Wednesday, April 7, 2010

Maisha ya uzeeni/Kuishi nyumbani au kituo cha kulelea/kutunzia wazee!!!



Nasi twaelekea huku!!!



Makala hii hapa chini http://tustaarabike.blogspot.com/2010/04/nikionacho-darubini.html nimeipenda ndiyo maana nikaamua kuichukua na kuiweka hapa kwangu kwani taratibu za huko Marekani ni sawa na za hapa Sweden Nami nataka kuongezea ni . Nashukuru kwa kuiweka hii mada -
Kwani najua nakamilisha lengo lake la kuifanya isomwe na wengi. Ni hivi hata mimi nilikuwa nikijiuliza hivi kwanini watu hapa Sweden, kila wakati wanaonekana wapo na shughuli tu kiasi kwamba wanashindwa hata kuwatunza wazazi wao- Kwa nini hawapo karibu sana na wazazi/ndugu zao.

Sijui kama ningeweza kumpeleka mmzazi wangu kwenye kituo cha kulelea/kutunza wazee. Napenda zaidi utamaduni/mila zetu za kiafrika na naomba Mungu tusiige kabisa tamaduni/mila hii. Sijui ni tabia gani? Maana kuna wengine ukiwauliza ni lini wameenda kuwasalimia mama/baba zao wanasema mwaka jana kweli huu ni upendokweli?

Zaidi soma hapa nimevutiwa na hii makala hii na nimeona niwaonyeshe na wenzangu ili tujadili kwa pamoja.


Nikionacho kwenye darubini.......



Nimekaa nimejiinamia huku mawazo kibao yakiwa yamenizonga. Nilimtupia jicho la haraka binti yangu mdogo ambaye ndio kwanza katimiza tumiezi kadhaa karibia na nusu mwaka. Mojawapo ya swali lililonizonga ni je kweli binti huyu na dada yake watanipeleka katika vituo vya kulelea wazee (nursing homes) pindi nitakapokuwa mzee na sijiwezi? Heh! Mungu na apishie mbali walah mimi nitaenda kuzeekea nyumbani kwetu bongo, labda nitazeeka kwa heshima astahiliyo mzee.
Kwa wale ambao hamjanipata vema nitawaelezea ili nanyi muelewe ni nini hasa kinachonikera. Hapa Marekani kama nchi nyingi za Ulaya kuna kasumba ya kuwapeleka wazee wasiojiweza katika vituo vya kulelea wazee. Vituo hivi vinaendeshwa kwa mfumo wa utoaji huduma za afya na masuala mengineyo. Wazee huishi katika vituo hivi na kupata huduma zote za kijamii na kuangaliwa kwa karibu afya zao. Chimbuko hasa la vituo hivi ni kutokana na mfumo wa kiuchumi uliopo katika maisha ya familia ya kila siku. Familia nyingi huwa ziko bize na maisha ya kila siku. Wengi makazini na wengine katika biashara huku wajukuu wakiwa wameshatawanyika aidha kwenda mashuleni au kuhamia majimbo mengine. Sababu hizi na zinginezo nyingi husababisha wanandugu kukaa na kuamua kuwapeleka wazazi wao katika vituo hivi.
Lengo huwa ni zuri tu kwasababu kama hauna nafasi ya kumtunza baba au mama yako ( dah!) pengine shangazi au mjomba na kuna sehemu ambayo kwa malipo ya bima basi atatunzwa basi ni vema kufanya hivyo. Lakini tatizo linakuja wapi??? Tatizo ni pale ambapo wazee hawa wanapogundua kuwa its about time. Hakuna anayependa kutenganishwa aidha kutoka nyumbani kwake na kwenda sehemu ngeni ifananayo na hospitali na kugundua wanatakiwa kupaita nyumbani. Wazee hawa hudhoofika kiafya haraka sana kwani hawaipendi hali hii na mara zote huonekana wamekuwa depressed. Magonjwa ya akili mara nyingi huwaandama na kuathiri afya zao na kusababisha urahisi wa kushambuliwa na magonjwa mengine. Kumbuka unapokuwa depressed muda wote huathiri kinga ya mwili hivyo kusababisha magonjwa kukushambulia kirahisi. Hali hii husababisha wazee wengi kudhoofika na hata kama walikuwa wazima vipi! Ni hoja tu jamani...
Tukirudi upande mwingine, vituo hivi vya kulelea wazee huendeshwa kwa mtindo wa kibiashara hasa chini ya mfumo wa kibepari. Faida kubwa ndio lengo na si vinginevyo. Ahadi kem kem hutolewa na pia kuna sheria maalum za kuwalinda wazee hawa. sheria hizi zimetungwa na serikali na zingine zimetungwa na majimbo. Vema basi kuna sheria kibao za kuwalinda wazee alright? Wrong! Kwanini basi nasema hivyo? Wale ambao wamepata kufanya kazi kwenye vituo hivi watakubaliana nami kuwa wazee hawa hunyanyaswa sana na wafanyakazi. Manyanyaso haya husababishwa na hasira za wafanyakazi kwa kufanyishwa kazi za watu wawili watatu bila hiari yao. Upungufu wa wafanyakazi katika vituo hivi ni jambo la kawaida kabisa ambalo huelekea kukosekana kwa ufanisi na morali za kufanya kazi. Mara nyingi upungufu huu husababishwa na mishahara midogo wanaolipwa wafanyakazi au menejimenti ipuuzavyo masuala ya ajira. tatizo hili husababisha wafanyakazi kubadili mwajiri kila mara hivyo vituo kukosa wafanyakazi wa uhakika. Utakuta kisheria mtu anatakiwa labda ahudumie wazee wanne mpaka watano kwa ufanisi lakini kutokana na upungufu basi mtu huyo huyo atapewa watu kumi mpaka kumi na tano wa kuwahudumia na hivyo kusababisha ufanisi kutoweka. Wafanyakazi mara kadhaa hasira zao huzimalizia kwa wazee hawa ambao maskini ya Mungu hawastahili haya kwani ni akina babu na bibi zetu na wanastahili mema toka kwetu. Hili ni tatizo sugu ambalo wamiliki wa vituo haliwasumbui sana kwani kwao ni faida kubwa sana kimapato. Familia nyingi zinafahamu tatizo hili na mara nyingi watembeleapo vituo hivi hutaka kujua rashio ya wafanyakazi (staff ratio).
Ninawaza sana, bora tu mfumo wetu wa nyumbani kwetu bongo. Tuendelee kuwalea wazee wetu na kuwathamini kwani ndio waliotufikisha hapa tulipo. Mfumo wa umimi na amerikani drimu usituingie kamwe kwani baadae utakuja kuturudi na kujikuta tunapambana na wanetu ili watupe haki yetu ya kututunza kwani nao tuliwatunza...

