Sunday, August 1, 2010

Malezi ya Watoto Katika Mpango wa Mungu!!!!

Malezi bora kwa watoto


Watoto ni kitu cha thamani sana ambacho Mungu anawazawadia watoto wake kadiri apendavyo yeye. Inashangaza sana kuona watu wanavyosahau kuwa watoto wametoka kwa Mungu na wanapaswa walelewe kwa upendo na misingi ya neno la Mungu na badala yake wanawaona kama ni mzigo. Jinsi unavyomlea mtoto tangia akiwa bado mdogo kabisa ndivyo unavyoyajenga maisha yake ya baadaye.
Kwanza kabisa yakupasa uifahamu thamani ya mtoto ambaye Mungu amekupatia. Umhesabu kama zawadi toka kwa Mungu na sio mzigo hata kama haukupangilia kuwa naye kwa wakati huo maana Mungu alishamfahamu kabla hata hajazaliwa. Katika vitabu vya Yeremia na Zaburi tunaona kuwa Mungu anayafahamu maisha ya kila mtoto kabla hata mimba yake yaijatungwa.
Yeremia 1:5a Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa;
Zaburi 139:16 Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; chuoni mwako ziliandikwa zote pia, siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado.
Tambua kuwa Mungu amekuheshimu na kukupendelea kwa kukupa watoto/ mtoto ili umlee na kumtunza, kwa hiyo yakupasa umpende na kumlea kwa hekima ya ki Mungu na hata siku moja usimuone kama mzigo au kumsema vibaya kwa watu wengine. Hata kama mtoto wako atakuwa na mapungufu kitabia wewe kama mzazi unayemjua Mungu na unaitambua thamani ya mtoto uliyenaye, usimseme vibaya kwa watu bali umuombee, kumuelekeza kwa upendo na kumuonya kwa busara. Fahamu kuwa mtoto wako anathamani kubwa mbele za Mungu naye ndiye anayemjua vyema. Wewe kama mzazi unawajibika mbele za Mungu kwa jinsi unavyomlea mtoto wako ha hivyo yakupasa kujitoa kwa uaminifu katika kumlea kwa upendo na uvumilivu wote.
Tafuta kulifahamu neno la Mungu na kuitafuta hekima ya kiMungu katika malezi ya mtoto wako kuliko hekima ya mwanadamu. Jifunze Mungu anasema nini kuhusu malezi ya watoto na uyafuate hayo kwa uaminifu hata kama kibinadamu yanaonekana yamepitwa na wakati. Tumia muda kwenye maombi kumwombea mtoto wako na maisha yake ya kimwili na kiroho ili aweze kuongozwa na Mungu siku zote za maisha yake. Mfundishe mtoto wako tangia akiwa na umri mdogo habari za Mungu na kweli yote ya neno la Mungu. Katika maisha ya siku hizi ni kawaida kuona baba na mama wote wanafanya kazi nje na nyumbani hali inayopelekea watoto kubaki na mlezi muda mwingi wa mchana. Hali hii usipoiwekea mikakati katika malezi ya mtoto wako kiroho inaweza kuleta madhara makubwa hapo baadaye. Hakikisha muda unaoupata kuwa na mtoto wako unautumia kumweka karibu nawe na kumfundisha habari za Mungu.
Kuna njia nyingi ambazo mzazi unaweza kuzitumia katika kumfundisha mtoto wako habari za Mungu kwa ufanisi kuanzia katika umri mdogo kabisa. Anza kwa kuomba na mtoto wako wakati wote iwe ni asubuhi, wakati wa kula, usiku na wakati mwingine wowote ambao unafanya maombi. Mfundishe kuwa ni muhimu kuomba kabla ya kula na kulala na pia asubuhi baada ya kuamka. Kwa kufanya hivi mara kwa mara basi taratibu ataaza kuona kuwa maombi ni kitu cha muhimu na kadiri anavyokuwa mkubwa ataendelea na tabia ya maombi. Biblia katika kitabu cha mithali inasema mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee. (Mithali 22:6).
Msimulie hadithi za biblia kwa njia ya kufurahisha huku ukiwa unamsomea biblia. Mwanzoni itakuwa ngumu kukuelewa lakini kadiri unavyoendelea na kurudia rudia mara kwa mara itakaa ndani yae na itamjengea hamu ya kusoma biblia ili ajue kwa undani zaidi habari ambazo unamsimulia pale atakapokuwa anajua kusoma. Ukiweza mtafutie biblia ya watoto yenye hadithi fupifupi za biblia kwa picha. Waweza pia kutafuta video za hadithi za biblia kwa watoto na mkawa mnaangalia pamoja naye huku ukimsimulia , pamoja na kupata nafasi ya kumfundisha neno la Mungu pia utapata muda mzuri wa kufurahi na mtoto wako na kuwa karibu naye.
Mfundishe kuonyesha shukrani pale mtu anapompatia kitu au kumtendea jambo jema. Hata kama hajui kuongea mwambie sema asante hii itamfundisha kuwa ukitendewa jambo ni lazima kuonyesha shukrani. Mfundishe kumshukuru Mungu kwa kuamka salama, kupata wazazi wanaomlea vyema, kununuliwa michezo mbali mbali, n.k Moyo wa shukrani utamsaidia kumjua Mungu zaidi na atakuwa anatafuta mema ya kumshukuru Mungu kila siku. Ishi maisha ya upendo, furaha, amani na ukarimu wakati wote ili mtoto aone uhalisia wa Mungu katika maisha yako.
Nenda na mtoto wako kanisani kila jumapili na uwe unamwambia kwanini unaenda kanisani. Usisahau kumpa sadaka naye awe anatoa na umweleze kwa nini tunatoa sadaka kuwa ni njia ya kumshukuru Mungu kwa vingi alivyotupatia. Kumbuka kila mara kumkumbusha upendo wa Mungu, wema na ukuu wa Mungu.
Malezi ya mtoto ni huduma inayojitosheleza, ni jukumu ambalo umuhimu wake ni mkubwa sana na pale unapokosea matokeo yake kuyabadilisha huwa ni kazi ngumu sana. Mwamini Mungu katika jambo hili na mtegemee na kumtazamia yeye pekee, kama alivyokupa mtoto atakuwezesha kumlea katika njia impasayo.
–Magreth Riwa–

