Thursday, August 19, 2010

HUYU NDIYE YASINTA NGONYANI!!!

Yasinta Ngonyani, Picha kwa hisani ya Maisha Blog

Ni binti halisi wa kitanzania, ingawa anaishi ughaibuni lakini hujivunia asili yake na utaifa wake, ni binti pekee aliyejitolea muda wake kuwaelemisha watu wa rika zote bila kujali rangi, kabila, itikadi, taifa wala jinsia.

Binti huyu si mjivuni na hupenda kubadilishana mawazo na watu mbali mbali, na pia hupenda kufuatilia habari za nyumbani kwao alikotoka na haoni tahayari kuongea lugha ya kwao. Daima hujitambulisha kwa jina la asili ya kwao na huona fahari kutumia jina hilo.

Binti huyu hakuona ajizi kuwajuza wanae asili ya kwao japo wamezaliwa ughaibuni, amekuwa msitari wa mbele katika malezi ya wanae ili kuhakikisha wanae hao hawajitengi na asili ya aliotoka yeye.

Si mchoyo wa ushauri na kupitia makala zake aziwekazo kibarazani kwake amekuwa ni msaada kwa wengi, amekuwa mstari wa mbele katika kuilemisha jamii bila kujali rika. Amejitolea kufundisha kile akijuacho juu ya malezi na matatizo mbali mbali yanayowakabili wanandoa na malezi ya watoto.

Kibaraza chake kimekuwa ni kitovu chenye kukutanisha wadau mbali mbali wenye fikra pevu, na kuibua mijadala yenye kuelimisha, kufundisha, kuburudisha na kuhuzunisha pia.

Binafsi napenda kumuita dada na kwangu mimi ni zaidi ya dada, kwani amekuwa ni mwalimu mzuri kwangu nikijifunza mambo mengi kupitia kibaraza chake nimekuwa nikijifunza mengi, na sisiti kukiri kwamba chimbuko la kibaraza cha VUKANI ni kutokana na kile nilichojifuza kwake.

Ni mkweli na muwazi, na hasiti kusema wazi hisia zake, lakini huwa makini sana ili kuepuka kumuumiza mtu mwingine kihisia, na kama kwa kusema huko kutamkera mtu mwingine, ni mwepesi kuweka sawa maelezo yake ili kuondoa msigishano wa mawazo.

Nakumbuka wakati fulani nlipopata msongo wa mawazo kutokana na tofauti zangu na wazazi wangu, alikuwa ni mtu wa kwanza kunitumia email binafsi akijaribu kuniliwaza na kunitaka nisichukue hatua yoyote kujidhuru, naomba nikiri kwamba email ile ilinisaidia sana kurudi katika hali yangu ya kawaida na nilijisikia fahari kuona kwamba kuna mtu ananipenda na kunijali japo sijawahi kuonana naye uso kwa uso.

Huu kwangu ulikuwa kama muujiza, inakuwaje, mtu kusoma mawazo yangu kupitia blog tu halafu awe karibu nami kiasi hiki, ni kitu gani kimemvuta? Kusema kweli tangu siku hiyo niliamni kuwa maandishi yana nguvu sana na kupitia maandishi yawezekana mtu mwingine kukufahamu vizuri sana.

Nimekuwa karibu sana na binti huyu, na amekuwa ni mwema sana kwangu na mshauri wangu pia, na kupitia vibaraza vyetu, tumekuwa tukibadilishana mawazo na kupeana ushauri mbali mbali ili kuboresha ustawi wetu na wa familia zetu.

Huyu ndiye Yasinta Ngonyani, kwa kumsoma zaidi bofya hapa.

Makala hii iliandikwa na mdogo wangu wa hiari Koero Mkundi mwaka 2009/08/14 bado nimevutiwa sana na hii makala na nimeona niiweke hapa kwangu pia kama kumbukumbu na pia kujikumbusha yaliyopita kwani si vibaya. Pia nachukua nafasi hii kwa kumshukuru sana mdogo wangu huyu wa hiari Koero Mkundi kwa kazi nzuri anazozifanya kwa kumsoma zaidi kazi zake ingia hapa. Pia nauthamini sana uwepo wake Mwenyezi Mungu na akulinde na akuongoze na yote utendayo yawe mema. Kwanni yeye ndiye mwezeshaji wa yote na yeye ndiye ajua anavyotuwazia maana mawazo atuwaziayo ni mema. Ni hayo tu kwa leo.

18 comments:

ERNEST B. MAKULILO said...

Ni makala nzuri zaidi. Huwa ni furaha pale rafiki yako anapotambua uzuri, tabia yako njema nk na kuweka ktk maandishi, ni zawadi moja nzuri sana maishani.

MAKULILO

San Diego, CA

www.tanzaniasports.com said...

Ni makala nzuri huku ikitupa picha halisi ya Yasinta kwa kumuona vizuri akiwa na taswila tofauti tofauti, yumkini makala imerudiwa,hii inatusaidia tusikusahau!

Marefu said...

Hata mimi nakubaliana na kile kilichoandikwa kuhusu "huyu ndiye Yansinta Ngonyani". Mimi neishi naye japo kidogo na familia yake huko ughaibuni, na nilijione sifa zote zilizoandikwa na mtoa mada. Hongera sana dada Yansinta

emu-three said...

