Sunday, January 3, 2010

NILILAZIMIKA KUCHUKUA MAAMUZI MAGUMU

Ni furaha isiyo kifani kutumiwa barua kama hii na ukizingatia ndio mwaka umeanza tu. Kwa vile napenda kugawana na wasomaji wengine wa blog hii na pia wanablog wenzangu nimeona niufikishe ujumbe huu:- Karibuni sana KUSOMA hapa.


Kwako dada Yasinta, ni matumaini yangu kuwa umzima wewe na familia yako huko uliko.
Dada mimi ni msomaji wa blog yako na nimejifunza mengi sana kupitia blog yako hii ya maisha, kwani mijadala unayoianzisha katika blog yako imekuwa ikileta changamoto na migongano ya mawazo kiasi kwamba nimekuwa nikijifunza mambo mengi kupitia mijadala hiyo.

Kusema kweli nimekuwa ni mfuatiliaji wa blog yako na kupitia blog yako hiyo ya MAISHA nimekuwa nikijifunza mambo mengi juu ya maisha na mafanikio pia.

Mimi ninao uzoefu wangu ambao ningependa uuweke katika blog yako ili wasomaji waweze kujifunza kupitia uzoefu wangu huu.

Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 37 na nina mke na watoto watatu. Kikazi mimi ni mtumishi serikalini na mke wangu by Professional ni mpishi na pia anao ujuzi kidogo wa ushonaji. Mke wangu alikuwa na ndoto za kumiliki biashara ya Catering wakati namuoa kwa sababu aliwahi kufanya kazi kwa mtu mwenye biashara hiyo alipokuwa kwao Mbeya kabla sijamuoa na kuhamia naye Dar, hivyo alitengetengeneza picha kuwa biashara ya Catering ndio biashara pekee yenye faida kubwa.

Ni kweli kuwa biashara ya Catering ina faida kubwa lakini inategema na mtaji utakaoanzishia biashara hiyo. Kusema ukweli nilikuwa na dhamira ya kumuanzishia biashara hiyo ya Catering na nilianza mchakato wa kutekeleza azma yangu, lakini nikakutana na vikwazo vingi sana, kwani ili kuanzisha biashara hiyo ni lazima uwe na vifaa kama Serving Dishes, maturubai, viti na meza, vyombo vya kupikia, sahani, vifaa vya Mziki na MC. Kama ukimudu kuwa na vitu hivyo basi na faida yako itakuwa kubwa kwani shuguli utakazokuwa unapata zitakuwa ni kubwa na zenye kulipa faida kubwa. Kwa mfano hapa Dar shughuli kama harusi, Send Off, Kitchen Party, Misiba, na kumaliza misiba wengine huita kumaliza arobaini, Vipa imara achilia mbali semina ndogo ndogo za kidini na za NGO’s, zote hizo ni kazi ambazo zinategemea sana watu hawa wa Catering, lakini kutokana na mtaji wangu kuwa mdogo nikajikuta nikikwama kwa sababu nilikuta vifaa hivyo vinauzwa ghali kutokana na watu wengi kukimbilia biashara hiyo kwa kuwa inalipa.

Nilikata shauri kumfungulia biashara nyingine ili japo asikae bure bila kazi na pia kuokoa hizo pesa tusije tukazifuja bure. Kwa haraka, niliamua kuanzisha biashara ya ushonaji, pamoja na uuzaji wa vifaa vya ushonaji.

Awali nilipata upinzani mkubwa sana kwa mama watoto na hakupenda hilo wazo langu kabisa, nilipata wakati mgumu sana kumuelimisha mpaka akakubali lakini hakuwa na mwamko wa kuipenda kazi hiyo. Sikukata tamaa, niliendelea kumuelimisha huku nikiendelea kununua vifaa kama vyerehani vitatu na ya kudarizi kimoja pamoja na vifaa vya ushonaji vya kuweka dukani kwa ajili ya kuuza na vifaa vingine muhimu kama makabati nakadhalika na kulifungua duka hilo rasmi. Hata hivyo nilimuahidi kuwa ahadi yangu iko pale pale, nitamfungulia biashara yake ya Catering kama nilivyomuahidi wakati ukifika.

