Monday, October 29, 2012

HUYU NDIYE YASINTA NGONYANI!!!

Nimeamka leo na mawazo mengi sana kichwani mwangu kuhusu huyu mdogo wangu wa hiari Koero Mkundi. Sijawasiliana naye kwa muda sasa nafikiri yupo salama. Baada ya kufikiri sana nikakumbuka mada hii nikaona ngoja niiweka hapa ni kumbukumbu kubwa sana kwangu.

Yasinta Ngonyani, Picha kwa hisani ya Maisha Blog
Ni binti halisi wa kitanzania, ingawa anaishi ughaibuni lakini hujivunia asili yake na utaifa wake, ni binti pekee aliyejitolea muda wake kuwaelemisha watu wa rika zote bila kujali rangi, kabila, itikadi, taifa wala jinsia.

Binti huyu si mjivuni na hupenda kubadilishana mawazo na watu mbali mbali, na pia hupenda kufuatilia habari za nyumbani kwao alikotoka na haoni tahayari kuongea lugha ya kwao. Daima hujitambulisha kwa jina la asili ya kwao na huona fahari kutumia jina hilo.

Binti huyu hakuona ajizi kuwajuza wanae asili ya kwao japo wamezaliwa ughaibuni, amekuwa msitari wa mbele katika malezi ya wanae ili kuhakikisha wanae hao hawajitengi na asili ya aliotoka yeye.

Si mchoyo wa ushauri na kupitia makala zake aziwekazo kibarazani kwake amekuwa ni msaada kwa wengi, amekuwa mstari wa mbele katika kuilemisha jamii bila kujali rika. Amejitolea kufundisha kile akijuacho juu ya malezi na matatizo mbali mbali yanayowakabili wanandoa na malezi ya watoto.

Kibaraza chake kimekuwa ni kitovu chenye kukutanisha wadau mbali mbali wenye fikra pevu, na kuibua mijadala yenye kuelimisha, kufundisha, kuburudisha na kuhuzunisha pia.

Binafsi napenda kumuita dada na kwangu mimi ni zaidi ya dada, kwani amekuwa ni mwalimu mzuri kwangu nikijifunza mambo mengi kupitia kibaraza chake nimekuwa nikijifunza mengi, na sisiti kukiri kwamba chimbuko la kibaraza cha VUKANI ni kutokana na kile nilichojifuza kwake.

Ni mkweli na muwazi, na hasiti kusema wazi hisia zake, lakini huwa makini sana ili kuepuka kumuumiza mtu mwingine kihisia, na kama kwa kusema huko kutamkera mtu mwingine, ni mwepesi kuweka sawa maelezo yake ili kuondoa msigishano wa mawazo.

Nakumbuka wakati fulani nlipopata msongo wa mawazo kutokana na tofauti zangu na wazazi wangu, alikuwa ni mtu wa kwanza kunitumia email binafsi akijaribu kuniliwaza na kunitaka nisichukue hatua yoyote kujidhuru, naomba nikiri kwamba email ile ilinisaidia sana kurudi katika hali yangu ya kawaida na nilijisikia fahari kuona kwamba kuna mtu ananipenda na kunijali japo sijawahi kuonana naye uso kwa uso.

Huu kwangu ulikuwa kama muujiza, inakuwaje, mtu kusoma mawazo yangu kupitia blog tu halafu awe karibu nami kiasi hiki, ni kitu gani kimemvuta? Kusema kweli tangu siku hiyo niliamni kuwa maandishi yana nguvu sana na kupitia maandishi yawezekana mtu mwingine kukufahamu vizuri sana.

Nimekuwa karibu sana na binti huyu, na amekuwa ni mwema sana kwangu na mshauri wangu pia, na kupitia vibaraza vyetu, tumekuwa tukibadilishana mawazo na kupeana ushauri mbali mbali ili kuboresha ustawi wetu na wa familia zetu.
--------------------------------------------------------------------------
KOERO HUKO ULIKO MUNGU AKULINDE NAKUKUMBUKA SANA KILA SIKU UWE SALAMA.


7 comments:

ray njau said...

Je, Ungependa Kuwa na Marafiki wa Karibu?
WATU wengi wangependa kuwa na marafiki wa karibu. Maisha hufurahisha zaidi unapowasimulia marafiki wa karibu mambo uliyojionea maishani. Hata hivyo, unaweza kuwapataje marafiki wa kweli? Karibu miaka 2,000 iliyopita, Yesu alionyesha kwamba ili kufaulu katika uhusiano wowote ule wa kibinadamu jambo muhimu zaidi ni kuwa na upendo usio na ubinafsi. Alifundisha hivi: “Kama vile mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni wao vivyo hivyo.” (Luka 6:31)Maneno hayo yanaonyesha kwamba ili uwe na marafiki unahitaji kuwa mkarimu na kuepuka ubinafsi. Naam, ili kuwa na rafiki, wewe pia unahitaji kuwa mwenye urafiki. Jinsi gani?
Urafiki wa karibu na wenye shauku hauwezi kusitawishwa kwa siku moja. Kuwa marafiki ni zaidi ya kujuana tu na mtu. Marafiki ni watu ambao unashikamana sana nao kihisia. Kusitawisha na kudumisha urafiki wa karibu kunahitaji jitihada. Mara nyingi, unahitaji kutanguliza mahitaji ya rafiki yako kabla ya mapendezi yako mwenyewe. Marafiki hushirikiana wakati wa shangwe na wa huzuni.
Unaonyesha kwamba wewe ni rafiki wa kweli hasa kwa kumsaidia mtu mwenye uhitaji kihisia na kwa njia nyinginezo. Andiko la Methali 17:17linasema hivi: “Rafiki wa kweli anapenda nyakati zote, naye ni ndugu aliyezaliwa kwa ajili ya wakati wa taabu.” Kwa kweli, huenda uhusiano wa kirafiki ukawa wenye nguvu zaidi kuliko uhusiano wa kifamilia. Andiko la Methali 18:24linasema: “Kuna rafiki wanaoelekea kuvunjana vipande-vipande, lakini yuko rafiki anayeshikamana na mtu kwa ukaribu zaidi kuliko ndugu.” Je, ungependa kujua mengi zaidi kuhusu jinsi ya kudumisha urafiki mzuri? Je, ungependa kuwa miongoni mwa watu ambao wanajulikana kwa kuwa na upendo kati yao? (Yohana 13:35 Ikiwa ndivyo, Mashahidi wa Yehova katika jumuiya yenu watafurahi kukuonyesha jinsi ya kupata marafiki wa kweli.

chib said...

.....
Ama baada ya salamu ..... uliye mbali nasi .....
Dhumuni la .......

Basi ujue nilikuwa nimepotea, kuibuka nikadhani nipo hukooo.

Siku njema!!

Anonymous said...

Ni kweli kabisa.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Ray, kaka Chib na kaka Goodluck! Ahsanten sana kwa kuwa nami...pamoja daima

Anonymous said...

Rafiki yangu wa Hiari, aliyosema mdogo wetu Koero kuhusu wewe ni kweli kabisa, nakuombea kwa Mungu akuzidishie upendo na apate kukumiminia baraka tele.
Na mimi naomba nichukue nafasi hii kukwambia nakupenda sana rafiki yangu wa hiari!

Unknown said...

Mungu akubariki sana Dada yasinta ngonyani.

Anonymous said...

Kweli kabisa.charity begins at home.