Thursday, November 18, 2010

BADILIKA, JIONDOE AU KUBALI ILI UISHI.

Huwezi kupingana na hali halisi

Yapo makosa matatu ambayo mtu huwezi kuyafanya bila kujua athari zake. Makosa hayo ni kulaumu, kuunga mkono na kulalamika. Makosa ambayo mtu anaweza kuyaepuka kwa kuona ukweli kwamba ni yeye anayewajibika kwa nafasi yake.

Lipo swali moja kubwa ambalo watu huuliza, nalo ni: ‘Ni vipi nitadhibiti kile kinachonitokea ama kile watu wengine wanachoweza kusema ama kufanya?’ Jibu ni wazi, nalo ni kwamba huwezi kudhibiti kile kinachokutokea.

Kitu pekee uwezacho kudhibiti ni jinsi unavyokabiliana na hali iliyopo mbele yako. Wapo wanaopenda kukabiliana na matatizo yao kwa kulaumu watu wengine ama kujaribu kuunga mkono na kutetea kile ambacho wao walifanya kabla ya hali hii kutokea, ama kulalamika kuhusu hali hiyo.

Uamuzi wa kubadili, kuacha ama kukubali hali iliyopo ndilo jibu sahihi la makosa matatu ambayo watu hufanya.

Ni wazi, chaguo hili linatakiwa kufanyika tu wakati unapokuwa kwenye hali usiyoipenda. Unawezaje kuamua kuachana ama kubadili hali ambayo kwako wewe imezoeleka? Watu wengi wanafanya hivyo na mara nyingi bila kujua. Wakati unapojikuta kwenye hali usiyoipenda, fikiria mambo haya matatu kabla ya kuanza kulaumu, kushutumu ama kujilazimisha kukubali:

BADILI: Unapojikuta kwenye hali usiyoipenda, unaweza kufanya jitihada za kuibadili au kubadili mtazamo wako kuhusu hali hiyo . Ikiwa uko katika uhusiano unaodhani haukusaidii kwa mfano, unaweza kwenda kwa washauri nasaha, unaweza kuzungumza na mwenzi wako na kujaribu kuufanya uhusiano huo uwe bora zaidi ama waweza kubadili mtazamo wako wa namna uhusiano wenye faida unavyotakiwa kuwa.

Mara nyingi huu ni uchaguzi mgumu sana kuufanya kwa sababu inaweza ikalazimu kumkabili mtu mwingine kutoka katika tabia isiyo na faida kwako. Kubadilika kunatuondoa kwenye nafasi yetu tuliyoizoea na ambayo tunaiona inatufariji na kunahitaji ujasiri mkubwa kufanya hivyo.

Kuamua kuacha kumtegemea mpenzi kukupa furaha na kutafuta furaha kutoka vyanzo vyenye kuaminika zaidi siyo jambo rahisi, lakini ni muhimu.

JIONDOE: Kama umeshindwa kubadili hali kwa sababu yoyote ile umeshindwa kumfanya mtu abadili tabia yake kwa mfano,ni bora kujiondoa, ondoka kabisa.
Kujiondoa kunakufanya uondokane na hali isiyofurahisha na kunasafisha njia kwako kwa ajili ya kuchagua jambo jingine mbadala.

Ni wazi,watu wengi hukimbilia kuchagua njia hii, hukimbilia kujiondoa kwa sababu huogopa sana kujaribu njia ya kwanza ya kubadili hali ama kubadilika wao wenyewe.

Lakini ingawa kukimbilia hatua hii bila kujaribu ya kwanza si busara, kuna wakati ambapo kujiondoa ni hatua pekee ifaayo kuchukua. Hata hii nayo inahitaji ujasiri mkubwa kwa sababu, mara nyingi akili zetu hutuweka katika nafasi ya kutumia methali ya ‘Zimwi likujualo’ kama utetezi wa kuendelea kuvumilia madhila yasiyo muhimu tunayokumbana nayo.

KUBALI: hatua ya mwisho unayoweza kuchukua kukubali. Ziko hali ambazo huwezi kuzibadili na kukwepa ukweli wa jambo hilo, ni sawa na wendawazimu. Hebu mfikirie mfungwa wa kisiasa kama ilivyokuwa kwa mzee Nelson Mandela wa Afrika Kusini na wenzake.

Wakati alipokuwa akishikiliwa jela, asingeweza kuibadili hali ile, wala asingeweza kuamua kuondoka. Hakuna jingine aliloweza kufanya ila kukubali hali halisi na kufanya kila analoweza kuishi katika hali hiyo.

Kuna wakati kukubali linakuwa ni chaguo la kwanza tunalopaswa kuelekeza macho yetu, wakati tukiwa tunafikiria njia bora ya kubadili hali au kujiondoa.

Nina hakika kila mtu anapotazama mambo yanayozunguka maisha yake, atakutana na moja ambalo haridhishwi nalo kwa asilimia 100. Utafanya nini kushughulikia hilo, utajaribu kubadili hali au mtazamo wako wa hali? Uko tayari kujiondoa ikiwa una hakika huwezi kubadili hali au uko tayari kubadili mtazamo wako kuhusu jambo hilo ili uweze kuendelea nalo? Uko tayari kukubali kile ambacho huna uwezo wa kukibadili na wala huwezi kujiondoa?

Nafasi ni yako kutumia busara zako kuchagua.

Kumbuka, maisha unayoishi ni chaguo lako mwenyewe, ingawa ni vigumu kuliona na kukubali jambo hilo.
Makala hii nimeitoa kwa kaka Shabani kaluse. nimeipenda na nimeona si vibaya kama tukirudia tena si mnakumbuka au mnajua kuridia kitu ndo kujifunza zaidi.

4 comments:

emu-three said...

Nimeipenda hii makala, ahsante kwa kutodondolea hii !

Unknown said...

Dondoo kamilifu! Ahsante dada Yas kwa kutupakulia!

Simon Kitururu said...

Imeenda shule hii kitu!

Upepo Mwanana said...

Lakini sisi binadamu ni wabishi, wabinafsi na kutokukubali kushindwa, ndio maana ugomvi auishi na kuwa mabingwa wa kuwanyooshea vidole wengine huku nasi tukiwa ni taka kuliko tunaowanyooshea vidole