Hata hivyo mwanzoni hakuipenda biashara hiyo na nilikuwa kama vile namlazimisha kwenda dukani kufungua kila siku asubuhi, lakini sikukata tamaa.

MSHANGAO………..

Dada siku za karibuni biashara ikaanza kukua na wateja wakaanza kuja kwa wingi kununua bidhaa, na mtaji umeanza kukua sasa. Hivi karibuni katika mazungumzo yangu na yeye nikamwambia kuwa mpaka mwezi wa pili mwakani nitakuwa nimemfungulia biashara yake ya Catering kama nilivyoahidi, ili ndoto yake itimie, lakini kwa mshangao aliruka na kukataa kabisa kuwa hataki tena biashara ya Catering kwani ile biashara ya ushonaji ina faida na ameipenda sana.

Sikuamini masikio yangu. Unajua wakati nabishana naye kuhusu kuanzisha biashara ya ushonaji nilidhani yeye yuko sahihi kuwa hiyo biashara haifai, na ilikuwa nusura nikubaliane naye, ila kuna kitu huwa tunaita machale au mlango wa sita wa fahamu, ambao huwa nautumia katika kufanya maamuzi magumu.

Baada ya kutafakari sana niliamua kufungua hiyo biashara, na sasa nimepata jibu kuwa nilikuwa sahihi, maana ameuona ukweli kuwa wazo langu lilikuwa ni sahihi. Kuna msemo mmoja unasema kuwa mwanaume ni kichwa cha nyumba, ki ukweli sikuwa nauzingatia huo msemo kwa kuwa niliona ni dalili ya kujikweza na kuwadhalilisha wanawake, lakini nadhani hiyo dhana ina ukweli fulani.

Nimejifunza jambo moja, kuwa kuna wakati mwanaume analazimika kuwa dikteta ili kufikia maamuzi fulani magumu, hasa pale mke anapoonekana kupinga bila kutoa wazo mbadala au kutoa ushauri.

Sio kwamba wanawake hawawezi kutoa ushauri au wazo zuri, la hasha, ninachomaanisha hapa ni kwamba kuna wakati kunapohitajika maamuzi magumu, mume anatakiwa kupewa nafasi ili aamue. Ila inategemea tabia za mume huyo.

Inasemwa kuwa nyuma ya mafanikio ya mume kuna mke na nyuma ya anguko la mume kuna mke pia, lakini huwa najiuliza, je utamjuaje mke ambaye maamuzi yake yanakupeleka shimoni?

NAWATAKIENI JUMAPILI HII YA KWANZA YA MWAKA 2010 IWE YA FURAHA TELE!!

7 comments:

EDNA said...

Jumapili yako na iwe njema dada Yasinta.

Mija Shija Sayi said...

Si uongo hata kidogo, kabla hata sijasoma hii habari hilo huwa nalijua nakukubaliana nalo kabisa kwamba kuna wakati mwanaume ni lazima awe dikteta ili mambo yaende ndani ya familia, ila ni lazima uwe udikteta wenye upendo na sio uliojaa ubabe na manyanyaso.

Stay blessed mleta habari hii.

Bennet said...

NAhisi MUNGU aliamua kukuonyesha njia ya kupitia wewe na mkeo kufika kwenye mafanikio, ingawa nyinyi mlidhani hamko sahihi lakini yeye (MWENYEZI MUNGU) ndio aliwaelekeza kufanya hilo

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

siku zote uamzi wa kwanza ndo uamzi wa kweli.... :-)

nadhani cha muhimu ni majadiliano katika jumba

Cheers

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

Huyu jamaa du,
Kuna wakati tunalazimika kupitia katika shughuli Fulani ili tuzifikie zile tuzipendazo.

Swali lake la kutaka kujua juu ya mwanamke ambaye ushauri wake utakupoteza / kukupeleka shimoni ndo sielewi, anataka kumjua wanini wakati hamwitaji?
Pia nyuma ya kila mwanamke aliyefanikiwa kuna taraka (divorce)
Labda yasinta na koero ushauri wao unaweza kukupeleka shimoni ndo maana wamejitangaza kuachana na blog harafu wakabadili uamuzi!

labda inabidi kuwa Idd Mani au Hitlerr kidogo ili mambo yawe mambmo

chib said...

Kuwa kadikteta fulani... DUH!!

MARKUS MPANGALA said...

<><><>