Wednesday, January 30, 2013

LEO TUANGALIA HADITHI: MWENDO WA KINYONGA!!!

Hapo mwanzo, yasemekana kuwa Kinyonga alikuwa na mwendo wa haraka na hata kukimbia kwa kasi kama wanyama wengine. Hakuwa na mwendo wa kusuasua kama tumwonavyo siku hizi. Je, ni kitu gani kilichomfanya Kinyonga awe hivi alivyo?
Siku moja, lilipogwa la mgambo la kuwataka wanyama wote wakusanyike pamoja ili kuwe na mashindano ya kukimbia, wapate kujua ni mnyama gani hodari wa kuchanganya miguu kushinda wengine. Taratibu zilifanyika ili kuweka mambo yote sawa. Siku ya siku ilipowadia, mashindano ya kukimbia yakaanza: Msimamizi wa mashindano alianza kuhesabu: Moja, mbili, tatu! Loo, vumbi likaanza kutimka kutokana na kishindo cha mbio za wanyama wale. Kwa vile mbio zilikuwa za kasi sana, baadhi ya wanyama walioweka vitu mfukono mwao, vikaanza kudondoka, kimoja baada ya kingine. Kinyonga kutokana na ukali wa macho yake, akaviona vitu hivyo. Kadiri mbio zilivyozidi kupamba moto, na ndivyo vitu viliendelea kudondoka. Hatimaye, Kinyonga akashindwa kujizuia. Vitu vile vilimtinga sana. Akabadili uelekeo. Akawapisha wanyama wengine na kujifanya kama vile anakwenda kujisaidia. Kumbe, anarudi nyumba na kuanza kuokota vitu vilivyodondoshwa na wanyama wenzake. Kwa kuwa vitu vile vilikuwa vingi na vilidondoka ovyo ovyo bila mapangilio wowote, Kinyonga alianza kwenda polepole, kwa maringo na makini, ili aweze kuokota vizuri vitu vyote kisiachwe hata kitu kimoja. Alifanya hivyo sio kwa ajili ya kuwarejeshea wale waliopoteza, la hasha, bali kuweka kibindoni, ili vimfae mwenyewe maishani.
"Tamaa mbele, mauti nyuma." Sasa basi, kutokana na tamaa hiyo, alikiona cha mtema kuni. Jamaa tangu siku ile, hadi leo hii, hakuweza tena kutembea haraka wala kukimbia. Akawa "amejitaiti" mwenyewe. Halafu, akawa anabadilika badilika rangi kufuatana na mazingira ya sehemu anayokuwepo ili asije akaonwa na wenye mali zao. Vile vile, anazungusha zungusha macho huku na huko kana alivyofanya siku ili "alipookota" vitu vilinyodondoshwa na wanyama wenzake.
Na Kat.V.A. Ndunguru kutoka gazeti la Mlezi.
Je hadithi hii wewe msomaji inakufundisha nini?

3 comments:

ray njau said...

Usitazame “Mambo Yaliyo Nyuma”
===============================
Lakini kwa nini mke wa Loti alitazama nyuma? Je, alitamani kuona mambo yaliyokuwa yakitukia? Je, alitazama nyuma kwa sababu alikuwa na shaka au alikosa imani? Au je, alitazama nyuma kwa sababu alitamani vitu vyote ambavyo alikuwa ameacha nyuma huko Sodoma? (Luka 17:31) Hata iwe alitazama nyuma kwa sababu gani, alipoteza uhai wake kwa sababu ya tendo lake la kutotii. Hebu fikiria jambo hili! Alikufa siku ileile pamoja na wakaaji wenye maadili mapotovu wa Sodoma na Gomora. Haishangazi kwamba Yesu alisema hivi: “Mkumbukeni mke wa Loti”!
Sisi pia tunaishi wakati ambao ni muhimu kutotazama nyuma kwa njia ya mfano. Yesu alikazia jambo hilo alipomjibu mtu fulani aliyeuliza ikiwa angerudi ili kuiaga familia yake kabla ya kuwa mwanafunzi wake. Yesu alisema hivi: “Hakuna mtu ambaye ameweka mkono wake kwenye jembe la ng’ombe na kutazama mambo yaliyo nyuma anayefaa kwa ajili ya ufalme wa Mungu.” (Luka 9:62) Je, Yesu alimjibu mtu huyo kwa ukali au bila ufikirio? Hapana, kwa sababu alijua kwamba ombi la mtu huyo lilikuwa tu kisingizio cha kuepuka daraka. Yesu alisema kwamba kuahirisha-ahirisha mambo kwa njia hiyo ni kutazama “mambo yaliyo nyuma.” Je, inategemea ikiwa mtu anayelima kwa jembe la ng’ombe anatazama mambo yaliyo nyuma kwa muda mfupi tu au ikiwa anaweka jembe hilo chini na kugeuka nyuma? Katika visa hivyo viwili, anakengeushwa kutokana na jambo analopaswa kufanya, na huenda kazi anayofanya ikaharibika.
Badala ya kukazia macho mambo yaliyopita, ni lazima tuhakikishe kwamba macho yetu yanakazia mambo ya wakati ujao. Ona jinsi jambo hilo linavyoelezwa waziwazi katika andiko la Methali 4:25: “Macho yako yatazame mbele moja kwa moja, naam, macho yako yenye kung’aa yanapaswa kutazama mbele yako moja kwa moja.”
Tuna sababu nzuri ya kutotazama mambo yaliyo nyuma. Ni sababu gani hiyo? Hizi ni “siku za mwisho.” (2 Tim. 3:1) Hivi karibuni Mungu hataharibu tu majiji mawili maovu, bali ataharibu mfumo mzima wa mambo ulimwenguni. Ni nini kitakachotusaidia kuepuka hali kama ile iliyompata mke wa Loti? Kwanza, tunahitaji kujua mambo fulani yaliyo nyuma yetu ambayo huenda tukashawishiwa kutazama. (2 Kor. 2:11) Basi acheni tuchunguze mambo hayo na kuona jinsi tunavyoweza kuepuka kuyakazia fikira.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Ray! Upo sawa kabisa..nami ngoja ...kweli tamaa ni mbaya sijui wewe na mimi "tunaokota" nini?

ray njau said...

"maisha na mafanikio"