Tuesday, December 27, 2011

"UJUMBE ULIOVUNJA REKODI KATIKA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO MWAKA 2011

Ndugu wasomaji wa blog hii ya MAISHA NA MAFANIKIO, katika kupitia mada mbalimbali nilizowahi kuweka humu ili kupata ile ambayo ilivuta hisia za wasomaji wengi na kuleta changamoto, nimevutiwa na ujumbe huu ambao ulileta vuta ni kuvute miongoni mwa wadau wa blog hii. Kwa hiyo basi nimeichagua ujumbe huu kuwa ndio ujumbe uliovunja rekodi kwa mwaka 2011. Natoa shukrani kwa wadau wote mlioshiriki katika kuchangia ujumbe huu. Naomba muungane nami katika kujikumbusha kile kilichotokea katika ujumbe huu.


NIMEJIFUNZA KUTOKA KWA CHRISTINA
Christina akiwa amelazwa KCMC Moshi

Akiwa mjini Arusha akifanya manunuzi baada ya kuruhusiwa kutoka KCMC

Akimsimulia rafiki yaka Laila, walipokutana mjini Arusha

Huwa tunajifunza kupitia kwa wengine hususan kwa yale mambo magumu na yaliyojificha. Naomba nikiri kwamba pamoja na kusoma ushuhuda mbalimbali kupitia magazeti na blogs, lakini sikuwahi kuzipa uzito shuhuda hizo. Naomba nikiri kuwa tukio la hivi karibuni lilipompata rafiki yangu na wifi yangu Christina aishiye Dar es salaam Tanzania nimejifunza kuwa imani ikichangizwa na ibada ina nguvu sana.Christina Kaluse ni wifi yangu wa hiyari ambaye ni mke wa mwanablog mwenzangu na ambaye ni mwanautambuzi anayetuelimisha kupitia kibaraza chake cha Utambuzi na Kujitambua, huyu si mwingine bali ni mwanablog Shaban Kaluse, ukitaka kusoma habari zake waweza kubofya hapa.Nimekuwa nikiwasiliana na Christina kwa takriban miaka miwili sasa, na tangu kufahamiana na familia hii ya mwanablog mwenzangu, nimejikuta nikiwa karibu nao tukiwasiliana mara kwa mara kama ilivyo kwa baadhi ya wanablog wengine.Nisiwachoshe, niwasimulie kisa cha kuandika kile nilichojifunza kwa wifi yangu huyu Christina au mama Abraham.Nakumbuka ilikuwa ni siku ya jumatatu ya Januari 31, 2011, majira ya mchana, nilipata ujumbe mfupi kupitia simu yangu ya kiganjani kutoka kwa Christina, na ujumbe wenyewe ulisomeka hivi, ‘Yasinta naomba uungane nami kwenye maombi, nimepofuka jicho moja’ .Ujumbe huo ulinishtua sana, nikaamua kumpigia simu ambapo tuliongea kwa muda mrefu sana.Kwa kifupi aliniambia kuwa mnamo siku ya jumatano ya Januari 19, 2011, akiwa dukani kwake, (Christina anamiliki duka la vifaa vya ushonaji na ubunifu wa mavazi maeneo ya Tabata jijini Dar es salaam) aliingiwa na vumbi kidogo kwenye jicho lake la mkono wa kushoto, na alijaribu kulisafisha jicho hilo kwa maji safi lakini halikupata nafuu na liliendelea kumuuma.Alikata shauri kurudi nyumbani kwake ambapo sio mbali na mahali ilipo ofisi yake, alipofika nyumbani aliendelea kulisafisha jicho lake hilo kwa maji safi, lakini halikupata nafuu yoyote.Usiku kucha hakulala pamoja na kumeza vidonge vya kutuliza maumivu.Ilipofika asubuhi akiongozana na mumewe walikwenda hospiali maarufu hapo jijini Dar iitwayo Regency ambapo alionana na daktari bingwa wa macho na baada ya vipimo iligundulika kuwa mboni ya jicho imepata kidonda na daktari huyo alidai kuwa huenda lile vumbi liliambatana na mchanga na hivyo wakati alipokuwa analisafisha