7 comments:

Markus Mpangala. said...

Siyo siri naogopa kuzeeka. Lakini kuhusu vituo vya kulea, mie sina neno

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

Turejee katika ujima au?

Kwani hapo zamani kulikwa na vituo vya kulelea watoto/wazee?

Unknown said...

Ng'wanambiti katika ujima wazee ni treasure katika jamii. je ulishawahi kusikia usemi usemao mzee akifariki ni sawasawa na kuchoma moto maktaba? Utajijua Lol!!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

siku hiz mambo yamebadilika na wazee hawana dili tena. wamejaa laana na lawama kwa watoto wao. ole wenu mtakaoishi mpaka uzeeni

mimi kulea wazee bado najiuliza na kujishauri sana

Koero Mkundi said...

Kamala, watch your language...eti wazee nini?
basi kwa taarifa yako labda wazee wa huko BK kwenu, lakini kwetu bado wanazo busara tena za kutosha tu.
Natamani nikukutanishe na bibi Koero, utashangazwa na hekima alizo nazo.

naomba uombe radhi kwa kauli yako hiyo...Loooo.....

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

@koero, sidanganyikii mimi na laana zako. sihitaji sana baraka zao wala busara zao. I can make it on my own

Anonymous said...

hi mpendwa!umenigusa sana na kwa hili,mimi nafanya kazi kama hizo hapa uk,uliyoyasema nikweli tupu,sitamani haya mambo yafike huko nyumbani.Kama mfanyakazi hizi unahitaji upendo zaidi kuliko pesa,kuna watu wanaongeza masaa ya kufanyakazi zaidi sasa anakuwa kachoka sana na anafanya usiku basi usiku wote analala,hawa wazee wanaita mpaka analia wakati mwingine mfanyakazi kalala,na wengine wakuwa na njaa si unavyojua huku cup of tea mzee analala,pia kuna waafrika wapo kwenye hizi home wao asilimia kubwa hawashibi,basi akikuona uko zamu anakuwa na furaha sana kwani anajua leo atalala vyema,yaani siwezi kumaliza yote hapa naomba niishie hapo,Mungu atusaidie na nifanye hii kazi kwa upendo zaidi kuliko tamaa.asante sana.