Thursday, April 28, 2016

JINSI YA KUPIKA MABUMUNDA/MIKATE YA NDIZI!

Nimekaa hapa huku nikuota/kumbuka jinsi tulivyokuwa watoto na tulivyoanza mapishi kwa mfano hiki chakula  cha makte wa ndizi/mabumunda  kule Lundo tulikuwa tukipika sana na hata kujipatia tusenti twa kununua pipi:-) Haya karibu  labda nawe kuna chakula ambacho ulianza kupika ulipokuwa mtoto..... NI HIVI:-

MFANO WA MABUMUNDA
MABUNDA ni aina ya chakula cha asili cha Afrika ambacho ni rahisi kukiandaa. Pia kinajulikana kama MKATE WA NDIZI Kwa lugha nyingine.Ni chakula kilicho katika mfumo wa mkate ila hiki upikwa na ndizi na unga wa mahindi.

MAHITAJI
> Ndizi mbivu zilizoiva vizuri au hata kukaribia kurojeka.

> Unga wa mahindi ila nzuri zaidi kama utatumia unga wa dona.

> Jani la mgomba.

JINSI YA KUPIKA

Menya ndizi zako na uziweke katika kinu kidogo kisha ziponde hadi zilainike na kuwa uji uji.Baada ya hapo,zitoe ktk kinu na weka katika bakuli kisha changanya unga wa mahindi hadi mchanganyiko wako ukolee.

Osha jani la mgomba vizuri na ulipitishe ndani ya moto ili lilainike.Kisha kata jani la mgomba vipande na chukua ule mchanganyiko wako wa unga na ndizi na uuweke katika jani la mgomba vizuri kisha ulisokote.

Weka katika sufuria au chungu na ubandike jikoni katika moto mkubwa kiasi.Funika na mfuniko wa chuma na juu paria moto kama unavyopika waki.

Subiri kwa dakika kumi au kumi na tano na ugeuze bumunda lako.Baada ya kuiva litakuwa gumu,hivyo tegua na ondoa mabaki ya majani ya mgomba na uache bumunda lako lipoe.

FAIDA ZAKE

=Ni chakula kinachodumu kwa muda mrefu bila kuharibika (kuchacha).

=Hakina madhara ya kemikali kama mikate ya viwandani.

Unaweza kula wakati wowote,waweza kunywa na chai au hata uji, pia usisahau juice AU tu maji

"Onyesha ufahari kwa kula vyakula kwa kula vyakula vyenye asili ya mtanzania"

Maswali na ushauri vinaruhusiwa.....TUPO PAMOJA!

MAPOSENI SEKONDARI WANAFUNZI WAWILI WANALALA KITANDA KIMOJA


Shule ya sekondari ya Maposeni iliyopo  katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma inakabiliwa upungufu mkubwa wa vitanda hali inayosababisha wanafunzi wawili wawili kulala katika kitanda kimoja.
Shule hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa mabweni ya kulala kufuatia idadi kubwa ya wanafunzi wanaoletwa  kuanza kidato cha tano hali iliyosababisha baadhi ya madarasa kubadilishwa matumizi na kuwa  mahali pa kulala.
Risala ya wanafunzi wa shule hiyo iliyosomwa na wanafunzi Ezekiel Kazeni na Prudensia Kitusi katika mahafali ya saba ya kidato cha sita katika shule hiyo imezitaja changamoto nyingine zinazoikabili shule hiyo kuwa ni kutokamilika kwa ukumbi wa chakula,mikutano na mitihani yaani multipurpose hall.
Kwa mujibu wa risala hiyo changamoto nyingine ni upungufu wa nyumba za watumishi ambazo zipo nane tu kati ya nyumba 48 zinazohitajika hali iliyosababisha walimu wengi kupanga mbali na eneo la shule.
Mkuu wa shule hiyo Dismas Nchimbi alizitaja changamoto nyingine kuwa ni uchakavu wa majengo ya shule,nyumba za watumishi,ofisi na vyumba vya madarasa kwa kuwa majengo hayo ni ya zamani ambayo yalijengwa mwaka 1987 wakati shule hiyo inafunguliwa.
“Kukosekana kwa maji ya uhakika ni changamoto kubwa ambapo shule hutegemea maji ya visima tu ambayo ni ya msimu na hayakidhi mahitaji ya idadi ya wanafunzi 903 waliopo hivi sasa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita’’,alisema.
Pamoja na changamoto hizo Nchimbi alisema shule hiyo imepata mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu ya kutoa elimu bora kwa mujibu wa Matokeo Makubwa Sasa ambapo shule hiyo imeweza kufaulisha  wanafunzi wa kidato cha sita kwa asilimia 100 kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015.
Mafanikio mengine ameyataja kuwa ni shule imefanikiwa ujenzi wa bwalo la chakula ambalo limeezekwa hata hivyo ametoa wito kwa wadau mbalimbali kusaidia kukamilisha ujenzi huo na kwamba shule ina mradi wa ufyatuaji wa tofali zinazotumika katika miradi ya ujenzi ambapo hadi sasa tayari tofali 105,000 zimefyatuliwa lengo likiwa wanafunzi kuwafundisha elimu ya kujitegemea.
Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 218 kati yao wavulana 131 na wasichana 87 walitunukiwa vyeti vya kuhitimu.Shule ya sekondari ya Maposeni ilianza rasmi mwaka 1987 na kutoa wahitimu wa kwanza wa kidato cha nne wapatao 53 mwaka 1990 ambapo kidato cha tano kilianza rasmi mwaka 2008.
CHANZO:- KWIRINUS MAPUNDA
Mwisho