ule mchanga ukawa umejeruhi mboni ya jicho hilo.Kumbe huo ukawa ni mwanzo wa safari ya jicho hilo kupofuka, Christina alinieleza kuwa pamoja na kupatiwa matibabu katika hospiali hiyo lakini hakupata nafuu yoyote na usiku kucha alikuwa akikesha kwa maumivu makali ya jicho hata pamoja na kumeza vidonge vya usingizi lakini hakupata lepe la usingizi.Ilipofika siku ya jumamosi ya January 29, 2011,ikiwa ni siku kumi tangu aanzwe na tatizo hilo, jicho likapoteza uwezo wa kuona na mboni ya jicho ikageuka na kuwa kama ina mtoto wa jicho, kwa maelezo yake Christina alisema kuwa hata yule daktari bingwa wa macho pale Regency alionekana kuchanganyikiwa kutokana na hali ile na alionekana kukata tamaa, lakini hata hivyo alimwandikia dawa nyingine na kumtaka akazitumie kisha arudi siku ya jumanne.Aliporudi nyumbani walishauriana na mumewe na wakakata shauri kuhamia katika Hospitali ya CCBRT ambayo ndiyo hospitali maarufu hapo nyumbani ambayo inasifika kwa kutibu matatizo mbalimbali ya ulemavu yakiwemo matatizo ya macho.Siku hiyo ya jumatatu ya Januari 31, 2011 aliyonitumia ujumbe mfupi, ndiyo siku ambayo alikwenda CCBRT. Baada ya vipimo, daktari aliyempima bila kutafuna maneno alimweleza waziwazi kuwa jicho limeshapofuka, na alimlaumu eti amechelewesha jicho huko vichochoroni mpaka limepofuka ndio anakwenda kwao…..Kauli hiyo ilimshangaza sana Christina, kwani tangu alipopata tatizo hilo alikwenda kupata matibabu kwenye Hospiali ya Regency ambayo inatambulika na inasifika kwa matibabu, sasa iweje alaumiwe na kuambiwa kuwa alikuwa vichochoroni? Christina alionesha kushangazwa kwake na maadili ya Daktari yule.Yule Daktari ambaye ni Mtanzania mwenzetu (Hospitali hiyo inayo pia wataalamu wa kigeni) alimweleza kuwa tiba pekee iliyobaki ni kuweka uzingativu kwenye kutibu kidonda tu, na hata akipona hataweza kuona kabisa kwani jicho limeshambuliwa na bacteria kiasi kwamba limeharibiwa kabisa. Hata hivyo alikiri kushindwa kubaini aina ya bakeria waliomshambulia, pamoja na kukwangua kidonda hicho na kupima maabara.Aliandikiwa aende siku ya Jumanne ya Februari 1, 2011, kwa ajili ya operesheni ndogo ya kuliweka dawa na kulifunga.Wakati naongea naye kwenye simu walikuwa wamekata shauri yeye na mumewe wamgeukie Mungu wakaamua waende kwenye maombi.Nilimuuliza zaidi ya mara mbili kuwa ana imani akienda kwenye maombi atapona, na alinijibu kwa kujiamini kabisa kuwa daktari pekee aliyebaki ni mungu.Ingawa tunatofautiana kimadhehebu, Christina yeye ni Msabato na mimi ni Mkatoliki, lakini nilimuahidi kuungana naye katika maombi.Ni kweli siku iliyofuata alinijulisha kuwa aliombewa na Mwinjilisti mmoja wa kanisa la Wasabato la Chang’ombe SDA aitwae James Ramadhan Rajabu na maumivu yakatoweka na jicho likafunguka na likaanza kuona siku hiyo hiyo….ingawa hata hivyo bado lilikuwa linaonekana kama lina mtoto wa jicho.Aliniambia kuwa anasafiri kwenda Moshi KCMC kuendelea na matibabu lakini bado imani yake kwa Yesu ni kubwa na anaamini atapona, kwani Mungu ndiye atakayekuwa Daktari mkuu atakayewaongoza Madaktari watakaomtibu huko KCMC.Tuliendelea kuwasiliana hata alipokuwa huko Moshi