Wednesday, January 23, 2013

Nimeshindwa vumilia !!!!

Siwezi siwezi tena, siwezi kuvumilia,
Hali miye tena sina, sinayo menizidia,
Usiku nao mchana, nazidi tu kuumia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Mejaribu kujikaza, kinywa nikakizuia,
Mezidi moyo umiza, nafuu h’ijatokea,
Moyo pendo mekoleza, mekolea kuzidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Mejaribu kutosema, moyo haujatulia,
Juu juu ninahema, kama nataka jifia,
Kwako nilishatuwama, sina ninalosikia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Usingizi siupati, wewe tu nakuwazia,
Nipo hoi hatihati, hatihati kuugua,
Nawaza kila wakati, ni vipi nitakwambia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nimechoka nimechoka, nimechoka vumilia,
Leo nakwita itika, moyo upate kutua,
Maana ushaniteka, na moyo usharidhia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nipo hoi taabani, moyo kwako umetua,
Nitakuwa furahani, wewe kinikubalia,
Nimekuweka moyoni, uniweke nawe pia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Chonde chonde muhashamu, nifanye moyo tulia,
Nikupe pendo adhimu, pekee hii dunia,
Pendo liso na awamu, kila siku lachanua,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nikupe pendo la huba, pendo nalosisimua,
Pendo tele na si haba, moyoni ‘shakujazia,
Pendo mara saba saba, mahaba yalozidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Siwezi tena kungoja, kusubiri kukwambia,
Moyoni ipo haja, zaidi nitajifia,
Nakupenda wewe mmoja, hakuna nokufikia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Uwe wangu wa milele, name niwe wako pia,
Nikupe mapenzi tele, nawe tayafurahia,
Pamoja huku na kule, kwa raha ilozidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nimeshindwa vumilia, nd’o ma’na nimekwambia,
Kwamba ninakuzimia, juu yako naugua,
Natumai mesikia, kisha tanikubalia,
Kwani siwezi himili, kutosema nakupenda.

Shairi hili kutoka kwa mtani wangu Fadhili Mtanga
NAWATAKIENI WOTE KILA LA KHERI..PAMOJA DAIMA.

4 comments:

sam mbogo said...

Shairi zuri na tamu.kaka s

Yasinta Ngonyani said...

Kaka S..yaani ni zuri na tamu kiasi kwamba,,,naishie hapa...

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Duh! hiro rimjamaa rinaropendwa rina bahati kweri kweri....

raiti ningerikuwa mimi ningerikubari mara mocha ha ha ha haaa!

utamu kunoga!!!

Aksante da Yasinta kwa kutunogesha na hilo shairi mujaarabu toka kwa Nguli baba askofu Fadhy wa Mtanga!!

emu-three said...

Mmmh thithemi mengi, kwani nitatoa uhondo.
Aliyonena ni mengi, yenye mizani na uhondo.