Wednesday, October 16, 2013

KAMA MVI NI KIPIMO CHA BUSARA, NI KWA NINI ZIFICHWE??


Mbona Profesa Mbele anazo mvi lakini hazifichi?

Habari zenu wasomaji/wandugu na wengine wote. Ni Jumatano nyingine .Basi mwenzenu nimeamka nikiwa na wazo hili la MVI au niseme nimeota nina mvi kichwa chote. Ndo nikakumbuka kuwa mwaka juzi niliandika makala na nimeona niiweke tena hapa. Kwani mimi naamini mtu unaporudia kusoma aidha kitabu au habari fulani ndipo unapozidi kujifunza haya karibu sana......
Mvi ni dalili ya uzee au ni kitu gani? Kwa zamani ingekuwa ni muhali mkubwa mtu kuuliza swali la aina hii, kwa sababu mvi zinahesabiwa kama dalili ya busara, bila shaka zikihusianishwa na kuona mengi ambayo ni wenye umri mkubwa tu waliokuwa na nafasi hiyo.
Lakini leo, mvi ni kisirani na karibu kila mtu anajaribu kuzikimbia, kwani kuendalea kuwa kijana ni sifa kubwa. Kwa sasa uzee unanuka na kila mmoja anajaribu kuukimbia kwa njia mbalimbali ikiwemo ya kukana umri na kujirudisha nyuma kimatendo. Kwa kifupi hii ndiyo historia ya mvi, usiziogope bure!
Karibu rangi zote asilia za nywele zinatoka kwenye kitu kiitwacho melanin, ambacho huzalishwa na mwili kutokana na seli zinazofahamika kama melenocytes. Nywele zinapobadilika na kuwa nyeupe ina maana kwamba, melenocytes haizalishi tena melanin. Mabadiliko haya ya nywele kutoka rangi nyeusi na kukosa rangi (mvi) siyo hatua ya siku moja bali mwaka na miaka, kwani nywele moja hubadilika baada ya muda mrefu na nyingine na nyingine. Siyo hatua ya siku moja tu.
Kwa kadiri mtu anavyozeeka ndivyo ambavyo uwezo wa mwili kuzalisha melanin unavyopungua. Uwezo huu huanza kupungua mtu anapofikia umri wa miaka 35 au 40. Lakini watu wengine huanza kuota mvi wakiwa na umri wa miaka hata 20 tu. Je, hii nayo inatokana na nini?
Hili kusema kwali siyo jambo la ajabu. Ingawa kuna watu ambao huwa wanalishangaa. hata hivyo wana sayansi wanasema kwamba hawajaweza hasa kujua ni kwa sababu zipi uwezo wa mwili kuzalisha melanin huwa unashuka. Lakini wana uhakika kwamba wale wanaoanza kuota mvi kabla hawajafikisha umri wa miaka 35, kwa sehemu kubwa wanaathiriwa na urithi au kizalia.
Kama mtu ataona kwamba anaanza kupata mvi mapema sana ni dhahiri kwamba akiangalia kwenye familia yao atakuta kuna mtu ambaye naye alianza mapema kuwa na mvi. Hii itasaidia kumuonyesha kwamba mvi zake ni matokeo ya kizalia.
Pengine ni jambo la ajabu kwamba kuvuta sigara kunatajwa kama sababu ya kuchochea mtu kupata mvi akiwa na umri mdogo. Ukiwachunguza wavuta wazuri, utagundua kwamba wameanza kuota mvi mapema kuliko umri wa miaka 35 au 40.
Matatizo kwenye kiungo kinachodhibiti ukuaji mwilini, yaani thyroid huweza pia kusababisha mtu kupata mvi kabla ya kufikisha umri wa miaka 35. Pia ukosefu wa vitamin B12 unatajwa kwa sababu nyingine.
Kuna watu ambao hata kama wana umri wa miaka 60 bado hawataki kuona nywele nyeupe vichwani mwao . Watu hawa huangaika huku na kule kutafuta dawa kuondoa mvi na pengine kutumia rangi ya nywele ili kufanya rangi ya nywele nyeupe zisionekane. Huu ni kama mwendawazimu kwa kiasi fulani. Kwanini?
Kwanza kuna ukweli kwamba nyingi kati ya hizo zinazodaiwa kuwa rangi za kuondoa mvi, zina athari katika mwili wa mtumiaji. Lakini wendewazimu mkubwa zaidi ni kitendo chao cha kukataa ukweli ambao inabidi waujivunie.
Mvi bado ni dalili ya busara. Kama umefikia umri wa kuota mvi na hujafanya jambo lolote la maana na hujatoa mchango wowote wa maana kwa familia yako au jamii unamoishi ni lazima utaficha mvi zako. Kwanini?Kwa sababu utaona haya sana kuonekana kwamba umri wako ni mkubwa lakini hujafanya lolote. Tunaposema mchango wa maana hatuna maana ya fedha au mali, bali zaidi tuna maana ya mawazo ya kujenga na pengine kuandaa misingi ya kujenga kwa nia ya kuleta maendeleo baadaye.
Hebu chunguza kwa makini, utagundua kwamba watu wote wanaojaribu kuficha mvi ni wale watu ambao wametawaliwa sana na vionjo na tamaa ya miili yao kuliko maendeleo ya binadamu. Ni wale watu ambao hata kama wana fedha, hawajajua hasa wako hapa duniani kwa sababu gani. Hivi ndivyo ilivyo kwa sababu watu wa aina hii huhofia sana umri, huhofia sana kufa kwa sababu hawajakamilisha walichokuja kukifanya duniani kwasababu hawajajua bado.
Kukosa kujiamini na kujikubali kwamba wewe ni fulani na uko katika hali fulani na kiwango fulani hupelekea watu wengi kubadili majina, kuchukua makabila yasiyo yao, kujiita maarufu au kuongopa kuhusu maisha yao kwa ujumla. Mtu anayejaribu kuficha mvi ili asijulikane kwamba ana umri mkubwa hana tofauti na watu hawa.
Mtu ambaye anajiamini hawezi kuogopa kutaja umri wala kuonyesha kwamba ana umri mkubwa. Na mtu hawezi kujiamini kama hajijui yeye ni nani na kujijua kunataka mtu asiishi kwa kutazama wengine watamuonaje, bali anajionaje.
Kuficha mvi inaweza kuwa ni dalili ya mtu kuvuka kipindi fulani bila kufanya mambo ambayo kisaikolojia alitakiwa kuyafanya wakati huo. Kama mtu alitakiwa kufanya mambo hayo katika umri wa miaka 20 hadi 25 na hakufanya, kuna kawaida ya mtu kama huyo kuja kutaka kuyafanya akiwa na umri wa juu zaidi.
Kwa kuwa wakati huu mvi ni dalili kwamba ameshapita umri wa kufanya mambo hayo, atahakikisha kwamba dalili hii inafunikwa au kufutwa ili isimfedheheshe. Wengi wetu tunawajua wa waficha mvi na vituko vyao huko mitaani kwetu. Habari hii chanzo ni Jitambue.......Ukitaka kusoma maoni ya mwaka juzi bazi unaweza kuingia KAPULYA. NAWATAKIENI JUMATANO YENYE AMANI NA UPENDO PANAPO MAJALIWA TUTAONANA TENA.....KAPULYA