KCMC, na alinijulisha kuwa awali madaktari wa KCMC walikanusha kuwa jicho lake limepofuka baada ya vipimo, ingawa hawakuweza kuona aina ya bacteria waliomshambulia.Walishauri alazwe halafu watajaribu kuwasiliana na daktari mwingine bingwa aliyeko Nairobi ili kuangalia kama anaweza kuja hapo KCMC kushughulikia kesi yake ambayo hata wao iliwachanganya sana, hasa baada ya kuwaeleza kuwa CCBRT wameshindwa kutibu jicho lake.Siku iliofuata yule daktari kutoka Nairobi alifika na baada ya kulipima jicho lake mara kadhaa hakupata majibu ya kueleweka, aliamua kuchuna sehemu ya kidonda na kuchukua sampuli ambayo ingepelekwa Nairobi kwa ajili ya vipimo katika maabara kasha. Aliamuandikia dawa za matone ambazo zitazuia wale bacteria wasiendelee kushambulia jicho lake wakati akisubiri majibu.Katika kipindi chote alichokuwa amelazwa hapo KCMC akisubiri majibu ya vipimo vyake kutoka Nairobi, alikuwa akiendelea na maombi kwa kushirikiana na Mwinjilisti James pamoja na Wainjilisti wengine wa dhehebu lake la Kisabato aliowataja kwa majina ya Mwinjilisti Japhet Magoti Matotiwa kanisa la Manzese, na Mwinjilisti Benson Kilango Izoka wa kanisa la Bombo SDA Tanga.Baada ya siku tatu yule Daktari alirudi na majibu, lakini cha kushangaza alikuta kidonda kimepona kwa asilimia 75. Hali ile haikumshangaza yule daktari peke yake bali pia Madaktari wenzie nao walishangazwa na kule kupona kwake kwa haraka.Kwa mujibu wa majibu aliyokuja nayo, iligundulika kuwa jicho la Christina lilishambuliwa na Fangasi.Aliandikiwa dawa na siku iluyofuata ikiwa ni siku ya tano tangu alazwe Hospitalini hapo aliruhusiwa kurudi nyumbani Dar, lakini alitakiwa kurudi klinik baada ya wiki mbili ili kuangaliwa kama anaendeleaje.Baada ya kurudi Dar, aliendelea na dawa pamoja na maombi, na ilimchukua wiki moja tu kupona kabisa, na jicho kurudi katika hali yake ya kawaida.Aliporudi Moshi KCMC, Daktari alithibitisha kuwa amepona kabisa, na hakusita kuweka bayana kuwa kupona kwake kumekuwa ni kwa miujiza kwa sababu kutokana na hali ya jicho lake walidhani ingechukua muda mrefu hadi kupona.Jana nilizungumza naye kwa muda mrefu sana akinisimulia safari hii ndefu ya ugonjwa wake huo na jinsi maombi pamoja na imani ilivyomsaidia kupona kwa haraka.Kwa kweli nimejifunza jambo moja kubwa sana kutokana na mkasa huu uliompata wifi yangu huyu wa hiyari ya kutokata tamaa pale tupatapo changamoto za kimaisha kama vile ugonjwa na hali zetu kimaisha.Kama Christina angekata tamaa na kusikiliza ushauri wa Daktari wa CCBRT, ni wazi kuwa leo hii angekuwa amepofuka jicho moja. Lakini yeye mwenyewe alidai kuwa alikataa katu katu kukubaliana na maelezo ya Daktari yule na aliiambia nafsi yake kuwa jicho lake halijapofuka na halitapofuka.Naamini hata wewe unayesoma hapa kuna jambo utakuwa umejifunza.Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Christina kwa kuwa na ujasiri wa kukabiliana na changamoto hiyo. Namuomba Mungu aendelee kuibariki familia yao, awape ujasiri wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha, na asiwape moyo wa kukata tamaa.Nimejifunza kutoka kwa Christina.
Na haya yalikuwa maoni ya wadau.....