Tuesday, April 26, 2016

NIMETAMANI SANA HIVI VYAKULA VYETU VYA ASILI/TULIVYOKUA NAVYO

 Nimekaa hapa nikiyafikiria matembele kwa ugali wa muhogo, lakini  duh  nimebaki kumezea mate tu...nikaanza kuota ndoto ya
...mahindi ya kuchoma hasa yale yanayochomwa moja kwa moja katika mkaa halisi wa kuni....mmmhhh maisha ....HAYA JAMANI KILA LA KHERI...PANAPO MAJALIWA...

Monday, April 25, 2016

TUANZE JUMATATU HII KWA KUANGALIA WANYAMA KATIKA MBUGA TOFAUTI AFRIKA/TANZANIA

 Hapa ni Pundamilia hawa si wakali sana ni kama vile farasi tu ....
 Hawa wanaonekena wazuri na wapole lakini ukikutana nao hawana huruma maana  watakuona kitoweo ..SIMBA. Nilipokuwa nikiishi Madaba/matetereka kulitokea simba na wakawa wanasema ya kuwa tusiogombe ya kwamba simba hali watu. Mie sikuwaamini ....sijui nilikuwa mwoga mno???
 Tembo huwa wana hasira za haraka sana au sijui za ziada pia....
TWIGA WA MANYARA
Hakuna wanyama niwapendao kama TWIGA... wana mwendo wa maringo  na ukizingatia wana shingo ndefu pia miguu Yao mirefu. Je wewe una mnyama umpendae?

Saturday, April 23, 2016

AFRIKA- KUMEKUCHA.....


NAWATAKIENI MWISHO MWEMA WA JUMA.... PAMOJA TUTAFIKA......KAPULYA

Thursday, April 21, 2016

PICHA YA WIKI:- UNAKUMBUKA HII MIAKA ILEEEE

Nina uhakika hii itarudi tu. Maana yote ya kale yanarudi sasa... yaani hii ilikuwa kila aliyekuwa na pasi alikuwa nayo na kama huna unaenda kwa jirani/rafiki na kunyoosha hivyo...Je? ww uliwahi kunyoosha shati lako hivyo?

Wednesday, April 20, 2016

WATU NA MAENDELEO YETU...TUMETOKA MBALI

 Nakumbuka sana mtindo huu wa jiko la kuni na mafiga matatu. Tumetumia sana hadi kuwa hivi tulivyo kwa kila Aina ya mapishi....
 Pia nakumbuka majiko haya pia, marehemu mama yangu alikuwa mtundu sana alikuwa akiweza kutengeneza kwa matofali na udongo jiko kama hili...ingawa hili hapa ni la sementi....lilikuwa linatunza sana moto na matumizi ya kuni yalikuwa madogo.......
Na sasa baadhi wanatumia majiko/jiko kama haya /hili lakini hapa mwenzangu mimi kaona ya kale ni bora ...Nimependa hii kwa kweli kwa namna fulani.

Tuesday, April 19, 2016

UJUMBE WA LEO: HASIRA

UNAPOSHINDWA KUSAMEHE KWA AJILI YA HASIRA
" Hasira ni kichaa cha muda, ni moto ambao huchoma kila kitu na kukigeuza majivu" Mahatma Gandhi.
Tupunguze hasira ndugu zanguni. WOTE MNAPENDWA.!!

Monday, April 18, 2016

TUANZE HII WIKI KWA KUUTEMBELEA MJI WETU SONGEA: TATIZO LA MAJI LAPELEKEA WANANCHI KUHARA DAMU ....

