Thursday, April 28, 2016

MAPOSENI SEKONDARI WANAFUNZI WAWILI WANALALA KITANDA KIMOJA


Shule ya sekondari ya Maposeni iliyopo  katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma inakabiliwa upungufu mkubwa wa vitanda hali inayosababisha wanafunzi wawili wawili kulala katika kitanda kimoja.
Shule hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa mabweni ya kulala kufuatia idadi kubwa ya wanafunzi wanaoletwa  kuanza kidato cha tano hali iliyosababisha baadhi ya madarasa kubadilishwa matumizi na kuwa  mahali pa kulala.
Risala ya wanafunzi wa shule hiyo iliyosomwa na wanafunzi Ezekiel Kazeni na Prudensia Kitusi katika mahafali ya saba ya kidato cha sita katika shule hiyo imezitaja changamoto nyingine zinazoikabili shule hiyo kuwa ni kutokamilika kwa ukumbi wa chakula,mikutano na mitihani yaani multipurpose hall.
Kwa mujibu wa risala hiyo changamoto nyingine ni upungufu wa nyumba za watumishi ambazo zipo nane tu kati ya nyumba 48 zinazohitajika hali iliyosababisha walimu wengi kupanga mbali na eneo la shule.
Mkuu wa shule hiyo Dismas Nchimbi alizitaja changamoto nyingine kuwa ni uchakavu wa majengo ya shule,nyumba za watumishi,ofisi na vyumba vya madarasa kwa kuwa majengo hayo ni ya zamani ambayo yalijengwa mwaka 1987 wakati shule hiyo inafunguliwa.
“Kukosekana kwa maji ya uhakika ni changamoto kubwa ambapo shule hutegemea maji ya visima tu ambayo ni ya msimu na hayakidhi mahitaji ya idadi ya wanafunzi 903 waliopo hivi sasa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita’’,alisema.
Pamoja na changamoto hizo Nchimbi alisema shule hiyo imepata mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu ya kutoa elimu bora kwa mujibu wa Matokeo Makubwa Sasa ambapo shule hiyo imeweza kufaulisha  wanafunzi wa kidato cha sita kwa asilimia 100 kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015.
Mafanikio mengine ameyataja kuwa ni shule imefanikiwa ujenzi wa bwalo la chakula ambalo limeezekwa hata hivyo ametoa wito kwa wadau mbalimbali kusaidia kukamilisha ujenzi huo na kwamba shule ina mradi wa ufyatuaji wa tofali zinazotumika katika miradi ya ujenzi ambapo hadi sasa tayari tofali 105,000 zimefyatuliwa lengo likiwa wanafunzi kuwafundisha elimu ya kujitegemea.
Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 218 kati yao wavulana 131 na wasichana 87 walitunukiwa vyeti vya kuhitimu.Shule ya sekondari ya Maposeni ilianza rasmi mwaka 1987 na kutoa wahitimu wa kwanza wa kidato cha nne wapatao 53 mwaka 1990 ambapo kidato cha tano kilianza rasmi mwaka 2008.
CHANZO:- KWIRINUS MAPUNDA
Mwisho

No comments: