Wednesday, July 30, 2014

WANAWAKE 280 PERAMIHO/LUNDUSI WAJITOKEZA KUPIMA KWA HIARI!!!

 

Baada ya kusoma habari hii sikuweza kuacha kuisambaza LUNDUSI ni nyumbani  mnajua. Mtu kwao ni furaha kuona wanawake wanajitokeza kwa hiari kwa zoezi hili. Habari yenyewe ndiyo hii hapa chini, karibuni
--------------------------------------------------------------------------------------------------------------
 
WANAWAKE 280 katika kijiji cha Lundusi kata ya Peramiho wilayani Songea mkoani Ruvuma wanahitaji huduma ya kupimwa kwa hiari virusi vya ukimwi ili kutambua afya zao.
Wanawake hao wametoa ombi la kutaka kupimwa virusi vya UKIMWI kwa hiari baada ya kupata elimu ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yaliyoendeshwa na shirika la maendeleo ya wanawake Ruvuma RUWODA.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa wiki moja katika vitongoji vya Ringa,Lundusi,Dodoma na Kiburungi vilivyopo katika kijiji cha Lundusi chenye wakazi zaidi ya 2500 ambapo wananchi hao wameweza kujifunza mada mbalimbali zilizotolewa na Radbord Ngonyani ambaye ni mratibu wa shirika la RUWODA.
Kulingana na mratibu huyo wa RUWODA, mada ambazo zimefundishwa katika mafunzo hayo ambayo yalishirikisha jumla ya watu 350 ni pamoja kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto(PMTCI),ongezeko la vituo vya huduma na wajibu wa jamii katika kuzuia maambukizi.
Mada nyingine ni lishe kwa mtoto aliyeambukizwa virusi vya UKIMWI toka kwa mama kwenda mtoto,,uwezekano wa mama mjamzito wa kumwambukiza mtoto,namna ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na uwezo wa mama mjamzito kuzuia maambukizi kwenda kwa mtoto.
Ngonyani amezitaja mada nyingine ambazo zimefundishwa kuwa ni athari za kuishi na virusi vya UKIMWI,mahitaji ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI,wajibu wa jamii katika kuzuia virusi vya UKIMWI na UKIMWI,uaminifu katika mahusiano ya mapenzi na mkakati wa kuhamasisha umuhimu elimu na faida ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mratibu huyo wa RUWODA amefurahishwa na wanawake wa kijiji cha Lundusi kuamua kwa hiari kutaka kupimwa virusi vya UKIMWI ambapo ameahidi kuwasiliana na mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea ili kutoa wataalamu wa upimaji waweze kwenda katika kijiji hicho kuwapima wanawake wanaotaka kupima kwa hiari.
“Wananchi waliojitokeza kutaka kupimwa kwa hiari watasaidia serikali kupata takwimu sahihi za maambukizi ya virusi vya UKIMWI na namna ya kuwasaidia watakaobainika kuathirika,tatizo la ,maambukizi ya virusi vya UKIMWI bado kubwa katika wilaya ya Songea’’,alisema.
Sera ya afya Tanzania ya mwaka 2007 inatamka wazi Serikali inafanya juhudi kubwa kukabiliana na janga la UKIMWI. Hata hivyo, kutokuwepo mwitikio sahihi wa kukabiliana na janga la UKIMWI miongoni mwa wananchi, kunaendelea kuathiri juhudi za kukabiliana na janga hili.
Kulingana na sera hiyo, hali hiyo, inaendelea kuathiri nguvu kazi, kuongeza vifo, yatima, umaskini na gharama za matibabu pamoja na kuathiri ustawi, uchumi na usalama wa taifa.
Kudhibiti maambukizi na ya Virusi vya UKIMWI nchini na kutoa matunzo na tiba ya kupunguza makali ya UKIMWI.Serikali itaendelea kushirikiana na wadau katika kukabiliana na janga la UKIMWI katika nyanja zote zikiwemo, kinga, huduma za tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya na majumbani, ili kupunguza athari zinazosababishwa na VVU/UKIMWI.
Kulingana na takwimu za UKIMWI kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Mkoa wa Njombe, Mbeya Iringa na Ruvuma ni vinara wanaoongoza kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi nchini.

Njombe inaongoza kwa asilimia 14.8 ikifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya tatu kwa asilimia 9.
Mikoa mingine na asilimia za maambukizi katika mabano ni Ruvuma (7.2), Shinyanga (7.4), Dar es Salaam (6.9) Rukwa (6.2), Katavi (5.9), Pwani (5.9),Tabora (5.1), Kagera (4.8) na Geita (4.7).
Kwa mujibu wa takwimu hizo mkoa wa Mara (4.5), Mwanza (4.2), Mtwara (4.1), Kilimanjaro (3.8), Kigoma (3.4), Simiyu (3.6), Morogoro (3.8), Singida (3.3), Dodoma (2.9), Manyara (1.5), Lindi (2.9), Tanga (2.4), Unguja (1.9) na Pemba (0.3).
Takwimu hizo zinatokana na utafiti uliofanyika mwaka juzi hadi mwaka jana. Hata hivyo kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzani maambukizi ya Ukimwi yanapungua kwa kasi ndogo.

Hata hivyo shirika la Afya Ulimwenguni WHO limetoa takwimu zinazoonyesha kuwa maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 50 katika nchi 13 za kusini mwa jangwa la sahara ikiwemo Tanzania.
Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 1999 inakadiriwa kuwa watu wazima na watoto milioni 33.6 walikuwa wanaishi na virusi vya UKIMWI na watu milioni 16.3 walikuwa tayari wamefariki dunia katika nchi zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara.
Pamoja na takwimu za shirika la afya duniani kutoa matumaini makubwa kwa nchi za kusini mwa jangwa la sahara bado nchi za Afrika mashariki zinawajibika kuongeza jitihada za kukabiliana na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI hasa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja kutoa huduma kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.

2 comments:

ray njau said...

Hi ni jambo jema kijamii.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Ray ni kweli kabisa. Na inapendeza na kufurahishs wengi wanajitokeza na kufanya zoezi hili.