Monday, February 4, 2013

MKE MWEMA NI UTULIVU NA NEEMA.......

KATIKA PITAPITA MTANDAONA NIMEKUTANA NA SHAIRI HILI NIMELIPENDA NI TAMU NA NIKAONA NISIWE MCHOYO NIWEKE HAPA...KARIBUNI
--------------------------------------------------------------------------------------------------
1.Mke mwema utulivu, hili halina Ubishi
Anakutoa machovu, ya kazini kama moshi
Hana chembe ya uvivu, kila kitu hash hashi
Mke mwema utulivu, ndio raha ya dunia.

2. Ni raha juu raha, nyumbani ukibakia
Wala hamna karaha, bashasha hunawiria
Huna haja ya kuhaha, baridi roho hukaa
Mke mwema utulivu, ndio raha ya dunia

3. Kidogo kwake chatosha, hakuna kudangadanga
Na hakuna mshawasha, hata upande wa kanga
Mahaba hunawirisha, japo kibaba cha unga
Mke mwema ni neema, ndio raha ya dunia

4. Na munapoambizana, hukaa na kusikia
Hafanyi hata kuguna, ishara ya kuchukia
Nyuso zina ng'ara sana, na watu huulizana
Mke mwema ni neema, ni fahari ya dunia

5. Na mume awa hakongi, majirani hushangaa
Kwa nini jamaa dingi, a shine na kung'aa
Siri chini ya mtungi, hataki hata umbea
Mke mwema ni neema, ndio pepo ya dunia

6. Na hapendi vijishoga, mara huku mara kule
Na hana muda wa soga, kila siku yuko mbele
Hapendi kuigaiga, kila kitu kwa sumile
Mke mwema rah a sana, kila mtu alijua

7. Na hata kwenye kibanda, mutaishi kwa murua
Na japo kupanda punda, msimamo hushikia
Hakuna kupinda pinda, na nyuma kufikiria
Mke mwema ni neema, mola akikujalia

8. Utulivu huwa moyo, si mali wala magari
Wangapi waliyonayo, kukicha haweshi shari
Asubuhi wenda myayo, usiku kucha ngangari
Mke mwema ni neema, Muume akiwa nayo

9. Tabia haifundishwi, mtu hujengeka nayo
Na mtu hababishwi, hiyo huwa mwenendoyo
Ni vibaya havipishwi, nafsi huwa na choyo
Mke mwema ni neema, kiumbe ukiwa nayo

10. Kukicha yananawiri, miaka nenda ishapita
Wala husikii kwiri, hutembea na kunyata
Shamsham bila shari, wajukuu washapata
Maisha huwa matamu, mke mwema kuwa nae.

11. Na ukipata mkorofi, atakutoa kipara
Kukicha hwishi makofi, na hakuna masikhara
Hugombana na mawifi, ajae humcharara
Mke mwema ni neema, na ni raha ya dunia.

6 comments:

ray njau said...

Urithi kutoka kwa akina baba ni nyumba na mali lakini mke mwenye busara hutoka kwa Yehova._Methali 19:14

Yasinta Ngonyani said...

wengi husema mwanamke ni maua/mapambo ya nyumba .....

ray njau said...

Hakika mwanamke ni zaidi ya waridi katika nyumba yenye utulivu na maelewano kati ya wawili ambao kwa ridhaa na mapendo yao waliamua kuyamwaga kila mmoja katika sakafu ya moyo wa mwenzake na kwa siku yake cherekochereko za walisema haoi sasa kaoa,walisema haolewi sasa kaolewa .........na lizombe kwa pamoja:"Ninapopenda mimi ni hapo tu x2.................

Mija Shija Sayi said...

Mimi nasubiri shairi la mume mwema..

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Ray! ulichosema hapo juu ni kweli kabisa...ngoja niongezeee kidogo:- Mwanamke haitakiwi apigwe ngumi,Mwanamke anatakiwa kuongozwa kwa upendo, Ukimpenda atanyenyekea, ukimpenda utamwongoza. Lakini ukimpiga hayo hayatatokea. Mtuze mke naye atakutunza. Mweshimu aye atakuheshimu.

Mija! Wala usikonde:-)

ray njau said...

Biblia inasema “kichwa cha mwanamke ni mwanamume.” (1 Kor. 11:3) Daraka la mwanamume akiwa kichwa cha familia linatia ndani nini? Maandiko yanasema hivi kuhusu daraka moja la kichwa cha familia: “Ikiwa yeyote hawaandalii mahitaji wale walio wake mwenyewe, na hasa wale walio washiriki wa nyumba yake, ameikana imani naye ni mbaya kuliko mtu asiye na imani.” (1 Tim. 5:8) Kwa kweli, mwanamume anapaswa kuiandalia familia yake mahitaji ya kimwili. Hata hivyo, ili aisaidie familia yake kukaa macho kiroho, ni lazima afanye mengi zaidi kuliko tu kuwapa mahitaji ya kimwili. Anahitaji kuijenga familia yake kiroho, na kuwasaidia washiriki wote wa familia kutia nguvu uhusiano wao pamoja na Mungu. (Met. 24:3, 4)