Natamani kukutana naye uso kwa uso, kwani kweli nakubaliana na aliyoandika mwenzetu, mungu akuzidishie uzima na afya tele.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

natamani kujua hata upande mwingine wa huyu Yasinta, maana umeongelewa upande mmoja tu, bila kuwa na upande mwingine, ubinadamu wetu haujakamilika

Shein Rangers Sports Club said...

Ni makala nzuri na yenye ukweli kwani sisi sote ni mashahindi, na angesema uongo juu yako nadhani sisi sote tungeungana kumkemea. Hongera sana dada Yasinta, hata sisi mwaka jana tulitoa makala ndogo sana juu ya sifa zako na ushirikiano wa dhati unaotupa.

Hongera Yasinza Ngonyani!!

SIMON KITURURU said...

Mmmmh!

Malkiory Matiya said...

Sipo mbali na Bwana Makulilo.

Hongera zangu kwa kazi nzuri ya ushauri nasaha uliyompatia Koero pale alipotaka kukata tamaa ya maisha kwa sababu ya msongo wa mawazo uliotakana na changamoto za maisha.

Koero Mkundi said...

Duh! kweli ya kale ni dhahabu. ingawa niliandika makala hii kitambo kidogo, lakini baada ya kusoma tena na tena, nahisi kama sio mimi niliyeandika..... naona kama ni wasifu mzuri sana ulioandikwa kwa ufundi na mtu akufahamuye kwa karibu sana.

Oh! kweli maandishi yana nguvu, hivi niliwaza nini wakati ule? ni swali ambalo bado najiuliza......

Niko hapa Arusha kwa sasa nikiendelea kushiriki shughuli za kifamilia....siku ya leo kwangu mimi ilikuwa imepooza sana na nilitamani nikutane na mtu tutakayebadilishana mawazo, lakini baada ya kufungua mtandao, nimejikuta nikiliwazika kwa makala hii.

Naomba nikiri kuwa dada Yasinta ni tunu kwa mzee Ngonyani na mama Nyonyani (RIP mama Ngonyani( Mungu amrehemu huko aliko)

Ahsante sana dada yangu kwa kumbukumbu hii maridhawa.

PASSION4FASHION.TZ said...

Hongera sana Yasinta umebarikiwa Koero hakupindisha chochote aliyosema ni kweli kabisa,kama utakumbuka huko nyuma niliwahi kukueleza kitu,unakumbuka?

Zaidi tuwashukuru wazazi kwa malezi mazuri,wao ndio wamechangia kiasi kikubwa katika makuzi yako.

Hongera Koero kwa uandishi uliotukuka,jaribu kuandika kitabu wewe ni muandishi mzuri na unakipaji cha hali ya juu sijui kama wewe mwenyewe unajijua.

Yasinta Ngonyani said...

Ndugu Marefu mimi na Familia yangu tungefurahi kujua mwenzetu ni nani. Maana umesema umewahi kuishi nasi. TAFADHALI SEMA WEWE NANI? natanguliza AHSANTE ZA DHATI!!!

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

swaaaafi sana!

NAJUA WAJUA said...

Hongera dada Yasinta kwani watu wamekukubali!!

Maisara Wastara said...

Koero kasema kweli...
You are amazing sissy

Markus Mpangala. said...

AMANI YA BWANA IWE NAWE DAIMA

emu-three said...

Labda niongezee kitu ambacho nimejifunza kwa ada Yasinta, ni mdadisi wa hekima. Mimi nimejifunza kwake kuwa mdadisi, na pia ni mtu asiyekubali kushindwa, na mwenye msimamo!
Ndio maana narudi ausemi wangu ningefurahi kumuoana live, na pili kumjua mume wake kwani huyo mume ana bahati kumpata mke ambaye anajua nini anachokifanya!
Tunakushukuru kwa wewe uliyejaraibu kumuelezea kwani umefanya yale yaliyokuwa moyoni mwetu, mungu akubariki sana

Shabani Kaluse said...

Sifa zote ziwarejee waliyemleta yasinta Ngonyani Duniani!

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Makulilo nakubaliana nawe ni zawadi nzuri pia kumbukumbu nzuri sana.

www.tanzaniasport.com! Nafurahi kama umepata picha halisi ya Yasinta mimi na najua hutanisahau kamwe.

Ndugu Marefu kama nilivyokuuliza wewe ni nani. Nimefurahi kuona kuna mtu nimeishi naye na simfahamu.

emu-three ipo siku utakutana nami. kumbuka milima haikutani bali wanadamu hukutana.
Kamala ni upende gani huo utakao kujua kuhusu huyu Yasinta?

Shein Rangers Sports Club naikumbuka ile makala na nasema tena na tena Ahsante sana.

Simon! kwanini mmmmh!

Malkiory! ahsante kwa kunikumbusha hilo.

Mdogo wangu Koero! wewe mwenyewe hujijui tu au unafanya makusudi ni mara nyingi sana wengi wamekuambia ya kwamba wewe ni mwandishi mahiri lakini unafikiri wanakutania au? Ahsante mdogo wangu wa hiari ambaye hata hatujawahi onana.

PASSION4FASHION.TZ! umesema kweli dadangu nami nawashukuru sana walezi/wazazi wangu. Na pia Koero kwa kuyaona hayo, ahsante

Chacha! ahsante

Najua wajua! namshukuru Mungu kuwa watu wamenikubali. Ahsante

Maisara! ahsante sana!

Markus. Awe pia nawe. Amina.

emu-three! Sina la kuongeza zaizi ya Ahsante sana ndugu yangu na ipo siku tutaonana.

Kaka Shaban! umenina neno hapo ahsante.