Wednesday, August 28, 2013

PALE WAZAZI WANAPOWACHAGULIA WOTOTO/MABINTI ZAO WACHUMBA!!!

Habari za jioni ndugu zanguni....Hivi karibuni nimetumiwa email kutoka kwa msomaji wa maisha na mafanikio kutoka huko nyumbani Tanzania ikiwa na ujumbe huu na kuniomba kama naweza niuweka hapa kibarazani ...karibu tujadili kwa pamoja
--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Kuna mdada mmoja ambaye ni miongoni mwa watu wasomi sana. Amemaliza chuo hapa mlimani. Wakati alipokuwa chuoni alibahatika kupata mchumba ambaye walikubaliana kuoana. Na walikuwa katika maelewano mazuri katika uchumba waoi.

Baada ya uchumba huo kuendelea, aliamua kumpeleka kwa wazazi wake na kuwafahamusha kuwa mimi nimepata mtu ambaye naona atanifaa katika maisha yangu. Baada ya kuwafahamisha jambo hili, mama dada huyo alikubaliana na wazo lake la kutaka kuolewa na huyo mchumba wake lakini upande wa baba yake kulikuwa na shaka. Huyo binti alikuwa karibu sana na baba yake na aligundua kuwa baba yake hataki kukubaliana na wazo lake. Baada ya mazungumzo ya hapa na pale na baadaye mvulani yule kuondoka, binti alimfuata baba na kuzungumza naye na akasema kwa jinsi nilivyomwona huyo mvulana hakufai. Binti akamwambia si vizuri kumhukumu mtu kwa kumwangalia tu. Mimi nimekuwa naye muda mrefu namfahamu vizuri sina shaka naye. Baba yake bado hakukubalina na hilo lakini upande wa mama yake hakukuwa na shida.

Uchumba uliendelea na yule mvulana akasema inaonyesha baba yako hataki kabisha, lakini nitaumia sana endapo kama bado ataendelea na msimamo wake huo. Ni mtu ambaye nimekuzoea, tumeheshimiana sana. Yule binti akamwambia kila kitu kinawezekana na itawezekana tu.

Siku moja yule binti akiwa katika mizunguko yake ya hapa na pale akiwa mjini, alikutana na kaka mmoja akiwa katika mavazi ya kijeshi, na alikuwa na mwonekano mzuri sana, lakini cha kushangaza yule kaka baada ya kumwona binti yule aliduwaa. Baada ya kuduwaa kwa kipindi aliamua kumfuata binti na kumsalimia na kumuuliza kila kitu, na baadaye walianza kuwasiliana mawasiliano ya kawaida kabisa lakini mwanajeshi huyo alikuwa na mawazo tofauti, na ndipo siku moja akamweleza kuwa angetamani siku moja awe mke wake. Yule binti akamwambia hapana, mimi tayari nina mtu wangu na tunaheshimiana sana, akamwambia sawa. Kwa vile  ni watu marafiki alimrudisha mpaka kwao, kumbe lengo lake yule kijana ni kutaka kujua binti anaishi wapi.
Na ndipo siku hiyo yule kijana aliamua kwenda peke yake nyumbani kwa wazazi wa binti huyo na kukutana na baba yake (Baba wa binti). Na ndipo alipozumza ukweli wa kile alichokiona na lengo lake ni lipi. Na mzee aliweza kumdadisi kijana na kumweleza kila kitu. Kwa  wakati huo yule binti pamoja na mama yake walikuwa hawapo na binti aliporudi akamweleza akaelezwa na baba yake kuwa kuna kijana mmoja alikua yuko hivi na hivi akanieleza kila kitu, nadhani huyo ndiye atakayekufaa. Binti akamwambia hapana, wewe ndiye umemwona na mimi itabidi nimwone. Baadaye yule mjeshi akaja wakazungumza.

Baada ya mazungumzo marefu ya hapa na pale yule kijana mjeshi aliamua kuondoka, na kwa kuwa binti hakutaka kukorofishana na baba yake aliamua kukubaliana na mawazo yake na baadaye wakamwita tena kijana huyo mjeshi. Baadaye taratabu zote za kuoana na mjeshi huyo zikafanyika, kisha binti huyo alienda kwa mchumba wake wa kwanza na kumweleza yote yaliyotokea na kumrishia pete ya uchumba waliyovishana hapao awali. Kijana huyo alisikitika sana kwa uamuzi aliouchukua lakini hakuwa na jinsi aliamua kufuata shinikizo la baba yake. Hatimaye baadaye yule binti aliolewa na mwanajeshi na ndoa ilifungwa kanisani.

Baada ya ndoa tu kinachotokea sasa hivi ni kwamba kosa kidogo tu anaambulia kipigo ambacho hajawahi kukipata, kiasi kwamba inampelekea kumkumbuka yule wa kwanza ambaye walikuwa wakiongea naye kwa utaratibu kabisa.

Ndipo baadaye binti (ambaye sasa ni mke wa mwanajeshi) akamtafuta yule mchumba wake wa kwanza na kumweleza kila kilichotokea. Lakini kijana huyo alijaribu kumweleza namna ya kufanya ili waendelee kuishi vizuri na mume wake na kuzidi kumwombea ili waishi vizuri.

Kwa wakati huu kijana huyo bado hajaoa na anamweleza binti itachukua muda mrefu kwa sababu kwanza itabidi nikusahau wewe pili nikae chini nitulie tatu nijianze upya hivyo itachukua muda sana.
Kikubwa zaidi ni kuwa binti huyo amekubali kuolewa na mwanajeshi kwa shinikizo la baba yake, lakini kinachoendelea ni kwamba kosa dogo tu anaambulia kipigo kisicho cha kawaida na kinachomuuma zaidi zaidi huyo dada ni kuwa siku moja walipotoka NJE walienda sehemu ile ile ambayo walikuwa wakienda na mvulana yule wa kwanza na hivyo hii humuuma zaidi.
Sasa dada huyu anaomba mawazo, ushauri na maoni afanyeje???

5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ngoja nianze kutoa yangu niliyo nayo moyoni...Huyu dada amefanya kosa nionavyo mimi najua ni mila na daesturi lakini yeye ilibidi ausikilize moyo wake maana yeye ndiye atakayeishi na huyo MUME na si BABA. Sasa anagalia anapata mateso, baba yupo wapi?? hayupo....mmmmhhh naoana nina hasira hapa ngoja nitulie nitarudi tena....

Anonymous said...

Hii ni fundisho kwa mababa wenye tabia ya kulazimisha mabinti zao kuolewa na wanaume wasiowajuwa/wasiowapenda. By Salumu.

Shalom said...

Bint alikurupuka angeweka msimamo kwa baba yake wala asingekataa ndoa ni watu wawili wazazi wanashirikiswa tu ili kutoa baraka lkn yy kamsikiliza baba ndio matatizo hayo yanampata arudi kwa baba yake amueleze kipigo anacho kipata kutoka kwa mwanaume wake maana kama walisha funga ndoa ya kanisa ndio mzigo wake huo mpaka kifo

Anonymous said...

pole dada wa watu ndo hy bb ajfunze tena kutokana na makosa alyofanya

Penina Simon said...

Hana jinsi maji keshayavulia nguo hana budi kuyaoga, Ila namwonea huruma hasa kama alishapata nae watoto ndio atazidi kumsumbua/kumtesa. na kwa uzoefu nilio nao wanaume hao huwa hawajirekebishi baadae hata akiamua kuondoka huyo mwanaume anaweza kumfanyia kitu kibaya (hata kumuua).