Monday, October 7, 2013

TUANZA JUMATATU HII NA MDADA HUYU:- HUYU NDIYO YASINTA /KAPULYA NAMBA 2...

Leo katika pita pita nimekutana na hii.. nimependa jinsi alivyoandika na alichoandika. Na zaidi ni kwamba huwa napenda sana kumwambia mtu vitu kama hivi wakati yupo hai ..kwa hiyo nachukua nafasi hii na KUMSHUKURU SANA KAKA RAY...Kwa kumsoma zaidi kaka huyu ingia hapa

Yasinta ni mzaliwa wa Lundo -Nyasa Songea mkoani Ruvuma na hatumii soda, pafyumu, wala mafuta makali, haweki dawa nywele zake daima na rasta ndiyo chaguo lake la kudumu. Mazoezi ya kukimbia kila fursa inapojitokeza imefanya awe na muonekano wa ujana hadi wakati huu.
Ni mkarimu, mtulivu, mkali, mwenye upendo, msikivu, mdadisi na hapa nampachika jina la dada wa Maswali magumu na pasua bongo .
Ni mpenzi wa lugha ya nyumbani na ana kipaji cha kujua lugha za wengine, najua ni wachache wanamudu hilo... lakini ameweza kujifunza lugha za wanyasa wale wanaongea kama wamalawi.... kimatengo... kingoni chenyewe, kimanda, kimpoto.... Kibena… nk. Ukitaka kufikia maisha na mafanikio ni lazima uupende na kuutambua utamaduni wako na kuuheshimu ule wa wengine .
Hana majivunao na hupenda kubadilishana mawazo na watu mbali mbali, na pia anapenda kufuatilia habari za nyumbani kwake alikotoka na haoni haya kuongea lugha yake ya kingoni chenye ladha ya kimanda na kuhanikizwa na ghani ya kindendeule.
Daima anajitambulisha kwa jina la asili ya kwao na huona fahari kutumia jina hilo.
Makazi yake ya sasa ni ughaibuni katika ardhi ya waswidi na hajafunga milango kwa uzao wake kutambua na kuenzi asili ya mama yao ijapokuwa wao ni wazawa wa ughaibuni, amekuwa msitari wa mbele katika malezi ya wanae ili kuhakikisha watoto wako hawajitengi na asili ya alikotoka.
Hana uchoyo katika kutoa mashauri na kupitia makala zake anazotundika kibarazani kwake na anaendelea kutoa usaidizi kwa wengi, amekuwa mstari wa mbele katika kuilemisha jamii bila kujali rika. Anajitolea kufundisha kile akijuacho juu ya malezi na matatizo mbali mbali anayoweka Kibarazani kwake (Maisha na Mafanikio) ambacho ni kitovu chenye kukutanisha wadau mbali mbali wenye fikra pevu, na kuibua mijadala yenye kuelimisha, kufundisha, kuburudisha na kuhuzunisha pia.kabili wanandoa na malezi ya watoto.
Kamwe hafuniki hisia zake kwa blanketi na siku zote anaweka wazi hisia zake kwa mume Wave na kwa jamii yake, lakini yeye ni makini sana ili kuepuka kumuumiza mtu mwingine kihisia, na kama kwa kusema huko kutamkera mtu mwingine, ni mwepesi kuweka sawa maelezo yake ili kuondoa mgongano wa mawazo katika jamii yake.
NAWATAKIENI WOTE JUMATATU NJEMA SANA !!!


4 comments:

ray njau said...

Hii mada ya leo nimepokea kama ilivyotundikwa kibarazani nami sitakuwa mchangiaji wa awali.Ni kweli kuwa inapendeza zaidi iwapo mtu atapewa madokezo ya utendaji wake wakati akiwa hai.
===================================================== {Kwa maana walio hai wanajua kwamba watakufa; lakini wafu, hawajui lolote kamwe,wala hawana malipo tena, kwa maana kumbukumbu lao limesahauliwa. Yote ambayo mkono wako unapata kufanya, yafanye kwa nguvu zako zote,kwa maana hakuna kazi, wala utungaji wala ujuzi wala hekima katika Kaburi,mahali unapokwenda._Mhubiri 9:5,10 }

Anonymous said...

Nampenda sana Dada Yasinta. Kwa kweli sijawahi kukutana naye ana kwa ana ila mh ni zaidi ya ndugu kwangu. Ana ukarimu wa ajabu sana na pia hana majivuno. Ila napanga kuna siku moja lazima nionane nae dada Yasinta iwe Sweden au Tanzania. Ubarikiwe sana.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Ray! kwanza nakushukuru kwa utafiti wako uloufanya kuhusu mimi na kuandika... Si watu wengi wanaweza kuandika au kumwambia mtu jinsi alivyo mpaka pale akatapo roho.

Usiye na ajina ambaye lakini una jina...Ahsante sana kwa yote nami nakupenda na najua ipo siku tutaonana tu.

Penina Simon said...

Hongera, isalimie familia najua ipo ok