Anonymous said...
dada yasinta ..nimeguswa sana na kisa cha christina..kwa sababu hakijatofautiana sana na cha mume wangu..kweli tunatakiwa tujifunze kutokata tamaa.
March 1, 2011 9:23 AM
Anonymous said...
Unajuwa ,Yasinta mkasa hu ni ushahidi tosha,kwa sisi binadamu,tunapo kabiliwa na shida au tatizo,liwe la mardhi nk,imani nikitu muhimu sana.vile vile mungu nimkubwa, na ananiayake na makusudi yake itokeapo shida ama tatizo kama hilo.mimi huamini kilakitu kitokeacho kwa binaadamu nimapenzi ya mungu.kama ni mkono wa binadamu na hila zake basi utateseka kwa muda lakini ,kwa imani na mapenzi ya mungu utapona.Lakini kama yeye ameaamua hataufanyeje utapofuka tu.na mwisho nisawa na tunavyo amini kuhusu kifo.unakuta mtu anapata ajali mbaya sana amboyo labda katika gari lile wote wamepoteza maisha, na ni mtu mmoja tu ka pona.hapo yatasemwa mengi,ikiwemo bahati,au mungu atasifiwa kwa sana,na wakati mwingine utambiwa jamaa alisali sana kabla hajaanza safari.Hivyo imamani ,jitihada,uvumilivu na uelawa/ufahamu nimsingi katika kukuvusha katika shida au tatizo linalo kukabili . kaka s
March 1, 2011 10:46 AM
Mija Shija Sayi said...
Mungu ni mwema. Tunaambiwa kwamba wanaadamu tumepewa jina moja tu ambalo kwalo kila kitu kinawezekana ukiamini hivyo. Jina la YESU.Tunaambiwa kwamba ktk majina yooooote hapa duniani hakuna lipitalo nguvu Jina la YESU, na yote yatalitii jina hilo, sasa FUNGUS nalo si ni jina?FUNGUS imelitii jina la YESU.Mbarikiwe wote...
March 1, 2011 12:11 PM
Koero Mkundi said...
Nimeishiwa maneno..... Nakumbuka niliwahi kumtumia kaka Shaban Email ya kumjulia hali na alinijibu tu kwa kifupi kuwa yuko KCMC Moshi akimuuguza mkewe ambaye alilazwa huko kwa kuumwa na Jicho. Nasikitika kwamba sikuwahi kuwasiliana naye tena, sijui ni usahaulifu au ni kitu gani.....Ni mara nyingi katika baadhi ya makala zangu za huko nyuma nimewahi kuandika juu ya somo la imani, na nimekuwa nikieleza kwa kirefu sana jinsi imani ilivyo na nguvu, lakini naomba nikiri kuwa pamoja na kuandika sana juu ya imani lakini siamini kama ninayo imani inayomfikia Christina. Huo ndio ukweli wenyewe.Dunia hii imetawaliwa na mapepo ya kila aina na kama mtu asipokuwa na imani basi anaweza kwenda na maji. Ahsante sana dada Yasinta kwa juhudi zako za kushirikiana na Christina katika maombi, na pia kupata muda wa kufanya naye mazungumzo hadi kutuwekea ushuhuda huu ambao kwa kweli utawafunua wengi.Mwisho napenda kuwapongeza Wainjilisti James Ramadhan Rajabu, Benson Izoka ambaye namfahamu ingawa sidhani kama yeye ananifahamu, Mwinjilisti Magoti huyu nimeshawahi kukutana naye pale Manzese SDA kwenye Effort moja, na washiriki wengine ambao kwa njia moja au nyingine walishirikiana na Christina kwenye maombi katika kipindi chote cha madhila yake.Mungu ashukuriwe.nami nimejifunza kutoka kwa Christina...