4 comments:

Anonymous said...

ni kweli kabisa watu wengi hawapendi mvi jamani! hata kina baba huweka nywele dawa ziwe nyeusi eti wanaogopa kuonekana na mvi! inashangaza sana. Ila pia kwa miaka hii kina dada wengi huota mvi mapema mno miaka ya 20 na kuendelea kisa ni madawa ya nywele haya marelaxer yanasababisha mvi kuota haraka mno! madhara nay kemikali kwenye mwili ni makubwa. Weengi huweka dawa ili kuzificha, ila wana mvi nyingi tu. Tuwe makini na tunayoamua kufanya kama kuweka dawa nywele, ambapo kunakuja kusababisha mvi ambazo huwezi kufanya zisiote tena.

ray njau said...

Wewe umetoka katika familia gani?
Hili ni swali muhimu katika jamii kila siku.Baada ya maelezo watu hukubali au hukataa majibu ya mhusika kutokana na ufahamu wao.Ndevu na mvi ni uwakilishi wa kifamilia na iwapo mtu anaficha basi anaficha uasilia wake.

Yasinta Ngonyani said...

Mvi...sioni sababu yaficha maana kuptaa mvi ni lazima kila mtu atapata. Je utakuwa unaweksakila siku Hizo dawa? Tuache hizo tabuia nds tuache kujibadili.

emu-three said...

Kuna mabadiliko ambayo hayakwepeki, ndivyo tulivyo, ndivyo tulivyoumbwa, ukifikia umri fulani, utaota meno, ...yatakuja yatang'oka,...ikifika umri fulani, utaota ndevu, utaota matiti....na halikadhalika, ikifika umri fulani, utaota mvi..sio ugonjwa, ni hali ya kimaumbile, sasa kwann tupate shida na hayo maumbile, cha muhimu ni kuyakubali, maana hayana jinsi,..ni kama uzee, upende usipende, utafikia mahali utakuwa mzee....