Monday, September 23, 2013

SIMTAKI......UAMUZI MZITO!!!

Leo nimeamaka nikiwa nikiwaza habari ambayo niliwahi kusoma.....Ilikuwa saa 11 jioni. Msichana mmoja kwa jina la Veronika alikuwa akitoka shuleni kwake. Alikuwa kidato cha nne. Alikuwa anaelekea kwenye shule ya Sekondari ya wavulana. Ilimbidi amwone Robert, rafiki yake wa kiume. Veronika alikuwa akifikiri moyoni: "Sina budi kumwona Robert leo. Siwezi kusubiri tena"

Wakati huo huo huo wavulani walikuwa wakitoka shuleni pia. Punde si punde alimwona Robert akitoka katika kikundi cha wavulana wengine akimji. Alikuwa akitabasamu lakini Veronika aliweza kuona kwamba Robert alikuwa na mshangao pia kumwona yeye pale. Kwa kawaida walikuwa wanakutana kwenye stendi ya basi. Na maongezi yaliendelea hivi:-

ROBERT: Habari za jioni  Veronika? Nina furahi kukuona .

VERONIKA: Sijambo, Robert ....ah.....Ninataka kuzungumza nawe. Je? kuna mahali pa faragha shuleni kwako- mahali ambapo tunaweza kukaaa na kuzungumza bila mtu kutubugudha?

Robert alimtazama kwa fadhaa kidogo lakini hakumuuliza zaidi.

ROBERT: Ndiyo, nadhani tunaweza kwenda kule maktaba. Leo ni ijumaa na ni mwanzo wa pumziko la wiki, hatuna masomo. Nina hakika hapatakuwa na mtu.

Veronika alimfuata bila kusema kitu. Waliketi mwishoni kabisa mwa chumba cha maktaba wakimpa kisogo mfanya kazi wa makataba ambaye alikuwa akishughulika na kadi za vitabu.

ROBERT: Kuna matatizo gani Veronika? Mbona unaonekana kuwa na wasiwasi na huzuni?

Veronika alimtazama Robert, halafu aliinamisha kichwa .

ROBERT: Veronika kuna nini? huna budi kuniambia unajua mimi ni rafiki yako. Unahofu nini? labda umeshindwa mrihani wako wa katikati ya muhula?
Veronika: Hapana Robert. Ni kitu kikubwa kuliko hicho.... Ni ...nina mimba.

ROBERT: Nini? Una uhakika?
Robert alishikwa na bumbuwazi. Mawazo mengi yalipita ghafla akilini mwake.

VERONIKA:  Ndiyo, nina hakika. Lakini simtaki. Robert, simtaki mtoto huyu. Wazazi wangu wakisikia juu ya jambo hili hawatanipokea tena nyumbani kwetu. Pia itakuwa ni mwisho wa masomo yangu. Unajua, mwaka kesho ningeanza masomo ya uuguzi.

ROBERT: Najua.....Utafanya nini sasa? Ninaona njia moja tu: Ondelea mbali "kitu" hicho.

Veronika alifikiri:"kitu" hicho ni mtoto. Moyo wake ulikuwa unamwambia kuwa alichokuwa anapanga sasa ni jambo  baya sana. Lakini Veronika hakustahimili ile aibu wala wajibu wa tendo lake. Sasa alikuwa amekata shauri.

VERONIKA: Ninajua nitafanya nini. Nitakwenda kwa rafiki yangu Sarah. Yeye ni muuguzi kule hospitalini. Nitamwomba anipatie dawa ya kuondoa mimba, nina hakika atanisaidia. Hakuna mtu mwingine atakayejua. Hapo maisha yataendelea tena kama mwanzo.
Maneno haya ya mwisho Veronika aliyasema kwa sauti ya kunongóneza. Robert alikuwa ameshika kichwa chake kwa mikono yake miwili naye hakuthubutu kumtazama Veronika. Yeye pia alitambua kuwa anahusika lakini alifikiri: "Kwa kweli, hakuna njia nyingine, au sivyo? Hakujua. Lakini Veronika alikuwa amekwisha amua tayari. Basi, alimuuliza tu....

ROBERT: Utakwenda kumwona rafiki yako lini?

VERONIKA: Kesho......

Inasikitisha kweli kuona jinsi hali hii inavyorudiwa rudiwa mara nyingi siku hizi. Katika namna zoto za maisha kutoa mimba kumekuwa ni jambo la kawaida, jambo linalotokea mara kwa mara. Magazetini huandika kinaganaga jinsi watoto wanavyookotwa kwenye mapipa ya takataka, katika vyoo vya uma, n.k. Kutoa mimba kunaonekana kama njia ya kuondoa kitu kisichotakiwa ; njia ya kusahau kitu ambacho kisingelikuwa kimetokea.....ITAENDELEA......Habari hii nimeipata katika kitabu cha NJIA YETU KWA MAPENDO NA NDOA...



6 comments:

Anonymous said...

Kwa kweli inasikitisha sana vijana kutoa mimba. Hii inaweza kusababishwa na mafunzo duni shuleni na nyumbani kuhusu dini na mambo ya kujamiiana (ngono zembe). By Salumu.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Salumu...kwa kweli inasikitisha sana ukizingatia kuna wengine hawawezi kupata watoto na wanatoa hadi pesa ili kupata mtoto na wengine wanatupa .....

Justin Kasyome said...

Lol!

ray njau said...

Haya ni maangamizi ya halaiki au............................???

emu-three said...

Hii sijasiki hata siku moja ikikemewa kuwa ni UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU....eti jamani mlishawahi kusikia, au huyu hatambulikani kama binadamu

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mie naona tatizo la vijana wengi ni kukosa malengo ya baadaye katika maisha. Wote tulipitia haya ila tulichagua ima dunia au yale tuliyotaka kufanikisha. Nakumbuka vizuri. Nilimaliza form four bila kujua mambo haya. Sasa watoto wanaanza mambo haya tangu shule za msingi unategemea nini? Sie kipindi kile tulionekana washamba. Ukituona tulivyofanikiwa sasa utajua kumbe ushamba wetu ulitusaidia. Kinachosikitisha ni kichanga kisicho na hatia. Ila kwa wahusika sina uchungu nao wala silaumu mfumo zaidi ya suala hili kuwa la mtu binafsi kulingana na malengo yake ya baadaye maishani. Kama unataka kuwa mtu wa maana baada ya kupata elimu. Mara nyingi huwa nawashauri vijana kutoruhusu kichwa cha chini kishinde nguvu kichwa cha juu. Kamdudu hako hata ukalishe vipi hakatosheki na hakana shukrani zaidi ya kukuongezea matatizo na kuvuruga ndoto zako za baadaye. Tieni akilini.
Kazi kwa vijana wetu kuanza kufikiri mbali badala ya kuangalia maisha pale walipo.