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkenda Songea Vijijini, Mkoani Ruvuma, mpakani mwa Tanzania na Msumbiji wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji na kulazimika kunywa maji yanayopatikana kwenye vidimbwi na maji ya Mto Ruvuma na hivyo kukumbwa na magonjwa ya kuharisha.

Friday, April 15, 2016

IJUMAA YA LEO:- NIMEKUMBUKA/TAMANI MLO HUU NDIZI KWA NYAMA....

 Nimekaa hapa nhuku nikikumbuka chakula hiki NDIZI NYAMA/NDIZI KWA NYAMA  ni moja ya vyakula vya asili nivipendavyo sana ukiacha samaki kwa ugali:-) IJUMAA NJEMA NDUGU ZANGU!

Thursday, April 14, 2016

NI WIMBO LAKINI UNA UJUMBE MZITO KWA JAMIÍ UKIPATA WASAA SIKILIZA


Huu ni wimbo maalum kwa ajili ya kupinga mimba za utotoni ambao umefanywa na Witnesz Kibonge Mwepesi pamoja na Ochu Shaggy. PAMOJA TUTAFIKA TU!

Wednesday, April 13, 2016

LEO TUELEKE MBINGA KUANGALIA MAENDELEO YA UJENZI YA NYUMBA/KIBANDA YETU/CHETU


Ile nyumba/kibanda yetu ya Mbinga imefikia hapa na hata mazingira  sasa yanaanza kupendeza hapo tumejaribu kupanda mahindi na viazi vitamu/mbatata ...safi eehh:-9
 Na hapa ni migomba ya ndizi ...Karibuni tutaongea mengine hapa.
Mazingira yanazidi kubadilika kila siku ziendevyo...hapa ni mbogamboga ...za maboga..Tutaendelea kufuatilia maendeleo ya Nyumba/kibanda hiki...

Monday, April 11, 2016

JUMATATU HII TUANZE HIVI! UNYWAJI WA TANGAWIZI NA FAIDA ZAKE KUMI UTAKAZOPATA UKIANZA KUNYWA LEO...!!

1. Huondoa halafu mbaya ya kinywa:-
Tofauti na vyakula vingine kama kitunguu swaumu. Tangawizi husaidia uwe na halafu nzuri pale unapopumua na kufanya maeneo ya mdomo kuwa safi.
2. Msukumo wa damu:-
Tangawizi husaidia msukumo wa damu mwilini kwa sababu huupa mwili joto ambalo mara nyingi mwili huhitaji wakati wa usukumaji wa damu mwilini
3. Huondoa magonjwa ya asubuhi:-
Licha ya kuwa tiba ya magonjwa kama kikohozi na mafua, tangawizi pia husaidia kupunguza magonjwa ya asubuhi kama uchovu na mninginio. Kwa akina mama wajawazito, tangawizi huwapunguzia homa za asubuhi wanapoamka, pia hutumika kama kichocheo cha utulivu.
4. Mfumo wa chakula:-
Husaidia mwili kunyonya virutubisho kwenye chakula. Hii husaidia sana pale unapoamua kupunguza uzito wa mwili na kupata virutubisho vilivyo muhimu.
5. Kurekebisha sukari ya mwili:-
Tangawizi husaidia katika kuweka sawa kiwango cha sukari kwenye damu. Wagonjwa wa kisukari wanashauriwa kutumia tangawizi badala ya chai.
6. Hamu ya kula:-
Huongeza hamu ya kula chakula. Kwa wale wenye mfumo mbaya wa umengényaji wa chakula wanashauriwa kutumia tangawizi ili kupata mfumo mzuri wa mmengényo wa chakula.
7. Uzalishaji wa mate:-
Tangawizi  husaidia uzalishaji wa mate mdomoni. Kuongezeka kwa mate mdomoni husaidia kutengeneza vichocheo muhimu vinavyosaidia wakati wa kula na kupunguza  uwezekano wa magonjwa ya meno.
8. Kuyeyusha mafuta
Tangawizi husaidia kupunguza kuganda kwa mafuta mwilini ambayo yana madhara makubwa mwilini. Hasa magonjwa ya kiharusi na shinikizo la damu.
9. Kuondoa sumu mwilini:-
Tangawizi husaidia kupunguza kichefuchefu na kutapika. Pia husaidia sana kwa wale watu waliotumia sana madawa na kuwa na sumu nyingi mwilini.
10. Tangawizi humsaidia mtu mwenye vidonda vya tumbo kwa kupunguza maumivu na hata kuponya vidonda hivyo kama vitakuwa kwenye hatua ya awali sana.
PANAPO MAJALIWA!!!

