Tuesday, September 30, 2014

KAMA MNATAKA MALI!!!!


Nadhani wengi hasa mlio na umri wangu mnakumbuka kitabu hiki au vitabu hivi ya TUJIFUNZE LUGHA YETU. Leo nimekumbuka shairi hili...haya fuatana nami......

Karudi baba mmoja, toka safari ya mbali,
Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili,
Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali,
Wakataka na kauli, iwafae maishani.

Akatamka mgonjwa, ninaumwa kweli kweli,
Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali,
Roho naona yachinjwa, kifo kinanikabili,
Kama mwataka kauli, semeni niseme nini.

Yakawatoka kinywani, maneno yenye adili,
Baba yetu wa thamani, sisi tunataka mali,
Urithi tunatamani, mali yetu ya halali,
Sema iko wapi mali, itufae maishani.

Baba aliye kufani, akalibi lile swali,
Ninakufa maskini, baba yenu sina hali,
Neno moja lishikeni, kama mnataka mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali,
Baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili,
Akili yetu nyembamba, haijajua methali,
Kama tunataka mali, tutapataje shambani?

Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli,
Fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali,
Haya sasa burianai, kifo kimeniwasili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili,
Mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili,
Na watoto kwa umoja, wakakumbuika kauli,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Fumbo wakatafakari, watoto wale wawili,
Wakakata na shauri, baada ya siku mbili,
Wote wakawa tayari, pori nene kukabili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali,
Tangu zile za mibuni, hata zitupazo wali,
Na mvua ikaja chini, wakaona na dalili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Shamba wakapalilia, bila kupata ajali,
Mavuno yakawajia, wakafaidi ugali,
Wote wakashangilia, usemi wakakubali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakawanunua ngómbe, majike kwa mafahali,
Wakapata na vikombe, mavazi na baiskeli,
Hawakuita pombe, sababu pombe si mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali,
Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali,
Walikiweka kibao, wakaandika kauli,
KAMA MNATAKA MALI, MTAYAPATA SHAMBANI.
NA HAPA NI MWISHO....!!!!

5 comments:

NN Mhango said...

Karudi dada mmoja toka taifa la mbali
Kachana moja kwa moja na kuunawilisha mwili
mashoga zake wakaji ili awape habari
Kama mnataka maisha, jua ni mafanikio. Da Yacinta hiki kitabu na vingine kama hivyo nina usongo navyo. Niliviagiza Afrika nikatumia garbage inayotumika sasa mshuleni kuharibu watoto wetu. Kama una mtu anayeweza kuvipata kuanzia cha la nne hadi saba nifanyie mpango nitamlipa gharama zake zote.

Yasinta Ngonyani said...

Mwl. Mhango usikonde ngoja nitakufanyia mpango utacipata tu

NN Mhango said...

Mungu akuzidishie kwa upendo wako. Ombi langu ukilisoma vizuri si kimoja bali vine yaani kuanzia la nne hadi la saba au vipi? Nataka vitegemezi vyetu visivyojua hata Kiswahili lau vione vitabu vilivyotuchonga na kuwa tulivyo. Shukrani sana dada yangu. Wfiyo atafurahi hakuna mfano!

Editha Theodory said...

Asante kwa kumbukumbu nzuri dada.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Mhango nimekupata sana ni vitabu vingapi unahitaji...Nitajitahidi niwezavyo!
Editha! kwanza karibu sana Maisha na Mafanikio...Pia ahsante kwa mchango wako.