa na mzungu. Ndo maana nafikia kuamini sisi nasi twajibagua.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

siamini katika ubaguzi na kubaguliwa, naamini ktika kujibagua kwanza na kutaka kuonewa huruma ndio ubaguzi wenyewe

NURU THE LIGHT said...

ndio maana nakupenda dada yangu maana unaongelea mambo ambayo yako very true na relevant..sasa sio wazungu tu hata mimi mtazanzania mwenzao wakiona tu nimtoka njee wananipig bei..kuna cku nilikuwa nataka taxi kutoka pale sters mpaka millenium towers ambapo si mbali kiihivyo na taxi pale nnje kuniona mimi tu basi kila mtu akataka elfu sita..yaani nilikasirika nakuwatukana kuwaambia mnanisikitisha na kukata moyo sanaa..hadi mimi mtanzania mwenzenu mnataka nigonga yaani its a big problem..watu wetu wanahitaji kubadilisha mentality yao na kuelimishwa zaidi kuhusu maisha ya ulaya..wakati naenda kushoot my video kigamboni tulienda beach inaitwa mikadi n that beach wameigawa kwamba kuna side inaitwa white beach na nyingine for other ppl..kule white wameweka bei ya juu ili watu watanzania halisi wasiwe wengi yaani hiii kitu ilinisikitisha sanaaaaa..ahsante dada

ERNEST B. MAKULILO said...

MAUAJI YA ZERUZERU (ALBINO) TANZANIA NAYO NI UBAGUZI WA RANGI

Nimekaa na kufanya tafakari ya kina kuhusiana na mauaji ya ndugu zetu Albino yanayoendelea kuisakama Tanzania. Dhana mbili zinajitokeza katika tafakari hiyo. Moja ni dhana nzima ya ubaguzi wa rangi na pili ni tathimini yangu kuhusu mikakati ya serikali ya Tanzania kuwahakikishia usalama ndugu zetu Albino.

Ukiangalia ubaguzi wa rangi uliokuwepo Afrika Kusini enzi za Makaburu, watu walipangwa katika makundi kutokana na rangi zao; weupe ( Wazungu ), watu wa rangirangi (coloured ) na weusi ( Waafrika ). Huduma zote, ikiwa ni pamoja na elimu, zilitolewa kwa kuzingatia rangi ya mtu.

Kulikuwa na kumbi za starehe kwa ajili ya watu weupe, ambapo mtu mweusi hakuruhusiwa kuingia. Kuna sehemu zingine ambazo mwafrika hakuruhusiwa hata kukanyaga kabisa. Akikamatwa, alipewa kipigo kikali na hata kutupwa lupango ( jela).

Ubaguzi wa rangi, hususani dhidi ya Mwafrika, ulikuwepo hata katika nchi za Magharibi. Nakumbuka nimeona picha zilizoandika “only for blacks and dogs here.” Hii ilikuwa hatari sana, kwani mtu mweusi alinyimwa haki zake kutokana na rangi ya ngozi yake .

Sasa tujiulize.Hivi Albinno ni mtu wa namna gani? Anaweza tambuliwaje kwa muonekano wake? Sintopenda kuingia ndani zaidi kuchimba sababu za kibaiolojia zinazo mfanya mtu azaliwe Albino. Hata hivyo mtu haitaji microscope ( darubini) wala elimu ya Chuo kikuu kumtambua Albino.

Nionavyo mimi, naamini bila pingamizi lolote kuwa mauaji ya Albino yanayoendelea kuitikisa Tanzania “Kisiwa cha Amani” ni mwendelezo wa dhambi ya ubaguzi wa rangi, lakini huu ni ubaguzi mkali zaidi katika historia ya mwanadamu kushinda hata dhambi ya biashara ya utumwa.

Nasema nimkali zaidi kwani unalenga kuondoa maisha ya mwanadamu kwa ukatili wa kunyofoa viungo, tofauti na ule wa kumzuia mweusi kutembelea mitaa fulani au katika upandaji wa mabasi n.k !

Ni kwa kuangalia rangi ya ngozi yake, unaweza kumtambua Albino. Kwa bahati mbaya, Albino anayezaliwa Afrika, ni tofauti na yule wa nchi za Ulaya na Marekani, kwani Albino wa nchi hizo, hatofautiani sana na mtu wa kawaida. Rangi yake inarandana na ya mzungu . Si ajabu kama naye angefanana na mwafrika, angebaguliwa na kuuawa.