March 1, 2011 12:21 PM
Mija Shija Sayi said...
Dah! dah! Yasinta nimekukubali wewe ni shapu si mchezo..siamini..Nafikiri umeelewa naongelea nini.Ubarikiwe.
March 1, 2011 2:50 PM
Anonymous said...
Samahani kwa mwandishi, naomba kuweka kumbukumbu sawa. Mwinjilisti James Ramadhan Rajabu ni wa Kanisa la Tabata Chang'ombe.Ukitaja Chang'ombe tu, mtu mwingine anaweza kudhani ni Temeke Chang'ombe.nami natoa pole na pongezi kwa dada Christina kwa ujasiri wake.Imani ina nguvu sana. nami nimejifunza pia.Liz wa Tabata
March 1, 2011 5:31 PM
Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...
Ni kisa cha kugusa moyo. Yote yawezekana ati!
March 1, 2011 6:05 PM
Lisa said...
Inafunza sana if you have faith as small as a mustard seed, you can say to this mountain, 'Move from here to there' and it will move.Yasinta topic ni ushuhuda wakutosha hakuna lisilo wezekana kwa yesu hongera sana kristina mungu awabariki wote.
March 1, 2011 7:40 PM
Swahili na Waswahili said...
Hongera sana da Christina kwa kunga'nga'nia njia ya uzima na kweli!Mungu azidi kukubariki,Kuhusu ccbrt nami nilishakwenda pale kwa vipimo, nikaonekana ninatazizo la macho na natakiwa kuvaa miwani haraka sana, wakanipatiwa yanayo nifaa na bei yake,Mungu ni mwema siku hiyo pia nikuwa na ahadi Ubalozi saa 8 mchana,hapo ilikuwa saa 6.Nikawaambia nitarudi kesho kuichukua,kwenda ubalozi nikapata visa na tukashauriana na baba watoto tukaona tuachane nayo,kuja huku nikapimwa tena nikaambiwa tatizo langu si kuivaa miwani kwa sasa labda niaka 15/20 ijayo.Wakaniuliza ulipima wapi?nikawaambia na kuwapa vyeti vyangu vya huko yaani walilaumu sana.Asante da yasinta kwa kuungana nasi na mafundisho haya!Mungu wetu hashindwi na jambo kama kweli unamuamini na kufuatanjia zake!.
March 2, 2011 12:38 AM
Celestina said...
Kweli hata mim nimejifunza kutoka kwa dada Tina kutokata tamaa.mungu ndo kila kila kitu katika maisha yetu,hata kwa bible amesema 'sitawaacha waaibike wanitengemeao.'Be blessed.
March 2, 2011 12:21 PM
Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...
Nguvu ya imani hakuna awezaye kuipinga!Pole sana da Tina na hongera kwa ujasiri!
March 2, 2011 3:12 PM
NN Mhango said...
Pamoja na tukio hili kugusa nyoyo na kufunza, tuchunge kutoa hitimisho la jumla kuwa imani ni tiba. Inategemea na imani. Maana kuna imani nyingine ni potofu zinaleta maangamizi kama vile ugaidi na mauaji ya kinyama ya albino. Shukrani dada Yacinta kukubali kushiriki nasi tukio hili.
March 2, 2011 8:52 PM
Jeff Msangi said...
Kisa au mkasa wa aina yake.Nilichoambulia mimi ni kitu kinachoitwa Power of Faith au Nguvu ya Imani.Ukiamini hakuna kisichowezekana.Asante Yasinta kwa ushuhuda huu wa Christina.The Lord is alive
March 3, 2011 1:46 AM
Salehe Msanda said...