Habari hii nimeipata hapa nikaona si vibaya kama nikieweka hapa katika blog ya Maisha na Mafanikio ili wengi tujifunze. PIA NACHUKUA NAFASI HII KUWATAKIENI JUMAPILI HII YA KWANZA YA MWEZI WA NANE IWE NJEMA SANA. MWENYEZI MUNGU AWE NANYI NA BARAKA ZAKE ZITAWALE NYUMBANI MWENU!!!!!!

7 comments:

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

aksante kwa ujumbe murua kwa sana.

uwe na wakati mzuri kabsaaa!

Matha Malima said...

NASHUKURU KWA MADA NZURI YA J PILI ITANISAIDIA HATA KUFUNDISHA KATIKA KANISA LANGU KWA WATOTO WADOGO KWAKWELI MNAJALI SANA JAMII ASANTE SANA MAISHA MAFANIKIO.

mdoti Com-kom said...

Nimeipenda sana hii lakini imekuwa ndefu mno. Yaweza kuwa ni tatizo langu binafsi ila huku bongo mtandao sio availabo kiviiiiiileeeee!

Mungu na akubariki maana ni ujumbe mzuri. Wakati mwingine tupe vipande vipande

PASSION4FASHION.TZ said...

Asante kwa kutusaidia ujumbe mzuri,unatupa msukumo kwa kuwafundisha watoto wote.

Yasinta Ngonyani said...

Nawashukuruni wote kwa mchango wenu na karibuni zaidi na zaidi- watoto wanahitaji maisha mema.

Anonymous said...

Dada Yasinta,

Mimi ni kawaida yangu kuchelewa kutoa maoni.
Na hapa nitatoa maoni yangu yanayochangamana na Science. Da yasinta, Mimba ikiisha tungwa, Mungu anamficha mtoto ndani ya bahari salama, sehemu iliyo jaa virutubisho vyote. Hapa, mama hawezi kumnyima mwanae chochote, na mara nyingi mtoto anakula kabla mama hajala (simaanishi anapewa undigested food). Chakula alichokula mama kikiisha kuwa tayari virutubisho bora vinaenda kwa mtoto. Kadiri mtoto anavyokuwa, Mungu anamtangaza mtoto huyu kwa kumweka mbele (tumbo linasongea mbele- haliendi nyuma) na ulimwengu wote huona. sasa inakuwaje mtoto akizaliwe anawekwa mgongoni badala ya kifuani?
Ujumbe muhimu hapa ni kuwa mtoto anatakiwa kuwa mbele,sio nyuma na saa zote yupo salama mikononi mwa wazazi, sio wasichana wa kazi au ndugu wengine. Mtaniwia RADHI KAMA UJUMBE WANGU NI TATA.

cytotec said...

obat telat bulan i think your blog very informative obat penggugur thanks for sharing obat cytotec