Sunday, April 10, 2016

SEMINA KWA WANAFUNZI WA KITAWA KATIKA JUMUIYA YA WATAWA HANGA

Mwezi Machi, wakati wa msimu wa Kwaresima, shule zetu tatu za kitawa (novisi) kutoka  Benediktini ya jumuiya ya watawa ya Hanga, Mgimwa na Peramiho walikutana katika jumuiya ya watawa Hanga kwa ajili ya semina ya wiki moja. Pia kulikuwa na novisi/watawa kutoka jimbo la Mtakatifu Paul iliyopo  Lighano katika  jimbo kuu la Songea. Mwalimu wa semina hiyo alikuwa sista kutoka St Getrude Convent wa Imiliwaha katika Jimbo la Njombe . Hakika, ilikuwa ni fursa kubwa kwa vijana hawa kuwa na muda wa kuomba kwa pamoja kijamii na chakula cha kiroho. Sisi sote tulipata moyo kuona vijana hawa katika malezi, matumaini  ya baadaye ya jamii zetu za kidini. Mungu awabariki!

Friday, April 8, 2016

PALE TUNAPOYACHUKULIA MAISHA KIRAHISIRAHISI

Kama utayachukulia maisha kuwa ni dharura ni wazi utakuwa unakasirishwa hata na vitu vidogovidogo. Unapohisi kwamba, unaelekea kwenye kukasirika, unapaswa kujiambia au kujikumbusha kwamba, maisha siyo dharura. Kuyachukulia maisha kuwa siyo dharura ni pamoja na kujua kwamba, migogoro ya kimaisha ni jambo la kawaida na haiwezi kuepukika. Kujua kwamba, kukasirika hata siku moja hakuwezi kutatua matatizo yetu, badala yake hutuingiza kwenye matatizo makubwa zaidi kimwili na kiakili.
CHANZO:- KITABU CHA MAISHA NA MAFANIKIO

Thursday, April 7, 2016

RANGI AZIPENDAZO KAPULYA......KIJANI

Hii rangi ni moja ya rangi nizipendazo. Sasa hapa hata sketi, gauni wala suruali  hakuna sijui itakuwaje .....Na hicho kiatu sijui nitafika niendako kweli..... ???

Tuesday, April 5, 2016

MADENGE ATAKA KUMPOSA BIBI YAKE KWA VILE BIBI ANAMWITA MCHUMBA....

Leo nimekumbuka  kitu ni kwamba babu yangu alipenda sana kuniita mchumba Wake na pia bibi yangu alikuwa akiwaita kaka zangu wachumba zake. Nilikuwa nikijiuliza sana inakuwaje  hii? Nilipata maelezo kiasi na nikaridhika ingawa ilinipa sana utata. Haikuishia hapo kulikuwa na  dereva mmoja  ambaye alikuwa rafiki wa familia naye alipenda sana kuniita mchumba hapo ndio nikabaki nimechanganyikia kabisa, nadhani nilichanganyikiwa kama MADENGE...hebu msome yeye alivyowaza kuhusu bibi yake..... Si mnakumbuka hadithi  ya Madenge darasa la .....

Je? hapa ni utata wa lugha au ndiyo mila na desturi zetu?  WOTE MNAPENDWA NA TUPO PAMOJA!!

Monday, April 4, 2016

WIKI HII IMEANZA VIZURI KWANGU:- NIMETUMIWA ZAWADI ZA VYAKULA NIVIPENDAVYO:-)

 Kwanza Samaki kutoka  huko Mwanza ...jina nimesahau
 Halafu kumbikumbi
Na mwisho  ni BOGA  kwa kweli nimefurahi sana sana maana ni haswa baadhi ya vyakula nivipendavyo ambavyo naweza nikala kila siku bila kuchoka:-) Je? Wewe unayesoma/angalia hapa una chakula pia ukipendacho sanaaa? JUMATATU NJEMA KWA WOTE!!

Saturday, April 2, 2016

MITINDO YA NYWELE KWA AKINA DADA/MAMA.....

Nimejiuliza sana hivi huu mtindo ukisuka itakuwaje kulala? Duh ama kweli ukitaka kupendeza yabidi uvumilivu....JUMAMOSI NJEMA KWA WOTE. .....Ngoja nijiandae nami nisuke huu mtindo ila nahisi mchana na usiku kwandu itakuwa sawa ...hakuna kulala:-)