Habari za siku kadhaa,Nimerudi kutoka mapumzikoNi kweli hilo somo tosha na ni muhimu kila wakati kuwa na matumaini kuliko kukata tamaa na hasa suala lenyewe kama linahusiana na afya yako. maana afya haina mbadala.Tumshukuru muumba kwa kuweza kumuongoza wifi yako kufikia uamuzi wa kuamini kuwa mungu yuko naye na atapona.Ni somo zuri na lina mafundisho mengi kutokana na kile kilichotokea na kwa watu wataalamu wa afya tunanaowaamini na kuwakadhi dhamana ya maisha yetu.Kila la kheri.
March 3, 2011 11:02 AM
emu-three said...
Kweli imani ni tiba, hasa unapokabiliwa na magonjwa ambayo `wataalamu wetu' wanasema `haiwezekani...usikate tamaa na muombe mungu wako kwa imani yako...utafanikiwa, lakini hakikisha kuwa `imani' ipo!
March 3, 2011 12:44 PM
Upepo Mwanana said...
Nijuavyo mimi, madakatari bingwa wa macho kwa Tanzania ni wachache sana, na hata hospitali kubwa zenye majina makubwa , nyingine hazina madakatari bingwa wa macho, ukifika unapokelewa na wasaidizi ambao kwa sera za nchi yetu ati wanatambulika kama madaktari.Hata CCBRT madaktari bingwa ni wachache, na wamejaa wasaidizi.Wanchi siku hizi tunapaswa kujifunza japo huduma ya kwanza na elimu kidogo ya magonjwa tujimudu na bidhaa feki hizi zinazojiita madaktari bingwa! Namkumbuka Kaka yangu Chib, nina imani anaweza kutoa mchango zaidi katika masuala haya ya macho!
March 3, 2011 1:25 PM
Mija Shija Sayi said...
Yasinta upo?
March 5, 2011 5:45 PM
chib said...
Habari hii imenigusa sana, tena moyoni kabisa.Nasikitika iwapo mtu ataangukia kwa mtu asiye elewa sawa tatizo la mwingine na kuishia kumwaga uongo ili aonekane kama anajua.Hospitali alizopitia Christina, nazifahamu vyema tena sana.Nina mengi ya kusema kutokana na maelezo ya Christina, lakini kusema bila kuona, ni sawa na kumwaga uongo zaidi. Kwangu kila moja linawezekana, kwa upande wa kupona haraka, na pia kwa upande wa maelezo ya madaktari. Sijui nisemee upande upi. Ila bado natafakari kwa KCMC kumuita mtaalamu kutoka Nairobi kuja kuchukua sampuli tu...., bado haijaingia kichwani kabisa.Baadaye nikipata muda, nitatoa mada ndefu kuhusu vidonda katika uso wa jicho. Nashukuru Tembe kwa kunikumbuka, japo nipo nahudumia waafrika wenzangu mbali na nyumbani.Lakini tupo pamoja
March 8, 2011 5:08 PM
Anonymous said...
NAOMBA NAMBA YA CHRISTINA .IMANI YAKE IMENITIA MOYO
March 10, 2011 7:16 AM


Ebu tumaliza kwa kusikiliza wimbo huu:-

3 comments:

Upepo Mwanana said...

ahsante kwa kutukumbusha, kumbe hata na mimi nilichangia! Ha ha haaa.

Mija Shija Sayi said...

Huu kwa kweli ni muujiza, anaendeleaje lakini?

Tuko pamoja.

Yasinta Ngonyani said...

Upepo Mwanana! kumbe ulikuwa huji kama hupo juu. Ahsante kwa kuchangia tena.

Mija! Nakwambia imani ni kitu muhimu sana katika maisha. Si muda mrefu sana nimeongea naye anaendelea vema kwa kweli tunamshukuru Mungu. Pamoja Daima.