Kinachonishangaza mimi, ni kwanini Tanzania au Watanzania kwa ujumla hatusemi ukweli kuwa mauaji ya Albino yanayoendelea, ni ubaguzi wa rangi ili tuweze kupambana nao ipasavyo na Jumuiya ya Kimataifa iweze kutoa msaada sawawa na ambavyo jumuiya ya Kimataifa, hususani Tanzania, ilivyojitoa muhanga kung’oa mzizi wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini?

Kwa mtazamo wangu, Watanzania tumeaminishwa kuwa Tanzania ni kisiwa cha Amani na hivyo sisi ni bora zaidi kuliko Taifa lolote kiutamaduni na kimaadili. Hii si kweli na huu ni mtazamo potofu ambao tusipokuwa makini, utatufikisha pabaya.

Kwa uzoefu wangu, kitendo cha ubaguzi kikifanywa na Taifa jingine mfano Burundi, Kongo, Afrika Kusini, Ujerumani, M arekani ama Israeli, tunawanyooshea kidole kuwa wamepotoka huku tukitamka wazi kuwa nchi hizo zinafanya ubagauzi wa rangi. Je, kwa nini kitendo hicho kikitendeka Tanzania kama cha mauaji ya Albino, tunapata kigugumizi kutamka wazi kwamba ni kitendo cha ubaguzi wa rangi na tunaanza kutafuta majina mengine kama vile “unyanyasaji wa Albino” na k.n yasiyotoa picha halisi ya mambo yanayoendelea?

Kwani ubaguzi wa rangi lazima kitendo kifanywe na mtu mweupe ( mzungu ) dhidi ya mweusi ( mwafrika ) ili kistahili kuitwa ubaguzi wa rangi? Vipi kama kitendo hichohicho kitafanywa na mtu mweusi dhidi ya mtu mweupe ( mzungu / albino ), hakiwezi kuitwa kitendo cha ubaguzi wa rangi?

Au kama mtu mweusi atafanya kitendo cha kumbagua mweusi mwenzake kutokana na rangi yake kama vile mweusi sana , mweusi tiii! mweusi wa kati, nacho hakiwezi kuitwa ubaguzi wa rangi? Na vipi kama mtu mweupe ( mzungu ) akimbagua na kumnyanyasa mweupe mwingine kama vile Mchina , Mwarabu n.k, kitendo hicho kitaitwaje?

Kwa uzoefu wangu, hasa baada ya kuangalia matukio ya hivi karibuni ambapo Waafrika Kusini waliamua kuwavamia na kuwaua wahamiaji kutoka nchi nyingine za Afrika, Tanzania ilikuwa mstasri wa mbele kukemea vitendo hivyo. Tanzania ilitoa tamko kali na kwa uwazi kabisa ikisema, “ Dhambi ya ubaguzi bado inaitafuna Afrika kusini.”

Nikaanza kuangalia mambo mengine ninayoyashuhudia kila kukicha huku Marekani. Mtu akifanyiwa kitendo fulani, kwa mfano, ikiwa ni mweupe kakifanya, hukimbilia kusema ni ubaguzi wa rangi.

Sasa mimi najiuliza. Je endapo Mtanzania mweusi mmoja ataenda nchi yoyote ya Magharibi kama vile kusoma au kufanya kazi halafu akauliwa na kunyofolewa viungo kama wanavyofanyiwa Albino, Tanzania itasemaje? Haina ubishi , kila mtu atasema “amebaguliwa na kuuwawa kutokana na rangi yake.”

Swali langu la msingi ni hili: Kitendo cha Albino kunyofolewa viungo vyake kinyama na hatimaye kuuawa na mtu mwenye rangi nyeusi kisa rangi yake ni tofauti na cha mtanzania mweusi aliyebaguliwa na kuuawa ugenini hususani katika nchi za magharibi? Kwa nini mauwaji ya Albino yasitajwe kama ubaguzi wa rangi? Maana Albino naye hutambuliwa kwa rangi yake!

Kama tumefikia hatua ya kuuana kutokana na rangi zetu; moja nyeusi, nyingine ya rangirangi ( coloured ) na wote ni binadamu tena watanzania, tuanaelekea wapi ndungu zangu?

Serikali ya Tanzaia inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kupambana na janga hili la mauaji ya albino. Uamuzi wa kugawa simu kwa albino wote, pengine waweza kusaidia kwa kuwawezesha kupiga simu polisi wanapovamiwa.

Lakini Serikali inawasaidiaje albino waishio kijijini ambako hakuna umeme? Simu hiyo inachajiwa kwa teknolojia gani? Je simu hizo hizitakuwa kivutio kingine na hivyo kuwafanya wavamiwe zaidi?


Kama imefikia hatua albino hawezi kutembea peke yake au kutembea baadhi ya masaa hususani jioni, kama imefikia hatua Mbunge maalum ambaye ni albino lazima apewe ulinzi maalum ili asinyofolewe viungo vyake, falsafa ya Tanzania kama kisiwa cha amani iko wapi?

Ndugu zetu wa Marekani wanaelekea kuishinda dhambi ya ubaguzi wa rangi, kwani hatimaye wamefikia hatua ya kumchagua mtu mweusi kuwa Rais wao kwa kuangalia uwezo wake, hoja zake na si tena kigezo cha rangi kama Dr. Martin Luther King Jr aliposisitiza katika ndoto yake ( I HAVE A DREAM). Mwaka 2010 kama mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa albino, tutakuwa tayari kumpigia kura endapo atakuwa na sifa za kutuongoza? Tafakari, Chukua hatua.

Nawasilisha hoja!

MAKULILO Jr

www.makulilo.blogspot.com

West Virginia, US

Anonymous said...

Nimetumiwa hii kwenye mail na nimeona ni vema niweke hapa ili wote tufaidike.

Nafurahi sana kila siku kusoma blog yako? Ipo very interesting kwa sababu inaangalia maisha katika sehemu na mitindo mbalimbali.

Anyway, unatoa very interest topics na mara nyingine nafikiri kuweka comments lakini sioni sehemu ya comments.

Mfano suala la watanzania kupenda wazungu kuliko wenyewe. Hili ni swala ambalo kwa kweli linauzi sana. Mimi mwaka 1994 nilikwenda YMCA Dar na mzungu mmoja nilikuwa treated very well tukiwa pamoja na mzungu huyo hawakuniuliza cha ID wala nini. Hali ilikuwa shwari kabisa. Baadaye mzungu yule aliondoka na mimi kurudi na kutaka kukaa ile sehemu pekee yangu niliambiwa kwamba hakuna vyumba. Cha kuuzi zaidi kuna Mswede mmoja akaja pale hakuwa na order ya chumba wala chochote yule akapewa chumba. Kweli hii ni aibu sana tena kwa YMCA ambayo lengo lake na original mission siyo necessary kwamba kutengeneza hela.

Hata Obama ukisoma kitabu chake cha dreams of my father sehemu ambayo alikuwa anatembelea Kenye kwenye hotel moja akiwa na dada yake wa shangazi yake walikwenda sehemu moja ndani ya hoteli hiyo Obama na shangazi yake walikaa na kusubiri kwa muda bila kupewa huduma yeyote ile. Wazungu ambao actually happened to American wamekaa pale jirani pamoja na kuja kwa kuchelewa bado walipewa huduma kabla ya akina Obama na shangazi yake. Ndani kwa pembeni Obama alisikia wakiteta kwamba hawana haja ya kuhudumia waswahili (black). Hii ni shame ya hali ya juu sana.

Kwa asilimia kubwa hii ni economics. Kila mtu anapiga hesabu kwamba pengine naweza nikabahatisha mzungu akanichukua au akaniachia tip kubwa. Kwa maana hii ina maana sisi watu weusi tutaendelea kuwa chini sijui hadi lini. Dunia inabadilika uchumi hata wa India sasa ni mzuri miaka 10-20 India itakuwa imesukuma na kutoa maskini wake na ombaomba wote lakini sisi tutabaki.

Lakini suala jingine ni suala la sisi ambalo linakwenda ndani sielewi historia yake nini? Lakini unakuta kwamba mtu ambaye ni mweupe au maji ya kunde generally speaking anapendwa zaidi kuliko wengine sina uhakika to what extend hii inakwenda watu kupenda na kunyenyekia wazungu. Sidhani kama hii ni asimilia kubwa kuliko tuu kwamba Economics na financial strength ya wazungu ndiyo inayofanya hivyo.

Nimefundisha Tanzania na wazungu na walimu waswahili kila mwalimu (majority to fair siyo wote) at least katika shule hii ya sekondari unaona alikua anatumia kila kupata nafasi na chance ya kuomba chance ya kwenda nje. Mzungu kwa hilo tuu alionekana ni mfalme.

Anyway, mimi mshamba inabidi niende shambani tutaendelea kujadili. Sisi wahehe (mimi mkinga lakini sijakaa makete hivyo ni mhehe) kwa kihehe tunasema vahungilage.

Mawazo haya yameruka kule na kule nimeandika na kuacha na kuanza tena samahani kama nimevunja utaratibu wa kuandika.

Evaristo